Habari za Punde

Serikali kuhakikisha watoto waliotoroka wanarudishwa maskuli


 

Na Maulid Yussuf WEMA

MKOA WA KASKAZINI UNGUJA.

Mkurugenzi Idara ya Elimu Mbadala na Watu Wazima bi Mashavu Ahmada Fakih amesema kutokana na kuwepo wimbi kubwa la watoto waliotoroka Skuli, Serikali imeona ni lazima kuhakikisha watoto hao wanarudi Skuli.

Amesema imeonekana wengi wa watoto hao wamekuwa wakidhalilishwa pamoja na kujihusisha na ajira za utotoni hali ambayo inawanyima haki yao ya msingi kikatiba na kupoteza nguvu kazi ya Taifa.

Akizungumza katika mkutano maalumu na Madiwani wa Mkoa wa Kaskazini A na B Unguja, katika ukumbi wa Baraza la Mji Kaskazini B, Kinduni bi Mashavu amesema  mradi wa kuwarejesha watoto Skuli, umekuja kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuhakikisha watoto wote wanapata haki yao ya Elimu, hivyo ni vyema kushirikiana kuunga mkono juhudi hizo.

Amesema utaratibu wa kuwarejesha watoto Skuli haukuanza kipindi hiki, bali umeanza tokea mwaka 2000 ambapo Serikali imeweka Idara Maalum ya Elimu Mbadala na Watu wazima kwa lengo la kuwasaidia vijana waliokosa elimu waweze kuendelea na masomo yao.


Aidha amefahamisha kuwa katika Mkoa wa Kaskazini Unguja, kuna jumla ya watoto 6477 ambao wapo nje ya masomo, hivyo ni lazima Madiwani hao kushirikiana na Masheha, Wakuu wa Wilaya pamoja na wazazi kuhakikisha wanawarejesha watoto hao Skuli.

Mapema akifungua mkutano huo, Mkurugenzi wa Baraza la Mji Kaskazini B, bwana Abrahman Ali Mukhtari amesema mashirikiano ya pamoja yanahitajika katika kuhakikisha mradi huo unafanikiwa.

Amewashauriwazazi na walezi kuwafuatilia watoto katika masula ya masomo katika Skuli pamoja na kuwa karibu na watoto wao ili kuwalinda na masuala mbali mbali yakiwemo ya udhalilishaji.

Akiwasilisha ripoti ya utafiti ya mradi huo mratibu wa mradi huo bwana Mzee Shirazi amesema jumla ya watoto 35732 kwa Zanzibar nzima wapo nje ya mfumo wa masomo idadi ambayo ni kubwa hasa ukizingatia kuwa watoto hao ndio tegemeo kubwa la Taifa.

Amesema, mradi huo unalenga watoto walio na umri wa miaka 7 hadi 14, lakini haimaanishi kama wapo watoto waliokuwa zaidi ya umri huo wasipelekwe, bali ni vyema kuwapeleka ili kuweza kuendelezwa na elimu kwa umri wao.

Amesema mashirikiano mazuri yameanza kupatikana kwani tayari watoto 3200  wamesharudi Skuku ambao tayari wameshasajiliwa rasmi, huku wakiwa na madarasa 82 ya watoto hao.

Pia amesema mradi huo  pia unalenga kuwapa mafunzo Walimu maalumu ambao ni wa kujitolea kuwasaidia watoto hao kwa kuwaweka vizuri ili wasitoroke tena, pamoja na kuwapa posho lao ili kuwasaidia kujiendeleza wao wenyewe kimaisha.

Hivyo amewataka madiwani kutambua kuwa wana nafasi kubwa kuhakikisha mradi huo unafanikiwa, kwa kuweka mikakati madhubuti kuhakikisha wanafanikiwa kwa kushirikiana kwa pamoja ili kufikia malengo.

Wakitoa michango yao Madiwani hao wameshauri kuongezwa kujengwa madarasa mengine mapya japo mawili katika kila Skuli walizozilenga kuwaweka watoto hao, kwani kutengeneza yaliopo yatachangia kuongezeka mrundikano wa Wanafunzi madarasani.

Pia wameshauri kuwepo mazingira rafiki ya watu wenye ulemavu kwani watoto wengi wenye ulemavu hasa wa Mkoa wa Kaskazini wamekuwa wakitoroka kutokana na kutokuwepo mazingira rafiki ya kujifunzia pamoja na kutokuwepo vifaa vya kusomeshea kwa watoto hao.

Hata hivyo wameipongeza Wizara ya Elimu kwa juhudi kubwa wanayoichukua katika kuendeleza utaratibu wa  kuwarejesha Watoto Skuli ili kuokoa  nguvu kazi ya Taifa.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.