Habari za Punde

Madalali wa Minada Kusajiliwa Kielektroniki.

Mkurungezi wa Takwimu za Uchumi, Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), Bw. Daniel Masolwa, (Kushoto) akiangalia vipeperushi kuhusu Mfumo wa Kielektroniki wa Utoaji Leseni za Udalali na Uendeshaji Minada ya Hadhara, alipotembelea banda la Wizara hiyo katika Maonesho ya Nanenane yanayofanyika kitaifa uwanja wa John Mwakangale, jijini Mbeya. Kulia ni Msimamizi wa mali za Serikali Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. George Killo, na katikati ni Afisa Masoko wa NBS Bw. Andrew Punjila.

Na. Rahma Taratibu na Hilda Mlay, SJMC, Mbeya.

Wizara ya Fedha na Mipango imeandaa mfumo wa kielektroniki wa utoaji Leseni za Udalali na Uendeshaji minada ya hadhara ambao utawezesha uombaji na upatikanaji wa Leseni kwa njia ya kielektroniki kwa kutumia simu za mkononi ili kuwaondolea wananchi adha na gharama ya kufuata leseni hizo Makao Makuu - Dodoma.

Akizungumza wakati akitoa elimu kwa wananchi waliotembelea banda la Wizara katika Maonesho ya Nanenane jijini Mbeya, Msimamizi wa mali za Serikali wizarani hapo, Bw. George Killo, alisema kuwa mfumo huo utamuwezesha mwananchi kufanya usajili popote alipo hivyo kupata leseni yake kwa wakati.

‘Mwombaji wa leseni ya udalali anapaswa kujisajili kupitia tovuti ya Wizara (www.mof.go.tz) na kisha kubonyeza kipengele cha GAMIS na kujisajili, kujaza taarifa zinazohitajika, kujaza fomu za maombi kikamilifu na kuwasilisha kwa Katibu Tawala wa Wilaya husika kwa ajili ya uhakiki na saini.’ Alieleza Bw. Killo.

Alisema mwombaji wa Leseni za Udalali na Uendeshaji Minada ya hadhara anahitajika kuwa na fumu ya maombi iliyojazwa kikamilifu na kugongwa mhuri na Katibu Tawala wa Wilaya husika, Tax Clearance Certificate/incorporation, leseni ya biashara pamoja na Tax Clearance Certificate na viambatisho hivyo viwe katika mfumo wa PDF.

Alisema kupitia mfumo huo mwombaji anaweza kupata taarifa za maombi yake ikiwa yametumwa, yamekataliwa au yamekamilika na waombaji waliofanikiwa wataorodheshwa Katika tovuti ya Wizara ya Fedha na Mipango na kuchukua leseni zao katika Ofisi ya Usimamizi wa Mali za Serikali katika mikoa yao. 

Bw. Killo alifafanua kuwa Leseni hizo zinatumika katika uendeshaji wa minada ya hadhara, ukusanyaji wa madeni, ushuru, tozo, udalali wa mahakama, udalali wa nyumba na viwanja na hutolewa kwa muda wa mwaka (Januari -Disemba) kwa Sh. 150,000/= na nusu mwaka (Januari – June) (Julai – Disemba) kwa Sh.75,000.

Alisema dalali yoyote ambaye anaendesha mnada wa hadhara anatakiwa awe amesajiliwa na awe na leseni ya halali ambayo haijaisha muda wake wa matumizi inayotolewa na Wizara yetu ya Fedha na Mipango.

Wizara ya Fedha na Mipango pamoja na Taasisi zilizochini yake inashiriki katika Maonesho ya Nanenane yanayofanyika kitaifa jijini Mbeya yenye kauli mbiu ‘Ajenda 10/30- Kilimo ni biashara, shiriki kuhesabiwa kwa mipango bora ya Kilimo, Uvuvi Na Mifugo”.

Afisa Ugavi wa Wakala wa Huduma ya Ununuzi Serikalini (GPSA) Bw. Francis Mwinyi, akimwelezea Bw. Frank Mhunda, kuhusu Mfumo mpya wa huduma ya ununuzi Serikalini uitwao GIMIS, alipotembelea banda la Wizara ya Fedha na Mipango katika Maonesho ya Nanenane yenye kauli mbiu ‘Ajenda 10/30 - Kilimo ni biashara, shiriki kuhesabiwa kwa mipango bora ya Kilimo, Uvuvi Na Mifugo”, yanayofanyika kitaifa uwanja wa John Mwakangale, jijini Mbeya.
Afisa Bima wa Mfuko wa Self Bw. Rasuli Sadala, akiwaelezea Bw. john pomela (kushoto) na Bw. Venance Raphael, kuhusu mikopo mbalimbali inayotolewa na Mfuko huo, walipotembelea banda la Wizara ya Fedha na Mipango katika Maonesho ya Nanenane yenye kauli mbiu ‘Ajenda 10/30 - Kilimo ni biashara, shiriki kuhesabiwa kwa mipango bora ya Kilimo, Uvuvi Na Mifugo”, yanayofanyika kitaifa uwanja wa John Mwakangale, jijini Mbeya.

Afisa Mipango – Mwandamizi wa Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana, (CMSA), Bw. Godfrey Laurent Makoi, (kushoto) na, Bw. Christopher Ngonyani, wakiwaeleza Bw. William Mgeni na Bi. Gladness Charles kuhusu uwekezaji kwenye hati fungani na hisa walipotembelea banda la Wizara ya Fedha na Mipango katika Maonesho ya Nanenane yenye kauli mbiu ‘Ajenda 10/30 - Kilimo ni biashara, shiriki kuhesabiwa kwa mipango bora ya Kilimo, Uvuvi Na Mifugo”, yanayofanyika kitaifa uwanja wa John Mwakangale, jijini Mbeya.

(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, WFM, Mbeya)


No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.