Habari za Punde

SERIKALI YASEMA HAITOVUMILIA VITENDO VYA UKEKETAJI

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Amon Mpanju akizungumza na Mangariba walioacha Ukeketaji ambao wamesalilisha vifaa ambavyo walikuwa wakivitumia  kukeketa alipofanya ziara kujionea shughuli zinazofanywa na wadau kupinga Ukeketaji katika Kituo cha Hope for Girls and Women kilichopo Wilayani Serengeti mkoani Mara.

Na WMJJWM- Serengeti Mara

Serikali imesema haitovumilia kuona vitendo vya ukatili hasa Ukeketaji vinaendelea kufanywa katika jamii kwani vinasababisha madhara makubwa kwa watoto wa kike na wanawake.

 

Hayo yamesemwa na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Amon Mpanju akiwa wilayani Serengeti, mkoa wa Mara alipotembelea kituo cha Hope for Girls and Women kuona shughuli zinazofanywa na kituo hicho katika kupambana na ukeketaji.

 

Mpanju ameongeza kuwa Wizara itashirikiana na Wizara za kisekta na wadau ili kuhakikisha mapambano dhidi ya vitendo vya Ukeketaji yanaenda kwa kasi zaidi kwa lengo la kutokomeza vitendo hivyo katika Mikoa mbalimbali.

 

Aidha ameitaka jamii na wadau kuwalinda Watoto wa kike na wanawake dhidi ya vitendo vya Ukeketaji na kusisitiza kuwa hakuna Jamii ambayo inaruhusu kukatiza ndoto na maisha ya watoto wa kike kwa kuwafanyia vitendo vya Ukeketaji.

 

"Tunaweza kuishi katika jamii ambayo haina vitendo vya Ukeketaji katika maeneo yenu tuwalinde Watoto wetu wa kike kwani ni Hazina na tegemeo kwa maendeleo ya Taifa" alisema Mpanju

 

Pia amewataka Viongozi wa Kimila kuachana na Mila zilizopita kwa wakati ili kuwaokoa Watoto wa kike na vitendo vya Ukeketaji ambavyo vinasababisha Watoto wengi kupoteza ndoto zao katika maisha.

 

Akitoa taarifa ya Wilaya Afisa Maendeleo ya Jamii Wa Wilaya ya Serengeti Sunday Wambura amesema Wilaya inashirikiana na wadau Wilayani humo katika kutoa elimu kwa wananchi hasa mangariba na Wazee wa Kimila ili waweze kuachana na vitendo hivyo ambavyo vinasababisha hofu, vifo na matatizo ya kisaikolojia kwa watoto wa kike na wanawake.

 

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Kituo cha Hope for Girls and Women Robi Samwel amesema Kituo hicho kimelenga kimewasaidia Watoto wanaokimbia  kukeketwa kwa kuwapa hifadhi na kuendelea kutoa elimu kwa jamii kuachana na vitendo vya ukatili hasa vitendo vya Ukeketaji kwa kuwawezesha mangariba walioacha kukeketwa kupata fursa za kujikwamua kiuchumi na kuachana na vitendo hivyo.

 

"Pia tunawaendeleza wahanga wa Ukeketaji na waliokimbia vitendo hivyo kwa kuwawezesha kupata ujuzi katika fani mbalimbali ili waweze kujitegemea katika kuendesha maisha yao na wengi wamefika katika hatua za juu akiwemo mmoja aliyepo Chuo Kikuu cha Dar Es Salaam" alisema Robi.

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Amon Mpanju akizungumza na  wadau wa kupinga Ukeketaji katika Kituo cha Hope for Girls and Women kilichopo Wilayani Serengeti mkoani Mara alipofanya ziara kituoni hapo kujionea shughuli zinazofanywa na Kituo hicho. 
Mkurugenzi wa Kituo cha Hope for Girls and Women Robi Samwel akitoa taarifa ya Kituo hicho mbele ya Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Amon Mpanju alipofanya ziara Kituoni hapo Wilayani Serengeti mkoani Mara kujionea shughuli zinazofanywa na wadau katika kupinga Ukeketaji.  

Baadhi ya Watoto waliopo katika Kituo cha Hope for Girls and Women waliokimbia kukekekwa katika maeneo yao.

 Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Malaum Amon Mpanju akicheza ngoma ya ritundu alipofanya ziara  katika Kituo cha Hope for Girls and Women kilichopo Wilayani Serengeti mkoani Mara akiwa kituoni hapo kujionea shughuli zinazofanywa na Kituo hicho. 

Picha zote na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini WMJJWM

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.