Habari za Punde

Uhamasishaji wa SENSA ya Watu na Makazi Kwa Wahariri na Waandishi wa Habari Zanzibar.

Na Khadija Khamis- Maelezo/ 22/06/2022.

Kamisaa wa Sensa. Balozi Mohammed Haji Hamza amesema sensa ya watu na makaazi itaisaidia  serikali kutathmini utekelezaji wa malengo ya maendeleo nchini

 

Akiyasema hayo huko Ukumbi wa Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali ya Zanzibar, Mazizini, katika kikao Cha uhamasishaji kwa Wahariri na Waandishi wa habari kuhusiana na  Maandalizi ya Sensa ya Watu na Makaazi ambayo yanatarajiwa kufanyika August 23 mwaka huu.

 

Alisema jamii inatakiwa kutoa ushirikiano kwa Serikali ikiwemo kutoa taarifa sahihi za idadi ya watu na makaazi kwa makarani wa sensa ili ipatikane takwimu halisi ambayo itasaidia kupanga mipango ya maendeleo kwa wananchi wake

 

Alieleza suala la sensa linamuhusu kila mmoja hivyo kila  mtu aliyelala usiku wa kuamkia siku ya sensa katika mipaka ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ana Haki ya kuhesabiwa .

 

Aidha alisema  zoezi la kuhesabiwa ni la kila mtu  bila ya kujali rangi, jinsia, dini, kabila, asili ya mtu anapotokea  kwa hivyo hata wageni watahesabiwa siku hiyo

 

Nae Mkurugenzi wa Idara ya Habari Maelezo Hassan Khatib Hassan aliwataka wahariri wa vyombo mbali mbali na waandishi wa habari kuelimisha jamii kuhusiana na zoezi zima la sensa ili lengo lililokusudiwa nifanikiwe ipasavyo.

 

Alisema waandishi wa habari ni kiyoo cha jamii  kwa kuelimisha , kuburudisha na  kuhamasisha hivyo kosa dogo la uandishi linaweza kuleta dosari kubwa nchini

 

Kwa upande wa mtoa mada Mkurugenzi wa Idara ya Viwango na uratibu,(OCGF) Ali Idrissa amesema sensa hii ni ya Mara ya sita kufanyika katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lakini Sensa ya safari hii itakuwa  ni ya aina yake kutokana na kutumika Teknolojia ya kisasa pamoja na kuhusisha   watu na makaazi.

 

Alifahamisha kuwa ni muhimu kila mtu akubali kuhesabiwa ili nchi ipate taarifa za msingi katika kupanga matakwa ya kusheria ya Takwimu ya Tanzania kwa Kila miaka 10.

 

Amesema Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ina dhamira ya kufanya sensa ya kipekee na ni moja ya matakwa ya Umoja wa Mataifa ya kuhakikisha inafanyika Sensa ya watu na makaazi nchini.

 

Sensa ya mwanzo ilifanyika katika mwaka 1967 ambayo ilipatikana idadi ya watu milioni 12.3 na makadirio Katika sensa ya 2022 ni watu milioni 61.3

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.