Habari za Punde

SMZ Inathamini Juhudi Kubwa Zinazochukuliwa na OPEC Katika Kuiunga Mkono Zanzibar ikiwa ni pamoja na kusaidia katika kuimarisha miundombinu ya barabara, elimu na mengineyo.

 
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi ameupongeza utayari wa Mfuko wa Nchi zinazozalisha Mafuta kwa wingi Duniani (OPEC Fund) wa kuendela kuiunga mkono Zanzibar katika miradi mbali mbali ya maendeleo.

Rais Dk. Mwinyi aliyasema hayo leo Ikulu Zanzibar wakati alipokutana na Mkurugenzi Mtendaji wa Mfuko wa Nchi zinazozalisha Mafuta kwa wingi Duniani (OPEC Fund) Alkhalifa Abdulhamid Saleh akiwa amefuatana na ujumbe wake.

Katika mazungumzo hayo, Rais Dk. Mwinyi alisema kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inathamini juhudi kubwa zinazochukuliwa na OPEC katika kuiunga mkono Zanzibar ikiwa ni pamoja na kusaidia katika kuimarisha miundombinu ya barabara, elimu na mengineyo.

Hata hivyo, Rais Dk. Mwinyi alitumia fursa hiyo kumueleza Mkurugenzi huyo azma ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ya kuimarisha uchumi wake kupitia Uchumi wa Buluu na kumueleza jinsi mikakati iliyowekwa na Serikali anayoiongoza katika kufikia azma hiyo.

Pamoja na hayo, Rais Dk. Mwinyi alimueleza kiongozi huyo kwamba katika Uchumi huo wa Buluu suala la miundombinu nalo limepewa kipaumbele hivyo, ni matarajio yake kwamba Mfuko huo utaendeleza utamaduni wake wa kuiunga mkono Zanzibar ili malengo yaliyokusudiwa katika uchumi huo pamoja na kuibua nyanja nyengine za mashirikiano ikiwemo sekta ya afya.

Sambamba na hayo, Rais Dk. Mwinyi alieleza haja kwa Mfuko huo kuunga mkono juhudi za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuviimarisha vyuo vya Amali ili kuwasaidia vijana walioshindwa kuendelea na masomo ya ngazi za juu.

Nae Mkurugenzi Mtendaji wa Mfuko wa Nchi zinazozalisha Mafuta kwa wingi Duniani (OPEC Fund) Alkhalifa Abdulhamid Saleh alimuhakikishia Rais Dk. Mwinyi kwamba Mfuko huo unahistoria ya kuiunga mkono Zanzibar kwa muda mrefu katika kuimarisha miradi mbali mbali ya maendeleo hivyo, atahakikisha hilo linaendelezwa.

Aidha, Mkurugenzi huyo alimueleza Rais Dk. Mwinyi kwamba kwa vile Mfuko huo una uzoefu na umekuwa ukisaidia vyuo vya amali na kutolea mfano katika nchi ya China hivyo, alimuhakikishia kwamba Mfuko huo utaangalia utaratibu wa kuisaidia na Zanzibar.

Imetayarishwa na Kitengo cha Habari,

Ikulu Zanzibar. OF RESPONSIBILITY ABUSE@THEWORLDNE

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.