Habari za Punde

Wizara ya Elimu yaifutia usajili Skuli ya Eden kwa kuendeshwa kinyume na sheria

 Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, imeifutia usajili Skuli ya Eden inayomilikiwa na Shirika la Afrika Agape Association kuanzia Januri 3 mwakani.

Hatua hiyo imefikiwa baada ya Wizara kubaini mmiliki wa Skuli hiyo kuendesha Skuli kinyume na sheria,  miongozo na kanuni za Wizara.

Akizungumza na wamiliki wa Skuli hiyo huko Shakani Kaimu Mrajis wa Elimu na Katibu wa Baraza la Elimu Zuwena Mataka Hafidh, amesema kumekuwepo malalamiko mbalimbali  yaliyowasilishwa na wazazi hali iliyopelekea Wizara kuchukua maamuzi hayo.

Ameyataja baadhi ya malalamiko hayo ni pamoja na Wanafunzi wa kislam kutosomeshwa somo la dini ya kislaam na kiarabu, kulazimishwa kujifunza dini ya kikiristo, kutotakiwa kufunga katika mwezi mtukufu wa Ramadhan na Wanafunzi kutoruhusiwa kuvaa hijabu.

Malalamiko mengine  amesema kupandishwa ada bila ya utaratibu, kutokuwa na mashirikiano mazuri baina ya wazazi, walimu na mmiliki wa skuli na mmiliki huyo kuendesha skuli kwa hisia zake binafsi.

Aidha amebainisha kuwa malengo ya Wizara sio kuifutia leseni Skuli hiyo bali ni kuhakikisha inafuata sheria na miongozo ya Serikali katika kuendesha Skuli yao.

Kaimu Zuwena, amebainisha kuwa mmiliki wa Skuli hiyo amekuwa mgumu kufuata sheria na miongozo ya Wizara na kuendesha Skuli yake anavyotaka yeye jambo ambalo halivumiliki.

“Haiwezekani Skuli kuendeshwa bila ya kufuata miongozo ya Wizara kwani tuna skuli 590 hatutakuwa tayari kuona mmiliki yoyote wa skuli binafsi anakwenda kinyume na utaratibu na hatutasita kuchukua hatua,” amesisitiza.

Hata hivyo, amesema Skuli hiyo imekuwa ikifatiliwa mara kwa mara na kupewa maagizo ya kurekebisha kasoro hizo lakini haizingatii maagizo anayopewa na badala yake kuendelea kuendesha skuli kinyume na sheria.

Amesisitiza kuwa skuli yoyote ya binafsi inatakiwa kufuata sheria, miongozo na mambo mbalimbali yanayotolewa na wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar .

Nae Afisa Elimu Taaluma Mkoa wa Mjini Magharibi, Amosi John Henock, amesema toka skuli hiyo kusajiliwa mwaka 2010 imekuwa ikijitokeza migogoro baina ya mmiliki na jamii pamoja na kushindwa kujirekebisha baadhi ya kasoro ambazo alitakiwa kuzifanyia kazi.

Aidha amesema Skuli hiyo imeshawahi kufungiwa na aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi Ayoub Mohammed Mahmoud na kutakiwa kurekebisha kasoro zilizoonekana lakini aliendelea kukaidi.

Amesisitiza kuwa Skuli hiyo haitaendelea kufundisha mpaka pale itakapokubali kwenda sambamba na maagizo ya Serikali katika kuwapatia watoto elimu.   

Amesema hata katiba ya Zanzibar imeeleza wazi kwamba mtu yoyote hapaswi kufanya jambo lolote kwa lengo la ubaguzi wa moja kwa moja ama kwa taathira yake.

Kwa upande wake Sheha wa Shehia ya Shakani bi  Mwanaisha Khamis Rashid amebainisha kuwa mara nyingi amekuwa akikaa na uongozi wa Skuli hiyo katika uendeshaji elimu kwa kufuata miongozo na mitaala ya Wizara lakini hakuifuata.

Nae   mmiliki wa skuli hiyo bwana    Youung Am Kim ameahidi kuheshimu maamuzi ya Wizara ya Elimu ya kutofungua Skuli na hiyo na kuwajuillisha wazazi juu ya suala hilo.

Aidha amesema atahakikisha anafuata sheria ya elimu ya Zanzibar na kuondoa changamoto ambazo zinalalamikiwa kupitia Skuli yake.

Akizungumza kwa niaba ya walimu wenzake Mwalimu Ummy Aga amesema wameweka jitihada binafsi kwa wanafunzi wao kuona wanafanya vizuri katika mitihani yao na kujipima katika ufundishaji lakini kufutwa kwa Skuli hiyo imeondosha ndoto yao kwa Wanafunzi wao.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.