Habari za Punde

Benki ya Dunia Kuendelea Kuiunga Mkono ZanzibarKatika Sekta Mbalimbali za Maendeleo.

 

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt.Hussein Ali   Mwinyi (katikati)  akisisitiza jambo wakati wa mazungumzo na Ujumbe wa  Makamu wa Rais wa Benki ya Dunia anayesimamia Kanda ya Kusini mwa Afrika,(kushoto)   katika Ukumbi wa Ikulu Jijini Zanzibar leo (kulia) Viongozi wa taasisi mbali mbali za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar .[Picha na Ikulu] tr 12 julai 2022.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi ameipongeza Benki ya Dunia kwa kuendelea kuinga mkono Zanzibar katika sekta mbali mbali za maendeleo.

Rais Dk. Mwinyi ametoa pongezi hizo leo Ikulu Zanzibar, wakati alipofanya mazungumzo na Makamu wa Rais wa Benki ya Dunia anayesimamia Kanda ya Kusini mwa Afrika, Bi Victoria Kwakwa aliyefika Ikulu kwa ajili ya kujitambulisha sambamba na kueleza jinsi ya utekelezaji wa miradi iliyo chini ya Benki hiyo.

Katika pongezi hizo, Rais Dk. Mwinyi alieleza kwamba Benki ya Dunia ina historia ya muda mrefu katika kuiunga mkono Zanzibar kwenye sekta za maendeleo.

Rais Dk. Mwinyi alisema kuwa Zanzibar ni miongoni mwa nchi zilizoathirika na Uviko-19 hasa kupitia sekta ya utalii ambayo imekuwa na mchango mkubwa katika pato la taifa.

Hata hivyo alisema kwamba hivi sasa shughuli za utalii hapa nchini zimekuwa zikiimarika kila uchao mara kutokana na kutokuwepo kwa janga la Uviko-19 hatua ambayo inapelekea watalii kutoka nchi kadhaa duniani kuja kuitembea Zanzibar.

Aidha, Rais Dk. Mwinyi alimueleza kiongozi huyo hatua zilizofikiwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuendeleza miradi ya elimu na afya inayotokana na fedha za Uviko-19 zilizotolewa na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), ili kushuhulikia huduma za jamii.

Hivyo, Rais Dk. Mwinyi alitumia fursa hiyo kuishukuru na kuipongeza Benki ya Dunia kwa kuendelea kuisaidia Zanzibar katika miradi yake ya maendeleo huku akieleza vipaumbele vilivyowekwa na Serikali yake hivi sasa katika kuimarisha miundombinu ikiwemo barabara na bandari pamoja na kuimarisha sekta ya uchumi wa buluu.

Alieleza jinsi ya sekta ya Uchumi wa Buluu ilivyochukua nafasi kubwa katika sekta ya utalii, uvuvi, kuwasaidia akina mama wanaojishughulisha na kilimo cha mwani, bandari pamoja na sekta nyenginezo.

Rais Dk. Mwinyi alieleza hatua zilinazochukuliwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuhakikisha zao la mwani linapata thamani na wakulima wake wanafaidika na kilimo hicho ikiwa ni pamoja na kujenga kiwanda cha kusarifu mwani huko Chamanangwe, kisiwani Pemba.

Alimueleza Makamu huyo wa Rais jinsi Serikali anayoiongoza ilivyoweka kipaumbele na kutilia mkazo uimarishaji wa sekta ya elimu, maji,miundombinu ya barabara pamoja na huduma za kijamii huku akieleza juhudi zinazochukuliwa katika suala zima la kuongeza nishati ya umeme hapa Zanzibar.

Sambamba na hayo, Rais Dk. Mwinyi alimuhakikishia Makamu huyo wa Rais wa Benki ya Dunia kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendeleza uhusiano na ushirikiano uliopo kati yake na Benki hiyo hasa kwa kutambua juhudi inazozichukua katika kuiunga mkono Zanzibar kwenye sekta zake mbali mbali za maendeleo.

Nae Makamu wa Rais wa Benki ya Dunia anayesimamia Kanda ya Kusini mwa Afrika, Bi Victoria Kwakwa alimueleza Rais Dk. Mwinyi jinsi Benki ya Dunia inavyofarajika na juhudi za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuendeleza na kuimarisha miradi ya maendeleo inayosimamiwa na benki hiyo.

Makamu huyo wa Rais wa Benki ya Dunia alimueleza Rais Dk. Mwinyi hatua zinazochukuliwa na benki hiyo katika kuhakaikisha Zanzibar inafaidia kwa mara nyengine tena na fedha za utekelezaji miradi ya maendeleo kupitia dirisha jipya la Jumuiya ya Kimataifa ya Maendeleo (IDA 20).

Katika mazungumzo hayo, Bi Victoria Kwakwa alimuhakikishia Rais Dk. Mwinyi kwamba Benki ya dunia itaendelea kuunga mkono miradi ya maendeleo iliyopewa kipaumbele na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ikiwemo miundombinu ya barabara pamoja na sekta nyenginezo.

Alieleza kwamba Benki ya dunia imekuwa na ushirikiano mkubwa na Zanzibar katika Nyanja mbali mbali za kijamaii na kiuchumi ikiwemo ujenzi wa miundombinu, elimu, afya, mazingira na mengineyo mingi kupitia mpango wa mikopo nafuu.

Aidha, Bi Kwakwa alimueleza Rais Dk. Mwinyi kwamba janga la Uviko-19 limeweza kuathiri kwa kiasi kikubwa ukuaji wa uchumi kwa nchi kadhaa zinazotegemea sekta ya utalii na kueleza matarajio yake kwamba Zanzibar itarudi katika hali yake ya mwanzo.

Nae Waziri wa Fedha na Mipango Saada Mkuya Salum ambaye alifuatana na kiongozi huyo pamoja na ujumbe wake, alieleza jinsi mashirikiano mazuri yaliopo kati ya Benki ya Dunia na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Makamu wa Rais wa Benki ya Dunia anayesimamia Kanda ya Kusini mwa Afrika, Bi Victoria Kwakwa yuko nchini kwa ziara ya siku mbili kufuatia mwaliko wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan, ambaye anachukua nafasi ya aliyekuwa Makamu wa Rais wa Benki hiyo Dk. Hafez Ghanem ambaye amestaafu.

 

Imetayarishwa na Idara ya Mawasiliano,

Ikulu Zanzibar. OF RESPONSIBILITY

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.