Habari za Punde

Mhe Hemed akutana na Mwanasheria Mkuu Dk. Eliezer Feleshi

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla akibadilishana mawazo na Mwanasheria Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Eliezer Feleshi aliefika Afisini kwake Vuga Jijini Zanzibar kujitambulisha kufuatia kuteuliwa kwake na Rais Samia Suluhu Hassan hivi karibuni.

Na Kassim Issa, OMPR

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla amesema usimamizi wa sheria zilizopo nchini ni moja ya misingi ya kuwaletea maendeleo kwa wananchi wake.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alieleza hayo alipofanya mazungumzo na Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Eliezer Feleshi alipofika kujitambilisha ofisini kwake vuga Jijini Zanzibar.

Alisema ana imani kuteuliwa kwake mwanasheria huyo kushika nafasi hiyo kutaweza kuisaidia Serikali katika kusimamia misingi ya kikatiba na utawala bora katika kuijenga Tanzania.

Mhe. Hemed alisema uwepo wa wanasheria wabobezi kutawapa nafasi ya kuishauri Serikali kuwa na sheria madhubuti hasa katika kipindi hichi cha kuzifanyia mapitio sheria hizo.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alimuhakikishia Dk. Feleshi kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itatoa kila aina ya ushirikiano na kueleza kufurahishwa kwake kuona wanakuza mashirikiano na Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar.

Alisema umefika wakati wanasheria hao kuhamasisha vijana kuingia katika fani ya sheria kwa moyo thabiti wa kulitumikia taifa kizalendo na kusema kuwa Tanzania inahitaji usimamizi na kuilinda sheria katika kueletea nchi maendeleo.

Mhe. Hemed alimueleza Mwanasheria Mkuu huyo kuwa, katika kupiga vita madawa ya kulevya Serikali inategemea zaidi ushauri wa wanasheria kuweza kupata sheria zitakazosaidia kudhibiti kadhia hiyo inaendelea kupoteza nguvu kazi ya vijana.

Kwa upande wake Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Eliezer Feleshi alimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kuwa ujio wake hapa Zanzibar mbali na kujitambulisha lakini kuna lenga kuongeza kasi katika kupanga namna bora ya kupata sheria zitakazoendana na kasi ya serikali ya awamu ya nane katika kukuza sekta ya uchumi wa buluu nchini.

Alisema kukuwa kwa uchumi wa Zanzibar kunahitajika wanasheria wabobezi watakaoenda sambamba na kukuza uchumi wa nchi.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.