Habari za Punde

NYIMBO MBILI ZA MDUMANGE

 

Na.Adeladius Makwega-DODOMA

Wasambaa wana ngoma yao moja inayofahamika kama Mdumange ambayo huwa inachezwa taratibu huku maungo yakitikishwa na wachezaji walio katika umbo la duara, wakiwazunguka wapigaji vyombo kama vile ngoma, manyanga, mabati na filimbi wakiwa katikati.

Mzunguko huo una raha zake mno hasa namna viungo vinavyochezeshwa wanaume na wanawake. Hapo mambo yanafana na kunoga mno kama wachezaji wanawake wamejifunga vibwebwe na angalabu wao hufanya hivyo.

Siku ya leo nimezikumbuka nyimbo mbili za ngoma hii ya shemeji zangu Wasambaa.

“Hata gulo naavina naye kumbe ni nshemeji hetia, Hata gulo naavina naye kumbe ni nshemeji hetia.Ooo nshemeji mwe imani hatei kodi azanhilia, Ooo nshemeji mwe imani hatei kodi azanhilia.”

NAAVINA NAE KUMBE NSHEMEJI-NACHEZA NAE KUMBE SHEMEJI. Hapo akimaanisha hata jana nilicheza naye kumbe ni shemeji yangu ni shemeji wa imani hata kodi amenilipia. Huo ni wimbo wa kwanza.

“Kandee kangu nkadodo kaeke kakukue, Kandee kangu nkadodo kaeke kakuekue tate. Huyu Neghanga nemdodo hazaiti hataie kudika, Huyu Neghanga nemdogo hazaiti hataie kudika.”

KANDEE KANGU NKADODO-BINTI YANGU BADO MDOGO akimaanisha kuwa Baba binti yangu bado mdogo muache akue, huyu Neghanga bado mdogo hajui kupika. Huu ni wimbo wa pili.

Mwanakwetu haya ni mambo mazito sana ukiyataka nenda kuyashuhudia huko Usambaani hasa hasa wa MTAE, KWEMAKAME, KWEMASHAI, SHAGAYU, LUKOZI, MALINDI, LUNGUZA, MBARAMO na hata MLOLA.

Katika wimbo huu palikuwa na ushindani juu ya kumuoza binti, mama anasema kuwa huyo binti yake bado mdogo hajui kupika kwa hiyo kuolea wakati wake bado.

Mama anaoneshwa wazi kuwa binti yake bado yupo mafunzoni akifundishwa mapishi (mapishi ya kikubwa). Wazazi wanaume (Tate) wao somo hilo halijawaingia wanalazimisha bila kufahamu hekima ya mama. Mama kafumba fumbo kumfumbia mumewe.

Mama tunapaswa kumpa nafasi ili aweze kumfundisha bintiye kupika vizuri wakati ukifika mama yetu ataruhusu bintiye aolewe. Kweli inapendeza binti yetu tumuoze alafu anakwenda huko anaachika kisa hajui kupika?

Wakati ukifika tutapokea posa kwa amani na hakika ya mama tutajua kuwa binti yetu kafuzu, hilo litasaidia sana waposaji wengine kujongea katika nyumba yetu kuposa. Mashaka ni ya pande mbili hata baba naye anaona kuwa chelewa chelewa huyo binti akiwa mafunzoni ataweza kutoka salama?

Ushindani na kutokuaminiana wa nini?

Tutambue kuwa tunapogombana tunawapa siri wale waliokuwa wakitamani kuposa kwetu wakatuweka kando na kwenda kuoa kwingineko na pengine binti zetu watazeekea nyumbani. Lakini ni muhimu kila upande upatiwe nafasi hadi maamuzi yafanyike.

Mama yetu tumpe muda na kama wale wengine tusimsongesonge ili aweze kushamiri na kujipambanua kumfundisha binti yetu vizuri wakati ukifika mambo yatakuwa uwanjani na sote tutaucheza mdumange ukiwa na wimbo mwingine ambao mama tayari ameshampa kazi mtunzi akiutunga kwa midundo ile ile lakini mashairi mengine.

Nakutakia siku njema.

makwadeladius@gmail.com.

0717649257

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.