Habari za Punde

NAIC yatakiwa kufikia lengo la kuhimilisha Ng’ombe Milioni 1 kwa mwaka

Na Mbaraka Kambona,

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki amekitaka Kituo cha Taifa cha Uhimilishaji (NAIC) kilichopo Mkoani Arusha kuhakikisha wanafikia lengo la kuhimilisha Ng’ombe Milioni 1 kila Mwaka ili ifikapo mwaka 2025 wawe wamefikia lengo la kuhimilisha  Ng’ombe Milioni 5.

Waziri Ndaki alitoa maelekezo hayo Disemba 29, 2021 wakati akikabidhi Basi jipya kwa kituo hicho ili waweze kulitumia katika shughuli zao za kila siku za mafunzo kwa vitendo na kuwapeleka Wataalamu katika Kambi za Uhimilishaji.

“Niwatake NAIC na Wataalamu waliofundishwa kuhimilisha wahakikishe tunahimilisha ng’ombe milioni moja kama ambavyo lengo letu linatutaka kwa mwaka huu, na usafiri huu tunaoukabidhi leo utusaidie kufikia lengo hilo”, alisema Mhe. Ndaki

Aidha, aliwataka NAIC kutunza vitendea kazi wanavyopatiwa na Serikali ili viweze kuwasaidia kufanya kazi yao kwa ufanisi na kutoa huduma stahiki kwa wananchi.

Aliongeza kwa kusema kuwa wanataka kuona kituo cha NAIC kinarudi katika hali yake ya mwanzo ya kufanya kazi kama ilivyokusudiwa ya kutoa utaalamu wa uhimilishaji wa mifugo hapa nchini.

Awali, Kaimu Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dkt. Bedan Masuruli alisema kuwa Wizara ilitenga kiasi cha shilingi Milioni 100 kwa ajili ya kununua basi hilo ambalo wanatarajia litasaidia kituo cha NAIC kufanya shughuli zao za mafunzo kwa vitendo na kuwapeleka kwa wakati Wataalamu katika Kambi za Uhimilishaji.

Naye, Kaimu Mkurugenzi, Kituo cha Taifa cha Uhimilishaji (NAIC), Dkt. Dafay Bura aliishukuru Serikali kwa kuwapatia basi hilo ambalo litawasaidia kutatua kero yao ya muda mrefu waliyokuwa nayo ya usafiri na kuahidi kwamba watalitunza na kulitumia kwa malengo yaliyokusudiwa.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.