Habari za Punde

KILELENI KUNA NYOKA-KADUMA

 


 

Na.Adeladius Makwega DODOMA

“…NItasema kweli daima fitina kwangu mwiko, Nitakuwa raia mwema wa Tanzania, Afrika na Dunia nzima, Nitakuwa mtii kwa Rais na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania…”

Nilisikia maneno hayo yakitamkwa na mzee mmoja ambaye alikuwa amevalia suti ya rangi kama ya samawati mbele ya ukumbi Mult-Purpose uliojaa watu wengi wakiwamo wahadhiri na wanachuo wa Chuo Kikuu cha Tumaini Iringa, wanahabari na wageni wengine.

Alipomaliza kukisoma kitabu hicho ambacho kwa macho yangu ya wakati huo kilionekana kimechakaa mno.Nilijiwa na swali yule ni nani?

“Ni miongoni mwa mawaziri wa serikali ya Julius Nyerere, anaitwa Profesa Ibrahimu Kaduma, anatoa mada juu ya mchango wa vijana wasomi walivyojitoa kutumikia taifa lao la Tanganyika huru.”

Aliniambiwa kwa kunong’ona Tito Mganwa ambaye alikuwa mwanachuo wa mwaka wa pili Shahada ya Sanaa ya Habari wakati huo chuoni hapo.

Siku hiyo Profesa Kaduma alimuomba mshereheshaji wa tukio hilo Godwin Gondwe ambaye alikuwa mwanachuo wa mwaka wa tatu wa Shahada ya Sanaa na Habari na Mtangazaji maarufu wa ITV na Redio One (Sasa Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni) kumtambulishwa kama Ndugu Kaduma na siyo Profesa Kaduma.

Alizungumzia umasikini wa Watanzania tangu uhuru na hali ya Tanzania ya wakati huo na namna ujamaa ulivyokuwa na lengo la kuwakomboa Watanzania. Hoja zake zilisindikizwa na sauti yake nzito iliyokuwa na mikwaruzo ambayo ilisaidia kila aliyekuwepo ukumbini hapo kusikiliza kwa umakini.

Ukumbi wa Chuo KIkuu cha Tumaini Iringa wa Mult Purpose  ulijazwa na wanachuo ambao walikuwa katika makundi matatu: Kwanza waliokuwa wakilipiwa ada na wazazi wao, Pili waliokuwa wakilipiwa ada na wafadhili na kundi la tatu waliokuwa wengi wao nikiwapo mimi tuliokuwa tukilipiwa ada na serikali ya Rais Benjamin Mkapa ambayo wakati huo ilianza na mikopo ya elimu ya juu.

Alisema bayana kuwa kila ahadi ya mwana TANU ilikuwa ina lengo mahususi.

“Nitaitumikia nchi yangu na binadamu wezangu wote kwa unyenyekevu na moyo wa upendo na huruma.”

Nimeambiwa kuwa huwa mnapanda mlima wenu jirani na chuo pamoja, nimeambiwa Rais wa wanachuo Ndugu Simon Berege kuwa huwa mnajitahidi mnafika wote kileleni, huku njiani mkisaidiana, kweli si kweli?  Aliuliza

“Kweli.” Alijibiwa ukumbini.

“Sasa unapomsaidia mwezako kunyanyuka aliyeanguka, unamtolea maneno ya ukali? Unasema kwa maneno ya unyenyekevu, upole na huruma ili mwisho mfike pamoja mlimani, hivyo ndivyo tulivyofanya katika kuijenga nchi yetu.Wewe ukiyatoa kwa ukali nayeeye mwanzoko kesho atayatoa kwa ukali”

Alifafanua Profesa Kaduma ukumbini hapo kukiwa kimya.

“Hivi ukifika kule kileleni wewe mwenyewe, ukikutana na kundi la nyuki inakuwaje? Kileleni kuna nyoka.(Ukumbini kulisikika kicheko)Ukiwa na wenzako watakusaidia  kutafuta fimbo , mawe ili kupambana na nyoka au nyuki hao.”

Ukumbi huu wa mikutano ulikuwa kimya zaidi huku milio ya kukisikika ndege wakiruka ruka tu, Profesa Kaduma aliwaasa wahitimu wa shahada mbalimbali ambao kesho yake walikuwa wanaanyiwa mahafali yao aliwaambia wajitahidi hata baada ya kuhitimu wakaisaidie jamii ya Tanzania yenye masikini wengi.

Alisema bayana kuwa hata jamii iliyokuwa inakizunguka chuo hicho ni jamii ya watu masikini akitutaka kila mmoja wetu kukumbuka jamii aliyotokea akisema kuwa ni jamii masikini sawa na hiyo ya Iringa iliyokuwa inakizunguka chuo hicho.

Binafsi nilivuta picha ya Mbagala nyumbani kwetu, maisha ya kununua sukari ilivyofungwa katika karatasi kama binzari, ikiuzwa kati ya shilingi 20-50/- Jamii ya kula makwasukwasu, miguu ya kuku, utumbo wa kuku na vichwa vya kuku. Somo la Profesa Kaduma nililielewa sana na kama Profesa Kaduma angetoa mtihani wa nadharia na vitendo A ingenyakuliwa.

Mara baada ya Profesa Kaduma kumaliza kuongea alimkabidhi maikrofoni hiyo mwendashaji wa wa sherehe Godwin Gondwe nayeye alimualika Simon Berege ambaye alikuwa Rais wa wanachuo wakati huo (Sasa ni Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri moja) alimshukuru Profesa Kaduma kwa kutoa mada hiyo.

Godwin Gondwe alimkaribisha Eliamani Laltaika ambaye alikuwa kiongozi wa umoja wa wahitimu wa chuo hicho (Sasa ni jaji wa mahakama Kuu). Ndugu huyu mwanasheria alitoa shukurani zake kwa niaba ya wahitimu wa miaka nyuma kwa Profesa Kaduma kuendelea kuwalea kitaalumu na kiimani kwa miaka mingi.

Ndugu Laltaika ambaye wakati huo alikuwa pia mhadhiri wa kitivo cha sheria alisoma wasifu wa Profesa Kaduma.“Ibrahimu Mohammedi Kaduma alizaliwa na wazazi wawili, Baba-Mohammed Kaduma na Mama-Mwanaidhza Kaduma huko Njombe mkoani Iringa mwaka 1937. Akasoma Chuo Kikuu cha Makerere, Chuo Vikuu Marekani na Uingereza.”

Alituambia kuwa mwaka 1961 alianza kazi na serikali ya Tanganyika kama mhasibu msaidizi, akapitia ngazi mbalimbali hadi akawa Waziri wa Mambo ya Nje, Waziri wa Biashara, Waziri wa Mawasiliano na Usafirishaji, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na vyeo vingine vingi.

Alipomaliza wasifu huo shughuli hiyo ilifungwa kwa sala na sisi kuondoka zetu majumbani. Huku Tito Mganwa akiniambia kuwa Profesa Ibrahimu Kaduma, Profesa Nicolaus Bangu na Profesa Andongwiysye Katule wakiwa ni miongoni mwa wasomi kutoka huko kwao Njombe.

Mwanakwetu huyo ndiyo Profesa Ibrahimu Mohammed Kaduma ambaye alifariki dunia Septemba 1, 2019. Mwaka huu wa 2022 anatimizia miaka mitatu tangu afariki dunia. Binafsi Profesa Kaduma nitaendelea kumkukumbuka kwa kuzitamka bila woga na kuziishi ahadi za mwana TANU.

Mwanakwetu naiweka kalamu yangu chini kwa kurudia mfano wake kuwa unapopanda mlima panda na wenzako kumbuka kileleni kuna nyoka.

makwadeladius@gmail.com

0717649257

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.