Habari za Punde

SERIKALI YAZIBANA WIZARA NA IDARA ZAKE KUKUSANYA MAPATO YASIYO KODI KWA UFANISI

 

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango Bw. Lawrance Mafuru, akizungumza wakati wa kikao na Wizara na Idara mbalimbali zinazojitegemea zinazokusanya maduhuli ya Serikali yasiyo kodi kilichoangazia njia bora za kusaidia katika kuongeza makusanyo ya maduhuli ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023, jijini Dodoma. Kushoto ni Kamishna wa Idara ya Sera, Bw. Elijah Mwandumbya.

Na Benny Mwaipaja, Dodoma

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango anayesimamia masuala ya Sera, Bw. Lawrence Mafuru, amezitaka Wizara na Idara zinazojitegemea zinazokusanya mapato ya Serikali yasiyo Kodi, kuhakikisha kuwa wanakusanya maduhuli hayo kwa ufanisi ili kuiwezesha Serikali kupata mapato yatakayosaidia kuwaletea wananchi maendeleo mwaka ujao wa fedha wa 2022/2023.

Bw. Mafuru ametoa maelekezo hayo alipokutana na kujadiliana na wadau kutoka Wizara na Taasisi 25 za Serikali zinazotoa mchango katika Bajeti Kuu ya Serikali kwa kukusanya maduhuli ya Serikali kila mwaka wa fedha.

Alisema kuwa katika kipindi cha mwaka wa fedha 2020/2021, makadirio ya mapato yasiyo kodi yalikuwa shilingi trilioni 2.92 sawa na asilimia 8.4 ya Bajeti yote ya Serikali ya shilingi trilioni 34.88 ambapo mapato halisi yalikuwa shilingi trilioni 2.21 sawa na asilimia 75.6 ya lengo lililokusudiwa.

Bw. Mafuru alisema kuwa mwaka ujao wa fedha 2022/2023, Serikali inatarajia kukusanya zaidi ya shilingi trilioni 3 za mapato yasiyo kodi na kuzitaka Wizara na Idara za Serikali kuimarisha mifumo ya ukusanyaji pamoja na kusimamia  ipasavyo mapato hayo.

Kwa upande wake Kamishna wa Idara ya Sera, Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Elijah Mwandumbya, alizitaka Wizara na Idara hizo zinazotakiwa kuiwezesha Serikali kupata mapato ya kutosha ya kutekeleza miradi mbalimbali kwa ajili ya maendeleo ya nchi, kusimamia vizuri matumizi ya fedha hizo.

Katika hatua nyingine, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Lawrence Mafuru, amezitaka, Wizara, Idara na Taasisi za Serikali zilizopokea fedha za kukabiliana na athari za Uviko 19 zilizotolewa na Shirika la Fedha la Kimataifa- IMF, kuwasilisha katika Wizara ya Fedha na Mipango mikataba yote waliyoingia na wazabuni waliotekeleza miradi hiyo.

Alisema kuwa kuna kusua sua kwa uwasilishaji wa mikataba hiyo hatua ambayo inakiuka makubaliano ya kimkataba yaliyoingiwa kati ya Serikali na IMF, hatua iliyolenga kuweka uwazi wa matumizi ya fedha hizo na kuzitaka Wizara, Idara na Taasisi hizo kutekeleza maelekezo hayo haraka iwezekanavyo.

Hivi karibuni, Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) liliipatia Tanzania mkopo usio na riba wenye thamani ya shilingi trilioni 1.3 kwa ajili ya kutekeleza Mpango wa Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano dhidi ya Ugonjwa wa UVIKO 19 na miongoni mwa masharti ya mkopo huo ni kuwepo kwa uwazi wa matumizi ya fedha kwa umma na kuweka bayana mikataba iliyoingiwa na wazabuni pamoja na wakandarasi mbalimbali waliotekeleza miradi inayohusiana na mkopo huo.

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Lawrance Mafuru, akimsikiliza Kamishna wa Idara ya Sera Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Elijah Mwandumbya, akifafanua jambo wakati wa kikao kati ya Wizara na Idara mbalimbali zinazojitegemea zinazokusanya maduhuli ya Serikali yasiyo kodi kilichoangazia njia bora za kusaidia kuongeza makusanyo ya maduhuli ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2022/2023, jijini Dodoma.
Baadhi ya washiriki kutoka wizara mbalimbali wakifuatilia mawasilisho wakati wa kikao kati ya Wizara ya Fedha na Mipango na Wizara na Idara mbalimbali zinazojitegemea zinazokusanya maduhuli ya Serikali yasiyo kodi kilichojadili namna ya kuongeza ufanisi na kuongeza makusanyo ya maduhuli ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2022/2023, jijini Dodoma.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango Bw. Lawrance Mafuru, akiteta jambo na Kamishna wa Idara ya Sera, Bw. Elijah Mwandumbya, baada ya kuhitimishwa kwa kikao kati ya Wizara na Idara mbalimbali zinazojitegemea zinazokusanya maduhuli ya Serikali yasiyo kodi, jijini Dodoma.
Maafisa kutoka Wizara ya Fedha na Mipango wakichukua kumbumkumbu za michango ya wajumbe wakati wa kikao kati ya Wizara ya Fedha na Mipango na Wizara na Idara mbalimbali zinazojitegemea zinazokusanya maduhuli ya Serikali yasiyo kodi  kilichojadili njia bora za kusaidia kuongeza makusanyo ya maduhuli ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2022/2023, jijini Dodoma.

Baadhi ya washiriki kutoka Wizara na Idara mbalimbali zinazojitegemea zinazokusanya maduhuli ya Serikali yasiyo kodi wakifuatilia majadiliano wakati wakiwasilisha taarifa za ufanisi wa makusanyo ya maduhuli hayo kwa mwaka wa fedha 2020/2021, katika Ukumbi wa Mikutano wa Kambarage, Jijini Dodom

(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, WFM, Dodoma)

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.