RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la
Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akizungumza na Makatibu Wakuu, Wakurugenzi
na Wakuu wa Taasisi za SMZ, baada ya kumalizika kwa kuwasilishwa kwa Mada mbalimbali
na baadhi ya Makatibu Wakuu, wakati wa mafunzo ya Upangaji wa Vipaumbele,
yalioandaliwa na Taasisi ya Tony Blair pamoja na Shirika la Maendeleo la Umoja
wa Mataifa (UNDP) mafunzo hayo
yaliyofanyika katika ukumbi wa Chuo cha Utalii Maruhubi Jijini Zanzibar
BAADHI ya Wawakilishi wa Taasisi ya Tony Blair
na Makatibu Wakuu,Manaibu Makatibu Wakuu, Wakurugenzi na Watendaji Wakuu wa
Serikali.wakimsikiliza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi
Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi.(hayupo pichani) akizungumza baada ya kusikiliza Mada
zilizowakilishwa na baadhi ya Makatibu Wakuu, katika mafunzo ya Upangaji wa
Vipaumbele yalioandaliwa na Taasisi ya Tony Blair pamoja na Shirika la Maendeleo
la Umoja wa Mataifa (UNDP) yaliofanyika katika ukumbi wa Chuo cha Utalii Maruhubi
Zanzibar.
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali
Mwinyi amesisitiza haja kwa watendaji Serikalini kubadilika na kutofanya kazi
kwa mazoea ili mipango iliyopangwa na Serikali iweze kutekelezeka.
Rais Dk. Mwinyi amesema hayo mara
baada ya kusikiliza mada zilizowasilishwa na Makatibu Wakuu wa Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar katika Mafunzo ya Upangaji wa Vipaumbele, yalioandaliwa
kwa ushirikiano kati ya Taasisi ya ‘Tony Blair’ pamoja na Shirika la Maendeleo
la Umoja wa Mataifa (UNDP), yaliyofanyika katika ukumbi wa Chuo cha Utalii Maruhubi, nje
kidogo ya Jiji la Zanzibar.
Rais Dk. Mwinyi alisema kuwa kazi
iliyobaki mbele hivi sasa ni utekelezaji kwani hakuwa na shaka na utekelezaji kwani
mipango ipo bali lengo ni kuimarisha Mpango wa Maendeleo wa miaka mitano,
kilichobaki ni utekelezaji.
Katika maelezo yake alirejea kauli
yake aliyoitoa siku aliyoyafungua mafunzo hayo kwa kusema kwamba hajaridhika na
utendaji Serikalini, na kueleza kwamba hakusema hilo kwa kwa kumnyooshea kidole
mtu bali alisema kutokana na hali halisi ilivyo kwani bado watendaji Serikalini
hawajawa wepesi katika kufanya mipango ya serikali itekelezeke.
Alisisitiza mabadiliko kubadilika
na kueleza kwamba kila mmoja ni vyema ajione kwamba ana wajibu wa Ofisi yake kutekeleza
mipango iliyopangwa na haitokuwa vyema kiongozi kumaliza kipindi chake cha uongozi
bila ya kuonesha mradi hata mmoja aliotekeleza.
Alieleza kwamba hivyo, hawezi
kusema amefanikiwa, bali atakuwa amefanikiwa kwa kwenda kazini tu lakini
hakufanikiwa kuonesha ama kuacha alama katika Ofisi yake na kusisitiza kwamba
kila mmoja anapaswa kuonesha alichokifanya pale atakapomaliza muda wake wa
kazi.
Rais Dk. Miwnyi alisema kwamba
hatokuwa tayari kusikia wawekezaji wanaokuja kuekeza wanazungushwa.
Alisema kwamba masuala ya uwekezaji
yanataka fedha hivyo, si jambo la busara wawekezaji wakazungushwa kwani wenye
fedha ni lazima wakapokewa vizuri na kuwapokea na kuwakarisha ili waweze
kufanya kazi.
Rais Dk. Mwinyi alisisitiza kwamba
bado kuna watu wanadhani kwamba urasimu ndio njia ya kufanyakazi na kusisitiza
kwamba wakati umefika watu wabadilike.
“ .....bado kuna hali ya kutojali
na hivyo ndipo niliposema kwamba siridhiki na utendaji wa Serikali.....nyinyi
mliokuwepo hapa ndio wakuu wa taasisi zetu ...inawezekanaje upo katika kipindi
chako cha uongozi kwa miaka mitano hata mtu mmoja hajakemewa....ina maana
katika ofisi zetu hamna anayefanya kosa, hayo ndio yanayotufanya tushindwe
kufanikiwa, ningependa kusikia kila mtu anachukua hatua ili kufanya ofisi zetu
zifanye kazi vizuri zaidi”, alisisitiza Dk. Mwinyi.
Aidha, Rais Dk. Mwinyi alisema kwamba
ana amini semina hiyo itawasaidia watendaji kubadilika na wameshajua mipango na
majukumu ya Serikali na lilobaki ni kwenda kupanda jinsi ya kuwezesha kifedha
ili mipango hiyo iweze kutekelezeka.
Sambamba na hayo, Rais Dk. Mwinyi
alitoa pongezi kwa wadhamini wa mafunzo hayo pamoja na kuwapongeza viongozi
wote waliopata mafunzo hayo ambayo alisema yana umuhimu mkubwa na yatasaidia
kwa kiasi kikubwa katika kufikia malengo ya Serikali.
Nae Katibu wa Baraza la Mapinduzi
na Katibu Mkuu Kiongozi Mhandisi Zena Ahmed Said alitoa pongezi kwa Rais Dk. Mwinyi
kwa kuhudhuria katika uwasilishwaji huo wa mada mbali mbali zilozotolewa na
Makatibu Wakuu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na kueleza kwamba mafunzo
hayo yamewapa mwanga mkubwa wa kutekeleza mipango na upangaji wa vipaumbele
vyake sambamba na kuyafanyia kazi maoni yake aliyoyatoa.
Mapema Makatibu Wakuu walipata
fursa ya kuwasilisha mada zao na kueleza mipango kabambe waliyoipanga katika
mafunzo hayo ikiwemo mipango ya kuimarisha sekta ya uchumi wa Buluu, sekta ya
utalii, sekta ya miundombinu, pamoja na masuala ya kijamii.
Imetayarishwa na Kitengo cha Habari
Ikulu Zanzibar.
No comments:
Post a Comment