Habari za Punde

Mhe Rahma Kassim Ali Amefungua Maonesho ya Karume Mapinduzi Square Michezani.

Na Rahima Mohamed          Maelezo Zanzibar        6/4/2022

Vijana nchini wametakiwa kumuenzi kwa vitendo aliyekuwa Rais wa kwanza wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Marehemu Sheikh Abeid Amani Karume kwa kuisoma historia ya nchi yao ili kujua wapi walipotoka kwa lengo la kuvirithisha vizazi vijavyo historia hiyo.

Wito huo umetolewa na Waziri wa Ardhi na Maendeleo ya Maakazi Mhe Rahma Kassim Ali wakati akifunga maonesho maalum ya Karume katika Mnara wa Kumbukumbu ya Mapinduzi kisonge Mjini Unguja kwa niaba ya Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar.

Amesema kuna haja ya Vijana kusomeshwa Historia ya Marehemu Karume kwa undani wakiwa bado wanafunzi wadogo maskulini ili historia hiyo igande vyema katika vichwa vyao.

Waziri Rahma amesema katika zama hizi za mitandao ya kijamii Vijanapia wanatakiwa kujitahidi kuchambua historia sahihi ya Karume ili kuepuka kupotoshwa na watu wabaya.

Hivyo ameshauri Wataalam wanaoijua vyema Historia ya Shekh Karume waitumie Mitandao ya kijamii kuiingiza historia yake katika mitandao hiyo.

Akielezea lengo la maonesho hayo Waziri Rahma amesema ni kumuenzi muasisi huyo aliyepigania uhuru wa Zanzibar ili wananchi waweze kujikomboa kutokana na ukoloni.

Kwa upande wake Msimamizi Mkuu wa Makumbusho ya miaka 50 ya Mapinduzi mnara wa kumbukumbu kisonge Ali Ussi Khamis amewaomba wananchi kujitokeza kwa wingi katika Makumbusho hayo ili kujifunza mengi ambayo hawayajui kuhusu nchi yao.

Aidhaamewaomba wananchi kuyaendeleza mazuri yote yaliyofanywa na Mzee Karume kwa lengo la kuiletea maendeleo Zanzibar.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.