Habari za Punde

Serikali itaendelea kuwekeza katika sekta ya elimu kwenye ujenzi wa miundombinu ya taasisi za elimu, kuzipatia vitendea kazi vikiwemo vifaa vya kusomea na kusomeshea na kutoa mafunzo kwa walimu ili wapate mbinu bora

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Mwinyi akihutubia katika  chakula maalum na kuwapongeza na kuwazawadia zawadi  Wanafunzi wa Kidatu cha Nne na cha Sita Unguja waliofanya vizuri Mitihani yao ya Taifa na kufaulu vizuri, hafla hiyo iliyofanyika katika viwanja vya Ikulu Jijini Zanzibar leo 3-8-2022
 

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi amesema kuwa dhamira ya Serikali ya Awamu ya Nane ni kuona kwamba kiwango cha ufaulu wa wanafunzi wa Skuli za Zanzibar unazidi kuimarika kila mwaka katika mitihani yao ya Taifa.

Rais Dk. Mwinyi aliyasema hayo leo katika hafla ya chakula alichowaandalia wanafunzi waliofaulu vyema zaidi katika mitihani ya Taifa ya Kidato cha Nne mwaka 2021 na Kidato cha Sita mwaka 2022, hafla iliyofanyika katika viwanja vya Ikulu ya Zanzibar.

Kwa mnasaba huo Rais Dk. Mwinyi alisema kuwa Serikali itaendelea kuwekeza katika sekta ya elimu kwenye ujenzi wa miundombinu ya taasisi za elimu, kuzipatia vitendea kazi vikiwemo vifaa vya kusomea na kusomeshea na utoa mafunzo kwa walimu ili wapate mbinu bora za kufundishia.

Rais Dk. Mwinyi aliwaahidi kuwapatia Kompyuta mpakato ‘laptop’ wanafunzi wote wa Kitado cha Sita na Kidato cha Nne waliopata daraja la kwanza wa Unguja na Pemba.

Pia, Rais Dk. Mwinyi aliwaeleza wanafunzi waliofaulu kidato cha Sita kwamba wote watapata mikopo ya Elimu ya Juu na kusisitiza kwamba Serikali itahakikisha inaiwekea mazingira mazuri bodi hiyo huku akiwaleza wkamba wana fursa ya kutumia bodi zote mbili za mikopo ikiwemo ile ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Rais Dk. Mwinyi alisisitiza haja kwa Wizara ya Elimu kufanya mashindano baina ya Skuli na Skuli, Mikoa na Mikoa pamoja na Wilaya kwa Wilaya kwani ushindani unaleta matokeo mazuri.

Katika kuzithamini juhudi za wanafunzi hao Rais Dk. Mwinyi ametoa nafasi za udhamini wa masomo “Scholaship” kwa wanafunzi 30 waliofanya vizuri katika mitihani yao ili kuendelea na masomo katika vyuo mbali mbali.

Alitoa pongezi kwa skuli binafsi  ambazo nazo zimekwua zikifanya vizuri na kuweza kuisaida Serikali katika kupunguza mzigo wa wanafunzi katika skuli zilizopo za serikali.

Sambamba na hayo, aliahidi mafunzo na maslahi kwa walimu na kuahidi kwamba Serikali anayoiongoza itahakikisha inayazingatia.

Nae Waziri wa Elimu Leila Mohamed Mussa alieleza mikakati iliyowekwa na Wizara hiyo katika kuimarisha sekta ya elimu huku akiwanasihi wanafunzi waliopata daraja la kwanza wa kidato cha Nne na Sita kujitambua na kuthamini jambo hilo walilofanyiwa na Rais.

Nae Naibu katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Ali Abdulgulam… alieleza kwamba mafanikio hayo yote yametokana na mashirikiano ya pamoja kati ya uongozi wa Wizara hiyo, watendaji,walimu pamoja na wazazi.

Nae Katibu mkuu Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar  Ali Khamis Juma akitowa Takwimu za uafaulu wa wanafunzi alisema Mtihani ya kidato cha nne ulifanyika mwezi Novemba 2021 na matokeo yake yalitoka January 2022 ambao jumla ya wanafunzi 15,569 walifanya mtihani huo na wanafunzi 4,403 wamefanikiwa kuendelea namasomo ya kidato cha tano Julai 2022.

Alifahamisha kuwa ufaulu wao ni kati ya daraja la kwanza hadi la tatu na ni sawa na asilimia 28.3, kati  ya wanafunzi hao ,wanafunzi 445 walipata daraja la kwanza ambapo  nisawa na asilimia 2.8 tu, ambao 308 ni miongoni mwao ambao wamefika Ikulu ya Mnazimmoja hivi leo.

Alisema mtihani wa kidato cha sita ulifanyika Mei 2022 na matokeo yake yalitokea mwezi Julai 2022 ambapo jumla ya wanafunzi 3,683 walifanya mitihani na wanafunzi 3,644 waliofaulu kuendelea na masomo kwa ngazi ya elimu ya juu katika vyuo vya ndani na nje kwa fani zote ambazo Serikali itawekea kipaumbele kulingana na mahitaji yake.

Alisema kuwa kati ya wanafunzi hao, wanafunzi 693 walipata daraja la kwanza, ambapo 542 ndio waliofika katika hafla hiyo ya chakula na zawadi Ikulu Zanzibar.

Alisema takwimu za ufaulu kwa kidato cha nne yamekuwa  za kutia moyo mwaka hadi mwaka kwa vile kuna ishara zilizowazi za kuimarika na hivyo kuifanya Zanzibar nayo kuwa ni mshindani halisi kwenye matokeo ya mitihani katika mikoa ya hapa nchini.

Katibu Mkuu huyo alisema kuwa Wizara inafanya jitihada za makusudi kuona kuwa matokeo ya mitihani ya kidato cha 4 na 6 yanakuwa mazuri na yenye kupendeza ambapo kuanzia mwaka huu, Wizara hiyo inakusudia kuongeza ufaulu angalau kwa wastani wa asilimia 5 kwa kila mwaka.

“Matokeo yote haya ni mazuri sana na mara ya kwanza kutokea tangu Mapinduzi matukufu ya Zanzibar ya mwaka 1964, matokeo haya yamekuja chini ya uongozi wako mahiri wa Serikali ya Awamu ya Nane, nidhahiri kuwa mafanikio yanakisi ile slogan yako ya uchaguzi kuwa ‘Yajayo yanafurahisha, yajayo ni neema tupu’,alisema.

Rais Dk. Mwinyi pia alitoa zawadi kwa wanafunzi waliofanya vizuri zaidi wakiwemo wanafunzi watatu waliopata kompyuta mpakato ‘laptop’  akiwemo mwanafunzi mwanafunzi bora katika Tahasusi ya ECA (Economic,Commerce na Account) Nasra Ali Omar ambaye pia anaingia katika kundi la wanawake 10 bora Tanzania.

Imetayarishwa na Idara ya Mawasiliano,

Ikulu Zanzibar.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.