Habari za Punde

ULEGA: TUMIENI TEKNOLOJIA KUZUIA UPOTEVU WA MAZAO YA UVUVI

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega akikata utepe kuashiria uzinduzi wa ugawaji wa Boti 3 kwa Wakuu wa Wilaya wa Mkoa wa Kigoma ikiwa ni sehemu ya  maadhimisho ya miaka 10 ya Mradi wa Tuungane yaliyofanyika Mkoani Kigoma

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega akiongea na wadau wa Sekta ya Uvuvi (hawapo pichani) wakati akizindua maadhimisho ya miaka 10 ya Mradi wa Tuungane yaliyofanyika Mkoani Kigoma Mei 5, 2022. Mradi huo wa Tuungane ambao unatekelezwa katika ukanda wa Ziwa Tanganyika umejikita katika kutunza mazalia ya Samaki, kupunguza Uvuvi haramu na kuwezesha wachakataji wa mazao ya Uvuvi.


Na Mbaraka Kambona, Kigoma

NAIBU Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega amesema kuwa sekta ya uvuvi nchini inakabiliwa na changamoto kubwa ya upotevu wa mazao ya samaki hususan dagaa huku akiwataka wadau kuhakikisha wanatumia teknolojia za kisasa ambazo ni rahisi zitakazowezesha kukabiliana na changamoto hiyo.

Waziri Ulega aliyasema hayo Mei 5, 2022 Mkoani Kigoma alipokuwa akizindua maadhimisho ya miaka 10 ya mradi wa Tuungane unaotekelezwa na mashirika ya kimataifa ya Tanzania Nature Conservancy na PathFinder International kwenye vijiji vya kusini mwa mwambao wa ziwa Tanganyika.

Alisema ni muhimu kufahamu kwamba tatizo la upotevu wa mazao ya uvuvi katika ukanda huu wa ziwa Tanganyika bado ni kubwa hivyo wadau wa maendeleo ikiwemo mradi wa tuungane kuwekeza zaidi kwenye teknolojia ya ukaushaji wa mazao ya dagaa na kuwaepusha wavuvi na hasara.

“Kama kweli tunataka kuwawezesha wavuvi wetu basi tuwekeze katika  ukaushaji wa dagaa, jambo hili ni muhimu sana kwa mustakabali wa watu wetu”, huku akiongeza kuwa “tusiruhusu kuona dagaa ambao wanaweza kuwainua Watanzania wa chini kuendelea kupoteza matumaini kutokana na upotevu wa mazao yao hasa katika kipindi cha mvua”,alisisitiza

Aidha, Waziri Ulega aliupongeza mradi wa tuungane kwa kuwajengea vichanja vya kuanikia dagaa wavuvi wanaofanya shughuli zao katika ukanda wa ziwa Tanganyika na kuongeza kuwa kitendo hicho walichokifanya kinaunga mkono nia ya  Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan ya kukuza uchumi wa buluu nchini.

Aliendelea kuwapongeza kwa kuimarisha  vikundi vya ulinzi shirikishi wa rasilimali za uvuvi katika mwambao wa ziwa Tanganyika kwani kumewezesha kuwepo na ongezeko kubwa la rasilimali za uvuvi kwenye ziwa hilo kufuatia ulinzi na uhifadhi  wa maeneo ya mazalia ya samaki na dagaa.

Pamoja na mafanikio hayo  alisema haitoshi kuishia kuhifadhi maeneo ya mazalio ya uvuvi na kuongeza uzalishaji bali kuna haja sasa ya kuwa na teknolojia za kisasa zitakazowawezesha wavuvi kuchakata mazao yao na kuyaongezea thamani.

Awali, Mkurugenzi Mkuu wa Tanzania Nature Consevancy (TNC), Lucy Magembe alisema kuwa katika kipindi cha miaka 10 kupitia mradi wa Tuungane wameweza kuhifadhi maeneo ya mazali ya samaki na maeneo ya uvuvi yenye ukubwa wa Hekta 12,015 katika wilaya za uvinza mkoa Kigoma, Mlele na Tanganyika wilaya ya Katavi.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Uvinza, Hanaf Msabaha alisema kuwa licha ya Serikali kufanya kazi kubwa katika kutekeleza miradi mbalimbali ya uvuvi kwenye mwambao wa ziwa Tanganyika, utekelezaji wa mradi wa Tuungane umewezesha kupunguza uvuvi haramu, kutoa elimu kwa wavuvi na wachakataji wa mazao ya uvuvi ambao wamewezesha kwa sasa dagaa wa Kigoma kuwa na thamani kubwa na kuwa na soko kubwa nje ya nchi.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.