Habari za Punde

Uzinduzi wa Nembo ya Tarehe ya Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022 Ukumbi wa Hoteli ya Golden Tulip Uwanja wa Ndege Jijini Zanzibar leo 8-4-2022.

 

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Samia Suluhu Hassan na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi wakipiga makofi baada ya kuizindua Nembo ya Tarehe ya Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022, uzinduzi huo uliofanyika katika ukumbi wa Hoteli ya Golden Tulip Uwanja wa Ndege Unguja Jijini Zanzibar leo 8-4-2022.(Picha na Ikulu)

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan leo ameizindua rasmi nembo ya Sensa ya Watu na Makaazi ya mwaka 2022 huku akiitangaza tarehe 23 Agosti 2022 kuwa ndio siku ya kufanya zoezi hilo hapa nchini.

Uzinduzi huo umefanyika katika ukumbi wa Hoteli ya Golden Tulip, Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amanai Karume Zanzibar na kuhudhuriwa na viongozi mbali mbali wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na viongozi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar akiwemo Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi.

Katika hotuba yake aliyoitoa Rais Samia alisema kuwa asilimia 79 ya matayarisho ya Sensa hiyo ya Watu na Makaazi ya mwaka 2022 iliyofikiwa imetokana na mashirikiano makubwa yaliopo ya viongozi wakuu pamoja na watendaji wa Serikali zote mbili ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Rais Samia alisisistiza haja ya uelimishaji na uhamasishaji kwa wananchi juu ya umuhimu wa zoezi hilo huku akisisitiza kwamba Serikali haiwezi kupata maendeleo bila ya kuwa na takwimu sahihi.

Aidha, Rais Samia alitoa wito katika kuitumia nembo hiyo na kuitaka sekta ya umma na sekta binafsi kuhakikisha inaitumia nembo hiyo katika shughuli zao zote mpaka mwisho wa zoezi la Sensa ya Makaazi ya mwaka 2022 huku akiwapongeza wadau wa maendeleo wanaoiunga mkono Tanzania katika kuhakikisha zoezi hilo linafanikiwa.

Nae Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapindzuzi Dk. Hussein Mwinyi kwa upande wake alisema kuwa uzinduzi wa nembo ya Sensa ambayo imebeba kauli mbiu pamoja na tarehe ya Sensa ni muhimu katika kufanikisha zoezi hilo.

Aliongeza kuwa ujumbe uliobebwa kwenye nembo utawataka wananchi wajitayarishe kushiriki na kufanikisha zoezi hilo.

“Naamini kwamba kuanzia leo wananchi watakuwa hawaulizani tena lini zoezi hili la Sensa litafanyika, ila tutaendeleza kazi ya kuhamasishana ni matumaini yangu kwamba nembo hii sasa itatumiwa vizuri na taasisi za Serikali, Vyombo vya Habari, Mashirika na Makampuni binafsi, Wafanyabiashara na Jamii kwa jumla kwa lengo la kuhamasisha Jamii juu ya umuhimu wa kujiandaa na kushirikiana katika zoezi la Sensa siku itakapofika”,alisema Dk. Mwinyi.

Aidha, Rais Dk. Mwinyi aliipongeza Kamati Kuu ya Kitaifa ya Sensa ya Watu na Makaazi kwa kukamilisha Sensa ya Majaribio kwa ufanisi mkubwa na kueleza kwamba mafanikio yaliyopatikana katika Sensa ya Majaribio iliyofanyika katika Mikoa 18 ikiwemo Mikoa yote mitano ya Zanzibar pamoja na changamoto zilizojitokeza yatakuwa ni dira katika kukamilisha kwa ufanisi kazi waliyopewa.

Nao viongozi mbali mbali wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa nyakati tofauti walieleza umuhimu wa Sensa ya Watu na Makaazi huku wakipongeza hatua iliyofikiwa ya matayarisho sambamba na mashirikiano makubwa yaliopo katika kufanikisha zoezi hilo hapa nchini.

Imetayarishwa na Kitengo cha Habari

Ikulu Zanzibar.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.