Habari za Punde

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe,.Hemed Suleiman Amefunga Kozi Fupi ya Uongozi.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla akiwakabidhi  Cheti mmoja wa Washiriki wa Kozi ya muda mfupi ya Kumi na Tatu ya Viongozi baada ya kukamilisha Kozi hiyo wakati wa Hafla ya ufungaji wa Kozi hiyo iliyofanyika katika Ukumbi wa Chuo cha Taifa cha Ulinzi Kunduchi Jijini Dar-es-salaam.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla akiwakabidhi  Cheti mmoja wa Washiriki wa Kozi ya muda mfupi ya Kumi na Tatu ya Viongozi baada ya kukamilisha Kozi hiyo wakati wa Hafla ya ufungaji wa Kozi hiyo iliyofanyika katika Ukumbi wa Chuo cha Taifa cha Ulinzi Kunduchi Jijini Dar-es-salaam.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla akiwa kwenye Picha ya pamoja na Washiriki wa Kozi fupi ya Kumi na Tatu ya Viongozi katika Hafla ya kufunga Kozi hiyo iliyofanyika Ukumbi wa Chuo cha Taifa cha Ulinzi Kunduchi Jijini Dar-es- Salaam.

Na.Abdulrahim Khamis.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla amewataka washiriki wa Kozi fupi ya Kumi na Tatu ya Uongozi kuongeza za kasi ya uwajibikaji kwa kuzingatia Usalama wa Taifa katika Majukumu yao.

Mhe. Hemed ameeleza hayo wakati akifunga Kozi ya Kumi na Tatu Fupi ya Viongozi iliyoandaliwa na Chuo cha Taifa Cha Ulinzi Kunduchi jijini Dar-es-salaam.

Ameeleza kuwa Masuala ya Usalama ni Sehemu ya Kuzingatia utendaji wa kazi kwa Kiongozi hasa wanaposimamia utekelezaji wa Sera za Nchi hivyo, ni vyema kuzingatia yote waliyojifunza katika Kozi hiyo ili kuongeza ufanisi zaidi katika kazi zao.

"Ni Imani yangu kuwa Mafunzo mliyoyapata yatakwenda kubadilisha kasi ya Utendaji kazi wenu, uwajibikaji, Nidhamu na kuongeza kiwango cha Uzalendo mlichonacho"

Mhe. Hemed ameeleza kuwa Serikali ina matumaini kwamba Mafunzo hayo yatasaidia kuleta fikra za kimkakati ambazo zitakuwa Chachu ya Mapinduzi ya Kimaendeleo kwa Taifa na ukanda Mzima wa Afrika Mashariki.

Mhe. Hemed amewataka Washiriki hao kuwa mfano kwa kuonesha utofauti katika utendaji wao ili kuwafunza walio katika ngazi zao za kiutendaji.

Sambamba na hayo Mhe. Hemed   ameeleza kuwa Serikali ina malengo makubwa ya kimaendeleo na kuwataka Washiriki hao kusimamia ukusanyaji wa Kodi na Matumizi mazuri ya Fedha za Serikali ili Tanzania iwe Nchi ya Viwanda na yenye Uchumi wa Kati na wa Juu.

Nae Kaimu Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa ambae pia ni Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mhandisi Hamad Yussuf Masauni ameeleza kuwa Jeshi la wananchi la Tanzania (JWTZ) ni Jeshi linalosifika kwa Nidhamu na Utii ukilinganisha na Majeshi ya Nchi nyengine.

Aidha Mhe. Masauni akiwa ni Mshiriki wa Kozi hiyo ameeleza kuwa Washiriki kwa pamoja wameahidi kuwa wabunifu na watiifu katika Kazi zao pamoja na kuongeza kasi ya Kazi kwa Maslahi mapana ya Nchi kwa kuzingatia Usalama wa Taifa.

Kwa upande wake Mkuu wa Chuo cha Taifa cha Ulinzi (NDC) Meja Jenerali Ibrahim Michael Mhona ameeleza kuwa Mafunzo hayo yamejumuisha Washiriki Hamsini na Tisa (59) ambapo wameweza kujifunza Usalama wa Taifa Kisera, kimkakati, Mipango na Usalama kwa Maslahi ya Tanzania.

Ameeleza kuwa Chuo kinatarajia ufanisi Mkubwa kwa Viongozi hao watakaporudi katika maeneo yao ya kazi na kukiri kuwa Washiriki hao wamefikia malengo ya kushiriki katika Kozi hiyo.

"Popote mutakapokuwa hakikisheni Taifa linabaki salama sisi Chuo tunakiri kuwa malengo ya Kozi hii yamefikiwa Hongereni sana"

 Afisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

05/08/2022.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.