Habari za Punde

Wanafunzi Wapatiwa Mafunzo Kujenga Uwelewa Dhidi ya Udhalilishaji

Kamishna Tume ya Haki za Binaadamu na Utawala Bora Amina  Talib akizungumza na wanafunzi   wakati wa mafunzo ya kuwajengea uelewa juu ya ukatili na udhalilishaji kwa wanawake na  watoto yaliyofanyika UKumbi wa maleria Mwanakwerekwe Zanzibar.

Na  Khadija Khamis –Maelezo,   12/10/2021.

Kamishna wa Tume ya Haki za Binaadamu na Utawala Bora Amina Thalib Ali amesema ukatili na udhalilishaji wa kijinsia dhidi ya wanawake na watoto humuathiri mtendewa wa vitendo hivyo  kiakili  kimakuzi na kimalezi pamoja  na kupelekea kuipoteza haki yake ya elimu ipasavyo. 

 

Alisema vitendo hivyo ambavyo vinaendelea kushamiri  hapa Zanzibar huathiri vijana ambao ndio tegemeo la taifa la kesho .


Aliyasema hayo katika mafunzo ya haki za binaadamu na utawala bora yaliyofanyika katika ukumbi wa Malaria Mwanakwerekwe, ambayo yaliwashirikisha wanafunzi mbali mbali kutoka skuli za msingi na sekondari zilizopo wilaya ya magharibi A  na B.


 Aidha alisema jumla ya kesi 868 zilizoripotiwa kwa mwaka huu na 567 ni za watoto wa kike sawa na asilimia 68 jambo ambalo linarejesha nyuma maendeleo ya taifa.


Kamishna huyo aliwataka wanafunzi hao kueleza matatizo mbali mbali wanayokumbana nayo  katika jamii ili kutafutiwa ufumbuzi muafaka kupitia tume hiyo kwa lengo la kuzishauri serikali zote mbili kutokana na changamoto hizo zinazojitokeza.


Kwa upande wa wanafunzi hao walisema uelewa mdogo wa wazazi na walezi katika jamii kuhusu vitendo vya ukatili na udhalilishaji wa kijinsia unapelekea vitendo hivyo kuzidi kuengezeka.


Walisema kutokana na umasikini na hali duni ya maisha ,mporomoko wa maadili kwa kuziacha mila desturi na tamaduni za awali pamoja  na matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii huchangia kuwa na tamaa kwa wanafunzi na hupelekea kufuata ushawishi na ulaghai ambao huchangia vitendo hivyo.


Nao Wanafunzi hao  walitoa wito kwa wazazi na walenzi kuwa karibu na watoto wao kwa kuwapa ushauri na mbinu za kuepukana na vitendo hivyo vinavyowapotezea ndoto zao.


No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.