Habari za Punde

Zoezi la Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka huu 2022 litakwenda vizuri kutokana na matayarisho mazuri

 

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akizungumza na Kamisaa wa Sensa Zanzibar Mhe.Balozi Mohammed Hamza alipofika Ikulu Jijini Zanzibar kwa mazungumzo na kutowa taarifa ya matayarisho ya Sensa ya Makazi na Watu Tanzania, inayotarajiwa kufanyika mwaka huu mwezi wa Agosti 2022, mazungumzo hayo yamefanyika katika ukumbi wa Ikulu Zanzibar.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi ameeleza matumaini yake makubwa kwamba zoezi la Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka huu 2022 litakwenda vizuri kutokana na matayarisho mazuri yaliyofanyika ikiwa ni pamoja na kufanikiwa kwa Sensa ya Majaribio.

Rais Dk. Mwinyi aliyasema hayo leo wakati alipokutana na Kamisaa wa Sensa Zanzibar, Balozi Mohamed Haji Hamza akiwa na ujumbe wake Ikulu Jijini Zanzibar, wakati alipofika kwa ajili ya kutoa taarifa juu ya Sensa ya Majaribio iliyofanyika pamoja na muendelezo wa matayarisho ya zoezi hilo linalotarajiwa kufanyika mwezi Agosti mwaka huu 2022.

Katika maelezo yake Rais Dk. Mwinyi alisema kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar iko tayari kuendelea kuunga mkono jitihada hizo na kusisitiza kwamba zoezi hilo kwa vile linamaslahi mapana ya Taifa na wananchi wake Serikali itaendelea kuliunga mkono wakati wote.

Rais Dk. Mwinyi alipongeza utaratibu uliwekwa wa ajira kwa watendaji wa zoezi hilo kwani mfumo huo utaondosha malalamiko yaliyowahi kutokea hapo siku za nyuma sambamba na kuweza kupata ufanisi mkubwa kutokana na watendaji ambao watatoka katika maeneo husika.

Alisema kwamba kutokana na utaratibu huo ana matumaini makubwa kuwa hakutokuwa na eneo ambalo watapatikana watu ambao hawatokuwa na sifa za kufanya kazi hiyo ambayo ina umuhimu mkubwa katika maendeleo ya nchi.

Mapema Kamisaa wa Sensa Zanzibar, Balozi Mohamed Haji Hamza alitoa pongezi kwa Rais Dk. Mwinyi kwa miongozo na maelekezo anayotoa juu ya matayarisho ya Sensa ya Watu na Makazi ya Agosti mwaka huu 2022, na kueleza kwamba sensa ya majaribio imefanyika kwa ustadi mkubwa na kuleta matokeo mazuri.

Alisema kuwa matokeo ya Sensa ya Majaribio ni mazuri kwani zoezi hilo limefanikiwa kwa kiasi kikubwa katika maeneo yote yaliyochaguliwa kufanyika na kuwashukuru wananchi kwa mashirikiano makubwa waliyoonesha katika maeneo yote ya majaribio Unguja na Pemba.

Alisema kuwa zoezi la kutenga maeneo ya kuhesabia watu kwa Zanzibar limekamilika kwa asilimia mia moja ambapo kwa upande wa Tanzania Bara zoezi hilo kwa sasa linaendelea katika Mkoa wa Dar es Salaam na kumalizikia Mkoa wa Dodoma ambapo linatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwezi huu wa Machi.

Alisema kuwa matokeo ya Sensa ya Majaribio hutumika kwa matumizi ya ndani ambayo huwa ni kigezo kinachotumika kupima nyenzo zote za utekelezaji wa zoezi la Sensa pamoja na kuzifanya kazi changamoto zilizoonekana ili kuhakikisha zoezi hilo ifikapo Agosti 2022 linafanikiwa.

Balozi Hamza alitumia fursa hiyo kutoa shukurani kwa Rais Dk. Mwinyi pamoja na viongozi wengine wote wakuu wa Serikali kwa kufanya uhamasishaji mkubwa wa zoezi la Sensa ikiwa ni pamoja na kuzitumia hotuba zao wanazozitoa kwa wananchi.

Alisema kuwa tayari wameshakutana na Mawaziri wa Wizara zote hapa Zanzibar kuwapa mukhtasari wa zoezi hilo na kuwaomba watumie nafasi zao katika kila mikutano wanayoifanya kwa azma ya kuwafikishia ujumbe wananchi.

Alieleza kwamba taasisi zote za Serikali zikiwemo Mikoa na Wilaya zimeshakabidhiwa majukumu ya utendaji kuhusu kuhamasiha zoezi hilo la Sensa huku akipongeza mashirikiano wanayopata kutoka ngazi ya Taifa hadi katika uongozi wa Masheha.

Aidha, Balozi Hamza alieleza mipango iliyowekwa katika kuhakikisha suala la ajira linafanyika ipasavyo kwa kuwaajiri makarani wa Sensa pamoja na wasimamizi maudhui ambapo zoezi hilo linatarajiwa kuanza mwezi wa Aprili na litahushisha Wakuu wa Mikoa na Wilaya ambapo waajiriwa hao watatoka katika Shehia zao ili kurahisisha utekelezaji wa zoezi hilo.

Nae Kaimu Mtakwimu Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Mashavu Khamis Omar alieleza namna ya zoezi hilo litakavyofanyika siku itakapofika kwani kila mwananchi atahesabiwa katika eneo husika alilolala na hapatotokea mtu kuhesabiwa mara mbili hiyo ni kutokana na teknolojia itakayotumika.

Imetayarishwa na Kitengo cha Habari

Ikulu Zanzibar.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.