Habari za Punde

Dirisha la Maombi SAMIA SCHOLARSHIP Lafunguliwa kwa Wanafunzi 640 Waliopata Ufaulu wa Juu

Serikali kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imefungua dirisha la maombi ya SAMIA  SCHOLARSHIP kwa wanafunzi 640 waliopata ufaulu wa juu kwenye masomo ya sayansi katika mitihani ya Kidato cha Sita 2022.

Majina ya wanafunzi hao yanapatikana kuanzia leo katika tovuti ya Wizara www.moe.go.tz na ya Bodi ya Mikopo ya wanafunzi wa Elimu ya Juu www.heslb.go.tz.  Aidha wanafunzi hao wataanza kuomba ufadhili huo kuanzia  kesho Septemba 28, 2022  kupitia tovuti ya Bodi ya Mikopo ya Mikopo https://olas.heslb.go.tz kwa siku 14.

Akitoa tangazo hilo leo Septemba 27, 2022 jijini Dodoma Waziri Mkenda amesema wanafunzi hao watafadhiliwa kwa asilimia mia moja kwa kipindi cha miaka mitatu hadi mitano kulingana na programu husika walizodahiliwa.

Amefafanunua kwamba wanafunzi hao ni wale Tahasusi za sayansi ambazo PCB, PCM, PGM, CBG, CBA, PMC na CBN.

"SAMIA SCHOLARSHIP itagharamia kwa asilimia mia moja masomo ya Chuo Kikuu kwa wanafunzi ambao wamepata udahili katika fani za Teknolojia, Uhandisi, Hisabati na Tiba katika Chuo kikuu hapa nchini kinachotambulika na Serikali ," amesema Waziri Mkenda

Prof. Mkenda amesema ufadhili huo utazingatia viwango na miongozo ya Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya juu kwa kugharamia ada ya mafunzo, Posho ya chakula na malazi, vitabu na viandikwa, mahitaji maalum ya vitivo, mafunzo kwa vitendo, utafiti, vifaa saidizi kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum na bima ya Afya.

Waziri Mkenda ametaja masharti saba ya ufadhili huo ikiwemo kiwango cha ufaulu wa mnufaika kisiwe chini ya GPA 3.8 katika mwaka wa masomo na chini ya hapo ufadhili utasitishwa.

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Mhe. Ali Abdulgullam Hussein amepongeza hatua ya Serikali kutoa ufadhili huo  ambapo kwa upande wa Zanzibar ufadhili wa aina hiyo pia umetolewa kwa wanafunzi 30 hivyo kuongeza fursa kwa watoto wa kitanzania kupata elimu ya juu.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.