Habari za Punde

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi Amewaapisha Viongozi Aliowateua Hivi Karibuni.

 

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akimuapisha Rajab Yussuf Khamis Mkasaba kuwa Mkuu wa Wilaya ya Kusini Unguja, hafla hiyo ya kuapishwa iliyofanyika leo 5-8-2022, katika ukumbi wa Ikulu Jijini Zanzibar na (kushoto kwa Rais) Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi Mhandisi Zena Ahmed Said. 

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi  Dk. Hussein Ali Mwinyi amewaapisha viongozi na watendaji mbali mbali wa Serikali kushika nyadhifa zao kufuatia uteuzi aliofanya  hivi karibuni.

 

Katika hafla hiyo iliofanyika ikulu  Zanzibar, Rais Dk. Mwinyi amemuapisha Juma Makungu Juma kuwa Naibu Waziri Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Makaazi pamoja na Masoud Hussein Idd kuwa Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Ikulu.

 

Aidha, Dk. Mwinyi alimuapisha Dk. Maua Abeid Daftari kuwa Kamishna wa Tume ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Rashid Ali Salim kuwa Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Biashara na Maendeleo ya Viwanda pamoja na Rajab Yussuf Mkasaba kuwa Mkuu wa Wilaya Kusini Unguja.

 

Hafla hiyo ya Kiapo ilihudhuriwa na Viongozi mbali mbali wa Kitaifa na Chama cha Mapinduzi, akiwemo Jaji Mkuu wa Zanzibar Khamis Ramadhan Abdalla, Mwanasheria Mkuu wa Serikali Dk. Mwinyi Talib Haji , Katibu Mkuu Kiongozi Mhandisi Zena Ahmeid Said pamoja na Naibu Katibu Mkuu CCM Zanzibar Abdalla Juma ‘Mabodi’.

 

Wengine ni Mufti Mkuu wa Zanzibar Sheikh Saleh Omar Kaab, Spika wa Baraza la Wawakilishi Zubeir Ali Maulid, Mawaziri, Mkuu wa Mkoa Mjini Magharibi Idrissa Kitwana Mustafa, Meya wa Jiji la Zanzibar Mohamed Mahamoud Mussa,  Wakuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama, Viongozi wa Dini pamoja na Wanafamilia.             

  

Imetayarishwa na Idaya ya Mawasiliano

Ikulu Zanzibar.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.