Habari za Punde

Mhe Dkt. Saada Mkuya Azungumza na Waandishi wa Habari

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais Mhe Dkt.Saada Mkuya akizungumza na Waadishi wa Habari wa Vyombo mbalimbali kuhusiana na Maadhimisho ya Sherehe za Miaka 58 ya Mapinduzi ya Zanzibar, katika ukumbi wa Sheikh Idrisa Abdulwakil Kikwajuni Jijini Zanzibar , 28-12-2021.

Ndugu Waandishi wa Habari 

Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi ALIAPISHWA RASMI kuwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi tarehe 02/11/2020 NA KUUNDA SERIKALI yenye muundo wa Umoja wa Kitaifa

Kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi alimteua Mhe Othman Masoud Othman kuwa Makamu wa Kwanza wa Rais na Dkt Saada Mkuya Salum aliapishwa kuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais.

Ofisi ya Makamu wa kwanza wa Rais imeanzishwa mwaka 2010 mara Baada ya uchaguzi Mkuu uliofanyika mwezi Oktoba 2010, kiongozi wa mwanzo wa Ofisi hii ni marehemu Maalim Seif Sharif Hamad aliyefariki tarehe 17/ 02/2021 Mwenyezi Mungu ailaze roho yake mahala pema peponi.

MAJUKUMU YA MSINGI YA OFISI

Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais inashughulika na masuala ya sekta mtambuka za Uhifadhi, Usimamizi na Utunzaji wa Mazingira, masuala ya Watu wenye Ulemavu, masuala ya VVU na UKIMWI na masuala yanayohusu Udhibiti wa Dawa za Kulevya. Kimuundo Ofisi ina Majukumu yafuatayo: -

              i.          Kuratibu mambo yote yanayohusu Ofisi ya Faragha ya Makamu wa Kwanza wa             Rais;

            ii.          Kusimamia na kuratibu utekelezaji wa masuala yote ya kisera na  mipango ya                Ofisi wa Makamu wa Kwanza wa Rais;

          iii.          Kuratibu masuala ya Utumishi na Uendeshaji wa Ofisi.

           iv.          Kuratibu masuala ya Watu Wenye Ulemavu;

             v.          Kusimamia masuala ya Mazingira;

           vi.          Kuratibu na kusimamia masuala ya VVU/UKIMWI; na

         vii.          Kuratibu masuala ya Udhibiti wa Dawa za Kulevya.

 Ndugu Waandishi wa Habari

Miaka 58 ya Mapinduzi Zanzibar Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais katika kuratibu Masuala ya Watu wenye Ulemavu

Kabla ya kuanzishwa kwa Idara na Baraza la Taifa la Watu wenye Ulemavu; Masuala ya Ulemavu yalikuwa chini ya Wizara ya afya na Ustawi wa Jamii mwaka 1980-1990s.  Kwasababu kabla ya hapo sote tulikuwa tukielewa kwamba suala la ulemavu lilikuwa ni suala la kiafya na ni suala linalohusu ustawi wa jamii.  Lakini kwa mujibu wa changamoto nyingi zilizokuwa zikitokezea na kuwapata Watu wenye Ulemavu, mfano suala la Udhalilishaji na mengineyo maovu yaliyokuwa yakiwafika Watu Wenye Ulemavu kote ulimwenguni; Serikali ikaona kuwa kuna haja kubwa ya kuliangalia suala hili katika upeo mwengineo.

Idara ya Watu wenye Ulemavu ni Sekretariati ya Baraza la Taifa la Watu wenye Ulemavu ambalo lilianzishwa rasmi na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mheshimiwa Abeid Aman Karume mwaka 2008.  Maamuzi ya kuanzishwa kwa Idara hii yalifanyika kwa kupitia na mujibu wa Sheria Na. 9 ya 2006 ya (Haki na Fursa) kwa Watu wenye Ulemavu pamoja na Sera ya Maendeleo ya Watu wenye Ulemavu ambazo zilitamka kwamba Idara ya Watu wenye Ulemavu ndiyo Sekretarieti ya Baraza la Taifa la Watu wenye Ulemavu na matamko yote haya yametokana na au ni kwa mujibu wa Tamko la Mkataba wa Kimataifa wa Watu wenye Ulemavu wa mwaka 2006.

Idara ya Watu wenye Ulemavu ilipitia katika usimamizi wa Ofisi kadhaa ikiwemo Ofisi ya Waziri Kiongozi, baadae kuhamishiwa katika Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais mwaka 2011-2012 / hadi 2015-2016 kikamilifu.

Baadae tena mwaka 2016 Idara ilikuwa chini ya Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, na mwaka 2020 ikarudishwa tena Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais

Baraza la Taifa la Watu wenye Ulemavu na Sekretarieti yake wanashughuli kubwa ya kuratibu masuala ya ulemavu katika serikali na kijamii kwa ujumla.

Mafanikio mengi yamepatikana tokea kuanzishwa kwa uratibu wa masuala ya Watu wenye Ulemavu ikiwemo ambapo Serikali imeendelea kuimarisha Jumuishi Database inayosajili na kuweka kumbukumbu za Watu wenye Ulemavu ili kuwatambua, kufahamu aina ya ulemavu walionao na kuweka mikakati sahihi ya kuwawezesha kuishi maisha kwa kiasi kidogo cha utegemezi

Serikali imechukua hatua za makusudi kuimarisha njia za watembea kwa miguu katika barabara kuu walkways), ambazo zimesaidia kwa kiasi kikubwa kwa Watu wenye Ulemavu kupunguza vihatarishi vilivyokuwa vikitokea hapo awali na kuwaongezea usalama zaidi wanapozifuata huduma mbalimbali. Kulingana na muongozo wa miundombinu rafiki kwa Watu wenye Ulemavu uliotolewa na Serikali, kumekuwa na marekebisho ya miundombinu kadhaa ambayo yameendelea kufanyika katika majengo hususan ya Serikali. (tuyataje ikiwezekana).

Ofisi yetu imekuwa na mashirikiano mazuri na Jumuiya mbali mbali zilizoanzishwa na Watu wenye Ulemavu pamoja na kuwapatia ruzuku, aidha tumekuwa tukiwapatia visaidizi na vifaa vyenginevyo watu wenye ulemavu kwa Unguja na Pemba kama fimbo nyeupe, mashine ya kuandikia kwa watu wenye ulemavu wa uoni nk

Ndugu Waandishi wa Habari

Miaka 58 ya Mapinduzi Zanzibar Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais kwenye sekta ya Mazingira

Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ilianza kusimamia rasmi shughuli za mazingira kuanzia mwaka 1989 pale ilipoanzisha Idara ya Mazingira iliyokuwa chini ya Kamisheni ya Ardhi na Mazingira na kupelekea kuundwa kwa Sera ya Mazingira ya mwaka 1992, Sera hii ilifutwa na kuundwa kwa Sera ya Mazingira ya mwaka 2013 ambayo ilifuatiliwa na Sheria ya Mazingira 2015.  Kwa kipindi cha kabla miaka ya 1988 shughuli za udhibiti wa mazingira zilikuwa zikisimamiwa na Kamisheni ya Ardhi na Mazingira pamoja na zile Taasisi zinazosimamia mambo yanayohusiana na mazingira zikiwemo Idara ya Misitu, Uvuvi nk.

Mamlaka ya Usimamizi wa Mazingira Zanzibar (ZEMA) imeanzishwa mwaka 2015 chini ya kifungu cha 14 cha Sheria ya Usimamizi wa Mazingira Zanzibar ya mwaka 2015.  Lengo Kuu la Mamlaka ya Usimamizi wa Mazingira ni kusimamia utekelezaji na uzingatiaji wa Sheria, Kanuni, Miongozo na Viwango vya mazingira kwa ajili ya kupunguza uchafuzi na uharibifu wa mazingira.  Mamlaka hii itasimamiwa na Bodi iliyoanzishwa kwa mujibu wa kifungu cha 15(1) cha Sheria ya Usimamizi wa Mazingira Zanzibar 2015.

Idara ya Mazingira ni miongoni mwa taasisi zilizomo chini ya Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais ambayo jukumu lake kubwa ni kuhakikisha kuwa nyenzo za usimamizi wa mazingira (environmental management tools) ikiwa ni pamoja na sera, sheria, kanuni, mikakati na miongozo inakuwepo; kutoa elimu ya Mazingira kwa jamii pamoja na kuratibu masuala ya mabadiliko ya tabianchi Zanzibar.

Baadhi ya mafanikio yaliyopatikana katika masuala ya usimamizi wa mazingira ni kama ifuatavyo:

Kurejesha maeneo yalioathiriwa kutokana na mmong’onyoko wa fukwe na uingiaji wa maji ya chumvi katika maeneo ya kilimo na makaazi, athari zilizosababishwa na mabadiliko ya tabianchi. Ujenzi wa kuta na matuta ya kuzuia maji ya baharí kupanda juu zimejengwa Unguja na Pemba.

Aidha, ukuta wenye urefu wa mita 300 umejengwa katika eneo la baharí ya Mizingani Forodhani na ukuta wenye urefu wa mita 500 unaojengwa katika eneo la Msuka, Pemba ambapo mita 350 tayari zimekamilika. Katika kusimamia matumizi mazuri ya fukwe na bahari, jumla ya hekta 337 za mikoko zimepandwa katika maeneo 23 (13 Unguja na 10 Pemba) ikiwemo Kilimani, Kihinani, Chukwani Kisakasaka, Nyamazi, Ukele, Nungwi, Kiwengwa, Matemwe, Kibele, Michamvi, Jambiani, Paje, Makunduchi kwa Unguja.

Maeneo ya Pemba ni pamoja na Mkoani, Mtangani, Kangani, Wambaa, Kisiwa Panza Pangawatoro, Tumbe, Tundaua, Vumawimbi, Tovuni, Ole Kichanganazi, Makangale, na Kichanjaani.

Aidha kupitia Idara na Mamlaka ya usimamizi wa Mazingira inakusudia kufanya uhakiki katika maeneo yote ambayo yameathiriwa na mabadiliko ya tabia yanchi na shughuli za zinazotokana na binaadamu

Hatua hio itasaidia kufahamu hatua za kuchukuliwa pindipo inapotokezea athari na kutolea mfano wa maeneo yanayohitaji kupandwa miti kwa kufahamu aina miti inayohitajika kwa mujibu wa eneo husika, 

Ndugu Waandishi wa Habari

Miaka 58 ya Mapinduzi Zanzibar Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais kwenye suala la Kuratibu na Kusimamia masuala ya VVU/UKIMWI

Katika kipindi cha miaka 58 ya Mapinduzi ya Zanzibar, Serikali ilichukua jitihada mbali mbali za kupambana na VVU na UKIMWI nchini kama ifuatavyo:

Kuanzisha Kitengo maalum chini ya Wizara ya Afya kilichojulikana kama Kitengo cha Kudhibiti UKIMWI (Zanzibar AIDS Control Program) mwaka 1987. Hii ni kutokana na kwamba kipindi hicho tatizo hili nchi zote duniani walikuwa wanaona kama ni tatizo la afya.

Kwa mnasaba huo elimu kwa jamii hasa miaka ya nyuma ilitolewa sana ambayo ilisaidia katika kudhibiti maradhi haya na imeweza kubaki kuwa chini ya asilimia

Kuanzishwa kwa Tume ya UKIMWI kupitia sheria namba tatu ya kuanzishwa kwa Tume ya UKIMWI ya mwaka 2003.  Baada ya kutanabahi kwamba suala la UKIMWI ni suala linalohitaji nguvu za kila sekta na sio Wizara ya Afya peke yake. Hivyo Serikali ikaamua kuanzisha Tume ya UKIMWI iliyokabidhiwa jukumu la kuratibu mapambano ya UKIMWI kwa sekta zote za Serikali na zile binafsi ambayo kwa sasa ipo chini ya Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais.

Katika kuimarisha uwezo wa nguvu kazi yetu kujiletea maendeleo, tunao wajibu wa kulinda afya ya jamii yetu kuepukana na maradhi thakili ukiwemo UKIMWI. Tume yetu ya UKIMWI Zanzibar kwa kushirikiana na Wizara ya Afya, imendelea kukusanya taarifa za hali halisi ya UKIMWI

Aidha Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais kupitia Tume ya UKIMWI Imeongeza hamasa ya upimaji wa hiari hususan kwa vijana pamoja na kuendelea kuzuia maambukizo ya VVU kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto kwa kuhakikisha kuwa wanawake wajawazito wanahudhuria kliniki na kupimwa afya zao.

Katika kudhibiti maambukizo ya VVU kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto kiwango cha maambukizo chini ya asilimia 5 kinachukuliwa kama ni ishara ya ufanisi katika kuwalinda watoto na maambukizo kutoka kwa mama.

Tume ya UKIMWI inaendelea kutoa elimu na kuhakikisha kuwa jamii inaongeza uelewa juu ya masuala mbali mbali yanayohusu UKIMWI ili kuisaidia jamii kujiepusha na tabia hatarishi zinazochangia kasi ya maambukuzi ya virusi vya maradhi ya UKIMWI

Ndugu Waandishi wa Habari

Miaka 58 ya Mapinduzi Zanzibar Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais kwenye suala la Kuratibu masuala ya Udhibiti wa Dawa za Kulevya.

Ili kuimarisha mapambano ya wimbi la uingizaji, ulimaji, usambazaji na utumiaji wa dawa za kulevya, mafanikio yafuatayo yamepatikana:-

Katika kutekeleza azma ya serikali juu ya kudhibiti uingizaji na matumizi ya dawa za kulevya ndani ya visiwa vyetu, hatua zimechukuliwa ili kufuta sheria iliyokuwepo ya Udhibiti wa Dawa za Kulevya (Namba 9/2009) na kutunga sheria mpya itakayopelekea kuunda Mamlaka itakayokuwa na nguvu za kisheria za kupambana na dawa za kulevya.

Kama tunavyofahamu hivi karibuni Baraza la Wawakilishi tarehe 24 mwezi wa Disemba 2021 limeupitia Mswaada wa Sheria ya Marekebisho ya kuanzisha Mamlaka ya kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya

Mamlaka ambayo itakayokuwa na uwezo wa kupeleleza, kukamata, kuchunguza na hatimae kupeleka Mahakamani mashauri yanayohusiana na dawa za kulevya pamoja na makosa mengine yanayofanana nayo.

Kutokana na taarifa ya hali ya Dawa za Kulevya katika nchi yetu, tatizo la usafirishaji na matumizi ya dawa za kulevya ni kubwa na linahitaji juhudi za pamoja.

Serikali imeendelea kufanya operesheni katika mitaa mbalimbali ikiwemo Kikwajuni, Sogea, Kidongochekundu, Miembeni, Chuini, Jangombe, Migombani, Maeneo ya Mji Mkongwe kwa Wilaya ya Mjini. Mitaa mingine ni pamoja na baadhi ya maeneo ya Makunduchi (Kijini, Miwaleni na Mtegani), Nungwi, Chake Chake, Pujini, Wete na maeneo yote yanayofanyika shughuli za utalii. Doria za mara kwa mara zimeendelea kufanyika na kupelekea kupunguza matumizi na biashara ya dawa za kulevya mitaani na kuimarisha mashirikiano baina ya wananchi na Serikali katika kupunguza wimbi la usambazaji wa dawa za kulevya.

Athari za matumizi ya dawa za kulevya inawapata vijana wetu wadogo ambao bado wako skuli za msingi, sekondari na hata vyuo vya elimu. Hali hii imepelekea Serikali kutoa taaluma juu ya athari ya matumizi ya dawa za kulevya kwa wanafunzi na walimu wa skuli za Unguja na Skuli za Pemba

 WITO KWA WANANCHI

Naomba nitowe wito kwa wananchi wa Zanzibar kuzidisha mshikamano ili tuende sambamba na ukuwaji wa uchumi na maendeleo ya sayansi na teknolojia katika masuala mtambuka, Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais inatarajia kuwa na jamii inayoishi katika Mazingira endelevu, iliyohuru na matumizi ya Dawa za Kulevya, UKIMWI na inayofurahia Haki na Fursa za Watu wenye Ulemavu kwa ajili ya kufikia Uchumi wa Buluu endelevu kwa faida ya wananchi wa Zanzibar. Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais inatoa pongezi na  kumtakia kheri Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi pamoja na Wazanzibari wote katika kuadhimisha miaka 58 ya Mapinduzi Zanzibar.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.