Habari za Punde

Benki ya Dunia Yaridhishwa na Maandalizi ya Utekelezaji wa Mradi wa Tanzania ya Kidigitali.

Naibu Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhandisi Kundo Mathew, akizungumza na waandishi wa habari wakati wa ziara ya ujumbe wa Benki ya Dunia kutoka makao makuu ya benki hiyo Washington Marekani uliotembelea Tanzania, Dodoma kufanya tathimini ya maandalizi ya utekelezaji wa mradi wa Tanzania ya Kidijitali.Kushoto kwake ni Dkt.Tim Kelly ambaye ni kiongozi na mkuu wa Msafara wa ujumbe huo.


Na. Prisca Ulomi, WHMTH                                                                                                                        

Ujumbe wa Benki ya Dunia kutoka Makao Makuu yake yaliyopo Washington DC, Marekani umefanya ziara nchini Tanzania ya tathmini ya maandalizi ya utekelezaji wa Mradi wa Tanzania ya Kidijitali mkoani Dodoma

 

Ujumbe huo umeongozwa  na Dkt. Tim Kelly, Kiongozi wa Ujumbe wa Benki ya Dunia Mradi wa Kidijitali Tanzania ambae leo amekutana na uongozi wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mjini Dodoma na kuzungumza na Naibu Waziri wa Wizara hiyo, Mhe. Maandisi Kundo Mathew, ambaye amemwakilisha Waziri wa Wizara hiyo, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji na Dkt. Zainab Chaula, Katibu Mkuu wa Wizara hiyo pamoja na Menejimenti yake na wanufaika wa Mradi huo

 

Katika kikao hicho, Mhe. Kundo amesema kuwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Wizara hii iko tayari kutekeleza Mradi huo wa miaka mitano ili watanzania waweze kupata huduma za uhakika, za kiwango kinachotakiwa na za gharama nafuu

 

Mhandisi Kundo ameongeza kuwa Mradi huu umekuja muda muafaka kwa kuwa unaendana na Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Miaka Mitano (2021/22 - 2025/26) ambao unatambua kwamba uchumi wa kidijitali unaingia fursa nyingi mpya za kiuchumi na kufungua njia kwa Tanzania kuinuka kidijitali katika kukuza uchumi wake na kuharakisha mageuzi ya kiuchumi huku Sekta ya Mawasiliano ikichukua nafasi kubwa katika Mapinduzi ya Nne ya Viwanda na unalenga kukuza maendeleo ya kidijitali kama kichocheo kikuu cha ukuaji wa uchumi, ukuaji wa viwanda, utengenezaji wa ajira, utoaji wa huduma na ufanisi katika Serikali

 

Naye Dkt. Chaula amesema kuwa Serikali imekamilisha maandalizi ya utekelezaji wa Mradi huo wenye gharama ya dola za Marekani milioni 150 ambazo ni sawa na shilingi bilioni 349 ikiwemo ujenzi wa Ofisi, upatikanaji wa wataalam wazalendo ambao watatekeleza mradi pamoja na uwepo wa Kamati ya Kitaifa ya viongozi na wataalam kwa ajili ya kusimamia na kutekeleza Mradi huo ipasavyo na Wizara iko tayari kuhakikisha kuwa malengo yaliyowekwa yanafikiwa ndani ya muda mchache badala ya miaka mitano ya Mradi huo

 

Naye Mratibu wa Mradi huo, Honest Njau pamoja na Mkurugenzi wa TEHAMA wa Wizara hiyo, wamesema kuwa mradi huo utajengea uwezo wataalam wa TEHAMA nchini, utaboresha miundombinu ya ya TEHAMA, mifumo ya TEHAMA, Anwani za Makazi na Postikodi, miundombinu na mifumo ya vituo vya Huduma pamoja ambapo vituo hivyo vitaongezeka kutoka vituo viwili vilivyopo Dodoma na Dar es Salaam na kufikia vituo 26 vya Tanzania Bara na vitano vya Tanzania Zanzibar ili kuwa na jumla vya vituo 31 vinavyotoa huduma maeneo mbali mbali nchini na utaongeza nguvu kwenye minara 488 ya mawasiliano iliyopo ya 2G ili iwe ya 3G kwa lengo la kuwawezesha watanzania wapate huduma ya intaneti na data badala ya huduma ya sauti na ujumbe pekee kwenye simu zao za mkononi ikiwa ni pamoja na ujenzi wa minara mipya zaidi ya 300.

 

Akiongea kwa niaba ya ujumbe huo kutoka Benki ya Dunia, Dkt. Tim Kelly, Kiongozi wa Ujumbe wa Benki ya Dunia wa Mradi wa Kidijitali Tanzania amesema ziara ya ujumbe huo imelenga kujionea utayari wa Tanzania katika utekelezaji wa mradi huo na wameridhishwa na maandalizi yaliyofanyika.

 

Akizungumza kwa niaba ya wanufaika wa Mradi huo, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Serikali mtandao Mhandisi Benedict Ndomba amesema mradi huo ukikamilika utawezesha huduma ya Serikali mtandao kufikishwa katika maeneo ya pembezoni mwa miji na hivyo kuwezesha utendaji kazi wa Serikali kuwa rahisi zaidi katika ngazi za vijiji na kata.

 

Mradi huo utatekelezwa kwa kipindi cha miaka mitano kuanzia mwaka 2021 hadi mwaka 2025.

 

Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini

Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.