Habari za Punde

Ndondo Kucheza Mapinduzi Cup ? Hapana.!

Na.Ally Saleh Alberto Zanzibar.

Waswahili husema "LISEMWALO LIPO," na hili lisemwalo sasa naona lipo njiani linakuja.

Uvumi ulianza kuenea jana kuwa kuna mjadala au sijui ndio maamuzi kwamba mabingwa wa Yamle Yamle watashiriki Kombe la Mapinduzi mwakani. Au sijui pia ni kuendelea au vipi.

Kwa kweli kama ilivyo ndondo basi pia Mapinduzi si mashindano  rasmi. Makombe yote mawili ni ya mshikizo tu na hayana ulazima katika mfumo wetu unaoendesha mpira chini ya ZFF.
Ni majuzi tu ZFF imekuwa ikipigia kelele  kuhusu hizi "kombe za ndondo" ambazo kwa sababu moja au nyengine ndio zinazozaa washabiki wengi viwanjani, imani ya watu, ili kujaza ombwe. 
Kujaza washabiki ni kitu kimoja, lakini sidhani "kombe hizi" zinasaidia makuzi ya soka au kukuza vipaji. Ni kama kukufuru kuwa mpira wa bichi Copacabana, Rio de Janeiro, na utamu wake huibua vipaji.
Nionavyo ma star ndio hustawisha soka la Copacabana na hata hapa kwetu wanaocheza ndondo tayari wana majina kwa daraja yoyote watayokuwa wanacheza tayari. 
Sasa baina ya ndondo zote inachaguliwa ya Yamle Yamle ndio itoe timu ya kushiriki Mapinduzi Cup. Kwa sababu gani, vigezo gani?
Tuyaache hayo na tuje katika Mapinduzu Cup ambayo ipo miaka kadhaa na brand yake ni kabambe shukran kwa wasimamizi.
Nembo hii huleta timu serious na zinazowekeza mamilioni kulea na kutunza wachezaji na zinazoshiriki michuano hiyo zikiwa na malengo.
Ama lengo ni kujijenga kwa kutumia kipindi cha mini pre season, yaani nusu ya pili ya ligi, mfumo ambao uko Ujerumani, au kwa timu, zinazoendelea kimataifa kuwa ni kujitatarisha zaidi. Au kupima na kuunganisha usajili wao wa dirisha dogo kujenga players chemistry. 
Mabingwa wa ndondo watashiriki Mapinduzi Cup kwa malengo gani?
Timu huja Mapinduzi ili zipate mechi za ushindani, jee bingwa wa ndondo kweli atatoa ushindani? Usinijibu kwa ubishi tu. Tulia unijibu kwa utuo. 
Timu ya mtaani tunaipaje dhamana ya nidhamu ya kucheza na vilabu vilivyosajiliwa... Na tukijua uhuni unaopita katika mechi zote za ndondo?
Kama wanaofikiria kutia timu ya ndondo kwa ajili eti watajaza uwanja, au watatia pesa wajue si rahisi timu kama Yanga au Simba kukubali kucheza na timu ya mtaani.
Walioanzisha wazo hilo au hata wanaolifikiria na wanaopanga kulitekeza wajue tunaenda kuichuja Mapinduzi Cup na kuiua kabisa
Mwaka jana nilikutana mpiga picha kutika Poland amekuja maalum kuona Mapinduzi Cup. Sisi Zanzibar tukiwa makini katika utalii tulipaswa kuibrand Mapinduzi Cup kama Tamasha la Busara, kama Zanzibar Film Festival au matamasha kama hayo.
Nionavyo mimi tusiushushe hadhi na  utamu wa Mapinduzi Cup tuibakishe kama ilivyo au tuizidishe kama tulipokuwa tukileta vilabu vya Kenya na Uganda
Kama tunazipenda ndondo tufanye kitu tuite labda Michuano ya Ndondo Kitaifa na mabingwa wa ndondo ( *National Ndondo* *Classic* ) tuwakutanishe na tuwaalike pia wale wa michuano ya Shafii Dauda. Ndondo ya mbuzi, ya n'gombe, ya pilau nk. 
Tuwe na wivu wa kulinda Mapinduzi Cup ndio alama pekee ya Zanzibar kisoka. Kule makombe ya Afrika hata kujamba hatuwahi tushatolewa (ashakum si matusi) ...
Na huku tukitegemea ligi kuu ya Zanzibar itachuchuka tena na kuin'garisha Zanzibar kama zama zileeee ambazo vizazi viwili vya sasa hawajaona. Zama ligi zetu hata za Central zikijaza viwanja.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.