Habari za Punde

Kamati ya Wataalam wa Mipaka Tanzania na Kenya Wakagua Mpaka.

Timu ya Wataalam wa upimaji kutoka nchi za Tanzania na Kenya ikiangalia muelekeo wa mpaka wa nchi hizo katika eneo la Serengeti/ Masai Mara tarehe 12 April 2022. Wa pili kulia aliyevaa kofia ni Mtendaji Mkuu wa Ofisi ya Mipaka ya Kimataifa ya Kenya (KIBO) Juster Nkoroi na aliyeegemea alama ya mpaka ni Mkurugenzi wa Upimaji na Ramani Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Hamdouny Mansoor.

Na Munir Shemweta, WANMM SERENGETI

Timu ya Wataalamu wa Mipaka kati ya Tanzania na Kenya imetembelea na kujionea kazi ya uimarishaji mipaka wa Kimataifa wa nchi hizo iliyofanywa kwa lengo la kukagua na kushauri namna bora ya kuendelea na kazi zinazofuta.

 

Ukaguzi wa mipaka hiyo ulifanyika tarehe 12 April 2022 na ni sehemu ya kikao cha pamoja cha Wataalam wa Mipaka wa nchi hizo kilichoanza juzi kwa ajili ya kupokea  mawasilisho ya kazi iliyofanyika sambamba na kutoa muongozo wa namna bora ya kutekeleza kazi iliyobaki. 

 

Wataalam hao wakioongozwa na Mkurugenzi wa Upimaji na Ramani Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Hamdouny Mansoor pamoja na Juster Nkoroi Mtendaji Mkuu Ofisi ya Mipaka ya Kimataifa nchini Kenya (KIBO) walitembelea mpaka wa Tanzania na Kenya eneo la Kirongwe wilayani Rorya kwa upande wa Tanzania na Muhuru Bay katika Kaunti ya Migori nchini Kenya pamoja na ule mpaka wa nchi hizo eneo la Serengeti/Masai Mara ili kukagua kazi ya uwandani.

 

Timu ya wataalamu wa mipaka kutoka nchi za Tanzania na Kenya tayari imekamilisha uimarishaji mpaka wa kimataifa wa nchi hizo kipande cha Kilomita 83 kutoka hifadhi ya Serengeti/ Masai Mara hadi Ziwa Natron na awamu ya pili ya kipande cha kilomita 110 uimarishaji wake utaendelea baada ya kukamilika kuandaliwa mpango kazi.

 

Wakati wa ufunguzi wa kikao cha pamoja cha Wataalam wa Mipaka wan chi hizo mbili, Mkuu wa wilaya ya Tarime Kanali Michael Mangwela kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mara aliwaambia washiriki kuwa, uimarishaji mipaka ulenge kuimarisha mahusiano pia pamoja na kujadili changamoto za maeneo ya mipakani.

 

Kwa upande wake Mwakilishi wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Kenya Balozi Joseph Vungo alishauri wataalamu wanaoshiriki kikao hicho kuhakikisha wanajadili na kuzitolea maamuzi changamoto kwa amani hasa wakizingatia nchi ya Tanzania na Kenya zimekuwa na mahusiano mazuri.

 

Mpaka wa Tanzania na Kenya eneo la nchi kavu una ukubwa wa Kilomita 758 na uimarishaji wake utasaidia kuondoa changamoto mbalimbali zilizokuwa zikijotokeza kutoka kwa wananchi wanaofanya shughuli maeneo ya mipakani katika nchi hizo.

Mkurugenzi wa Upimaji na Ramani Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Hamdouny Mansoor akionesha muelekeo wa mpaka kati ya Tanzania na Kenya eneo la Serengeti wakati timu ya wataalam wa mipaka kutoka Kenya na Tanzania ilipotembelea mpaka huo tarehe 12 April 2022. Wa pili kulia ni Mwakilishi wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Kenya Balozi Joseph Vungo na katikati ni Mtendaji Mkuu wa Ofisi ya Mipaka ya Kimataifa nchini Kenya (KIBO) Juster Nkoroi.
Mkurugenzi wa Upimaji na Ramani Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Hamdouny Mansoor akitolea ufafanuzi alama ya mpaka wa kimataifa kati ya Tanzania na Kenya eneo la Serengeti wakati Kamati ya wataalam wa mipaka kutoka Kenya na Tanzania ilipotembelea mpaka huo tarehe 12 April 2022.  Kulia ni Mtendaji Mkuu wa Ofisi ya Mipaka ya Kimataifa ya Kenya (KIBO) Juster Nkoroi na kushoto ni Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Maendeleo ya Makazi Wizara ya Ardhi Immaculate Senje.
Mkurugenzi wa Upimaji na Ramani Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Hamdouny Mansoor na Mtendaji Mkuu wa Ofisi ya Mipaka ya Kimataifa ya Kenya (KIBO) Kenya Juster Nkoroi wakizungumza baada ya kutoka kukagua alama ya mwisho wa mpaka ardhini (BP MWISHONI)  katika eneo la Kirongwe wilaya ya Rorya upande wa Tanzania na Muhuru Bay Counti ya Migori upande wa Kenya wakati timu ya wataalam wa upimaji kutoka nchi hizo ilipotembelea mpaka huo
 Muonekano wa alama ya mwisho wa mpaka ardhini (BP MWISHONI) eneo la Kirongwe lililopo wilaya ya Rorya mkoani Mara na Muhuru Bay iliyopo Kaunti ya Migori upande wa Kenya. (PICHA ZOTE NA WIZARA YA ARDHI)

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.