Serikali imetenga jumla ya shilingi
milioni 96,725,600 kwa ajili ya kutoa elimu ya uhifadhi kwa wananchi katika
vijiji 38 vinavyoizunguka Hifadhi ya Taifa ya Burigi-Chato vikiwemo vijiji 10
vya Wilaya ya Biharamulo ili kuondokana na migogoro ya mara kwa mara inayojitokeza kati ya wananchi na hifadhi hiyo
baada ya kuingiza mifugo hifadhini.
Hayo yamesemwa leo bungeni jijini
Dodoma na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja (Mb) alipokuwa
akijibu swali la Mbunge wa Biharamulo Magharibi, Mhe. Eng. Ezra Chiwesela
aliyetaka kujua lini Serikali itatoa elimu ya uhifadhi kwa vijiji hivyo.
Mhe. Masanja amesisitiza kuwa Serikali
imekuwa ikitoa elimu ya uhifadhi kwa wananchi wanaoishi jirani na Hifadhi ya
Taifa ya Burigi-Chato akitolea mfano katika mwaka wa fedha 2020/2021 Serikali
ilitumia shilingi milioni 20,836,200 kutoa elimu ya uhifadhi kwa vijiji 37
vinavyoizunguka hifadhi hiyo na katika Wilaya ya Biharamulo vijiji sita vya
Kiruruma, Nyabugombe, Ngararambe, Kabukome, Katerela na Kitwechembogo.
Aidha, sambamba na hilo, Mhe.
Masanja amesema Serikali itatumia makundi maalum ili kusaidia kusambaza elimu
ya uhifadhi kwa jamii hiyo akitolea mfano viongozi wa dini, wanasiasa na wanafunzi
wa shule za Msingi na Sekondari.
Mhe. Masanja amewaomba Waheshimiwa Wabunge
kuiunga mkono Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kuwaelimisha wananchi juu ya
umuhimu wa uhifadhi na kuepuka kufanya shughuli za kibinadamu katika maeneo ya
hifadhi.
Kuhusu hoja ya Mhe. Chiwesela ya wafugaji kurudishiwa mifugo pungufu baada ya kukamatwa hifadhini na kulipishwa faini ya shilingi laki moja kwa kila ngo’mbe, Mhe. Masanja ameahidi kuwa Serikali itawachukulia hatua watumishi watakaogundulika kudhulumu mifugo ya wananchi.
No comments:
Post a Comment