Habari za Punde

Kituo cha Uuzaji wa Mafuta cha “UP” Fuoni Yaonja Joto ya Jiwe. Kwa Kushindwa Kutumia Mfumo wa Kutolea Risiti za Kielektroniki (VFMS).

 

Maofisa wa Bodi ya Mapato Zanzibar (ZRB) wakikagua risiti wakati wa zoezi la kuwasaka Wafanyabiashara ambao hawatumia risiti za Kieletroniki wakati wa kuuza bidhaa zao kwa wanunuzi.

Na. Muandishi Wetu.

Bodi ya Mapato Zanzibar (ZRB) imekichukulia hatua kituo cha kuuzia mafuta cha United Petroleum (UP) kilichopo Fuoni kwa kukipa hati ya makosa iliyotokana na kushindwa kutumia Mfumo wa kutolea Risiti za Kielektroniki (VFMS).

Hatua hiyo imechukuliwa leo katika ukaguzi wa matumizi ya mfumo wa kutolea Risiti za kielektroniki kwa kwa Vituo vinavyouza mafuta ya nishati na aina zote za biashara Unguja na Pemba.

Afisa Uhusiano ZRB Ndg. Badria Atai Masoud, amesema kuwa ZRB haitasita kuwachukulia hatua za kisheria wafanyabiashara wote ambao wanakiuka agizo la Serikali, la kutumia mashine za kutolea risiti za kielektroniki kwa lengo la kuweka kumbukumbu za mauzo yao katika mfumo ambao unakubalika.

Bi. Badria amesisitiza kuwa, ZRB itaendelea kusimamia sheria na kuwachukulia hatua wale wote ambao hadi sasa hawatii agizo la Serikali pamoja na kuwasisitiza wafanyabiashara wote kuendelea kutoa risiti kwa kila mauzo ya bidhaa au huduma watakazokuwa wanauza katika biashara zao.

Kwa upande wake, Meneja Uhakiki kwa walipakodi ZRB Ndg. Suwedi Mohamed Suwedi amesema kuwa kwa mujibu wa kifungu cha 23 cha sheria za usimamizi wa kodi kinasema kuwa kila mfanyabiashara anaeuza bidhaa au huduma ni wajibu wake kutoa risiti za kielektroniki.

Hivyo kwa vile kituo cha UP Fuoni Petrol Station kimeshindwa kutii agizo hili, ZRB imempatia hati ya makosa ya shilingi milioni mbili (2,000,000/=) kama adhabu kwa kosa hilo.

Naye Meneja wa kituo hicho Ndg. Vuai Suleiman Vuai amekiri kuwa wamepokea barua kutoka ZRB inayowataka kununua mashine za VFD na kutoa risiti katika kila mauzo wanayoyafanya na kwamba mpaka sasa hawajanunua na kuanza kutumia mashi ne hizo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.