Habari za Punde

MAJALIWA: Tunaangalia Namna ya Kutoa Mikopo kwa Wanafunzi wa Elimu ya Kati.

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali inaendelea kufanya tathmini ya taarifa ya tume iliyoundwa na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia ili iangalie namna ya kutoa mikopo kwa wanafunzi wa elimu ngazi ya kati.

Amesema hayo jana (Jumanne, Mei 24, 2022) wakati akiweka jiwe la msingi kwenye jengo la Ufundi Tower katika  Chuo cha Ufundi Arusha na kumuagiza Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu ahakikishe anasimamia ujenzi huo ili wanafunzi wa chuo hicho waweze kulitumia jengo hilo.

 

“Wabunge waliishauri Serikali kuwa tuangalie ni namna gani tunaweza kuwawezesha wanafunzi wa ngazi ya kati ya astashahada na cheti, kada ambayo ndiyo yenye wataalaamu wanaoingia field, sasa tumeona tuimarishe na tutalifanyia kazi.”

 

Amesema kuwa katika bajeti ya mwaka huu Serikali itaendelea kuhakikisha kila mwanafunzi anayetoka katika familia zisizokuwa na uwezo wa kujilipia gharama mbalimbali kwenye vyuo ananufaika na mikopo hiyo. “Maboresho mbalimbali katika sekta ya elimu nchini yanaendelea”

 

Aidha, Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa kutokana na idadi kubwa ya udahili unaofanywa katika sekta ya elimu, Serikali itaendelea kutenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa mabweni katika vyuo mbalimbali nchini. “Sekta ya elimu imeendelea kutoa tija kwa Watanzania, uwekaji wa jiwe la msingi katika chuo hiki ni ushahidi kwamba vyuo vingi vya elimu ya juu vimepatiwa mgao huu na tunaendelea kuboresha.”

 

Aidha, Waziri Mkuu ameupongeza uongozi wa Chuo hicho kwa kusimamia viwango katika ujenzi wa majengo hayo na akawataka waendelee kusimamia viwango hivyo katika miradi yote wanayokabidhiwa na Serikali. “Nakiri kuridhika na ujenzi wa majengo haya, majengo haya yana hadhi ya kuzinduliwa na viongozi wetu wakuu wa nchi.”

 

Akizungumza na wanafunzi wa chuo hicho mara baada ya kuweka jiwe la msingi, Waziri Mkuu amewataka wanafunzi hao wazingatie masomo yao ili kila mmoja atakapohitimu aweze kutengeneza mazingira ya kujikuza kiuchumi kupitia elimu aliyoipata. “Hadhi ya chuo hiki katika utekelezaji wa miradi mbalimbali nchini inawatengenezea ninyi njia ya kwenda kutambulika popote pale mnapokwenda, tendeeni haki fani zenu.”

 

Ujenzi wa jengo hilo lililogharimu sh. bilioni 1.7 zilizotokana na programu ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa na Mapambano dhidi ya UVIKO-19 umefikia asilimia 88 na unatarajiwa kukamilika Juni 2022.

 

Mapema, Waziri Mkuu alitembelea eneo la Njiro inakojengwa hospitali ya Wilaya ya Arusha ili kukagua ujenzi wa majengo ya idara ya wagonjwa wa nje (OPD) ambayo yanatarajiwa kugharimu sh. bilioni 3.91.

 

Waziri Mkuu amemtaka mkandarasi anayejenga hospitali hiyo kutoka kampuni ya Ladwa  ahakikishe anakamilisha kazi hiyo ifikapo Septemba, mwaka huu kama alivyoahidi. “Wananchi hawa wanatarajia kazi hii ikienda kwa mfululizo, wajibu wetu ni kuwahakikisha kwamba kazi hii inakwenda, mkandarasi tumeshakupa fedha, tunatarajia kila siku utakuwa hapa.”

 

Waziri Mkuu amesema nia ya Serikali ya awamu ya sita ni kuwapunguzia adha wakazi wa Jiji la Arusha wanaoishi maeneo ya pembezoni na pia kupunguza msongamano wa wagonjwa kwenye hospitali za Mount Meru na KCMC.

 

IMETOLEWA NA:

OFISI YA WAZIRI MKUU,

S. L. P. 980,

41193 – DODOMA

JUMATANO, MEI 25, 2022.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.