Habari za Punde

SMZ na SMT zatiliana saini hati za makubaliano za masuala ya mafuta na gesi

 Na Mwashungi Tahir,  Maelezo     

Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania zimetiliana saini hati za makubaliano za masuala ya mafuta na gesi asilia.

Hafla ya utiaji saini huo ulifanyika huko katika Hoteli ya Verde iliyoko Mtoni imehusisha Taasisi sita tatu za upande wa Zanzibar na tatu kwa Tanzania Bara ikiwemo Mamlaka ya udhibiti mkondo wa juu wa Petrol (PURA),Mamlaka ya utafutaji na Uchimbaji wa mafuta Zanzibar (ZPRA), Mamlaka ya Udhibiti wa Maji na Nishati(EWURA) NA Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati Zanzibar(ZURA).

Taasisi nyengine ni Shirika la Maendeleo la mafuta na Petrol Tanzania(TPA) na Kampuni ya Maendeleo ya mafuta na gesi asilia (ZPDC.

Akizungumza mara baada ya utiaji saini Katibu Mkuu wa Nishati na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Eng. Felchesmi Mramba amesema utiaji wa saini huo wa mashirikiano katika suala la mafuta na gesi ,udhibiti wa rasilimali una dhamira ya kuboresha pamoja na uimarishaji wa maendeleo ya Nchi.

Amesema  Serikali imekuwa ikianya utafiti wa kutafuta mafuta na gesi ambapo kwa upande wa Tanzania bara unaendelea kutafuta rasilimali hiyo na sasa tayari mafanikio yamepatikana ambapo mpaka sasa zaidi ya futi za ujazo Tirioni 57 za mafuta na gesi asilia tayari zimeweza kugundulika.

Aidha amesema bado kuna dalili baadhi ya maeneo mbali mbali kwa upande wa Muungano pamoja na Zanzibar tafiti zinaendelea za kupata mafuta na gesi.

Vile vile alieleza kwamba pamoja na taasisi za Zanzibar kupiga hatua mashirikiano ya pamoja zitaongeza mafanikio zaidi.

Amezipongeza Taasisi hizo kwa mashirikiano ya pamoja yataweza kufikia malengo katika maeneo ya tafiti na kuendeleza rasilimali za mafuta nagesi ziende kwa haraka na kufikia mafanikio kwa muda mfupi.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Mjini Rashid Simai Msaraka amesema utiaji saini huo ni kiashirio kikubwa cha Muungano wa Tanzania na Zanzibar ulioasisiwa na Marehemu Abeid Amani Karume na Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na kuifanya Tanzania kuwa na nguvu kuliko Nchi nyengine zulizokuwweko katika Afrika.

Pia amepongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mama Samia Suluhu  Hassan na Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya ZanzibarDkt Hussein Ali Mwinyi kwa kazi wanayofanya kwa nia ya kuendeleza yaliyoachwa na waasisi na kuleta mstakbali wa maendeleo kwa Tanzania.

Akitoa taarifa ya kitaalamu kuhusu hati hizo Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Nishati na Madini wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Mngereza Miraji amesema kuwepo kwa mashirikiano mashirikiano makubwa kwa taasisi hizo hazikuwa na makubaliano maalum yanayosimamia ushirikiano huo.

Amesema  wizara imefikia uamuzi huo wa utiaji saini ili kuimarisha ushirikiano , kusaidiana na kubadilishana maarifa , ujuzi na uzoefu katika kuendeleza mashirika ya Taifa  , kujenga uwezo wa kitaalamu na wataalamu kubadilishana vifaa na teknolojia katika masuala ya ufatiliaji wa mafuta na gesi katika pande za Muungano.

Kwa upamde wa ZURA na EWURA alisema pamoja na kuwa na taasisi hizo zinadhibiti huduma zinazofanana ikiwemo umeme na maji makubaliano hayo yanalenga kuleta ushirikiano na kutoa ushauri wa kitaalamu.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.