Habari za Punde

Kiswahili Kinakuza Diplomasia ya Uchumi Jumuiya ya Afrika Mashariki

 
Balozi wa Tanzania nchini humo Mhe. Dkt. Jilly Elibariki Maleko akichangia wakati wa wasilisho la mada ya “Lugha Ya Kiswahili Inamchango Mkubwa katika Kukuza Diplomasia ya Uchumi” Septemba 07, 2022 Bujumbura nchini Burundi.

Na Eleuteri Mangi-WUSM

Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA) pamoja na Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT) kupita tawi lake la mkoa wa Kigoma kutumia fursa ya kufundisha Kiswahili nchini Burundi kwa kuanzisha programu fupi fupi za kufundisha lugha hiyo ili kukuza diplomasia ya uchumi miongoni mwa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).

Akichangia mada wakati wa wasilisho la mada ya “Lugha Ya Kiswahili Inamchango Mkubwa katika Kukuza Diplomasia ya Uchumi” Septemba 07, 2022 Bujumbura nchini Burundi, Balozi wa Tanzania nchini humo Mhe. Dkt. Jilly Elibariki Maleko amesema huu ni muda mwafaka kwa taasisi zinazofundisha Kiswahili kuongeza kasi ya kukuza na kueneza lugha hiyo miongoni mwa nchi za jumuiya hiyo.

Ili kukabiliana na hali hiyo, Mhe. Balozi Dkt. Jilly amesema ni muhimu kuwa na programu ya kufundisha walimu nchini Burundi ili waweze wao wenyewe kujitegemea katika kufundisha Kiswahili katika maeneo yao kuanzia ngazi ya shule za msingi, sekondari hadi Chuo Kikuu.

Aidha, Balozi Mhe. Dkt. Jilly amelitaka Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA) ambalo ni taasisi ya Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo pamoja na taasisi zinazojushughulisha maendeleo ya Kiswahili zisaidie katika kukuza na kueneza lugha hiyo miongoni mwa nchi wanachama wa jumuiya hiyo.

“BAKITA na taasisi zingine zitusaidie sasa katika utekelezaji wa hati ya makubaliano ili tuweze kuwasaidia wenzetu wanahitaji walimu, tunasaidiana vizuri sana katika kuhamasisha matumizi ya Kiswahili hapa Burundi, tunashirikiana kwa karibu na Chuo Kikuu cha Burundi, wanahitaji sana walimu katika shule za msingi na sekondari ambapo hawana walimu wa Kiswahili kabisa” Mhe. Balozi Dkt. Jilly.

Akiwasilisha mada kuhusu lugha ya Kiswahili inavyoweza kukuza Diplomasia ya Uchumi kwa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki wakati wa Tamasha la Tano la Sanaa na Utamaduni la Jumuiya ya Afrika Mashariki (JAMAFEST) linalofanyika kuanzia Septemba 4-12, 2022 nchini Burundi, Dkt. Rizati Hassani Mmary kutoka Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA) amesema Kiswahili kinakua kwa kasi katika nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kupitia miradi inayotekelezwa ikiwemo kufundisha Kiswahili kwa wageni, Muziki na filamu, biashara, utalii na hivyo kuwa na mchango mkubwa katika kukuza diplomasia ya uchumi miongoni mwa nchi wanachama wa jumuiya hiyo.

Dkt. Rizati Hassani Mmary kutoka Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA) akiwasilisha mada kuhusu “Lugha ya Kiswahili Inavyoweza Kukuza Diplomasia ya Uchumi kwa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki” Septemba 07, 2022 wakati wa Tamasha la Tano la Sanaa na Utamaduni la Jumuiya ya Afrika Mashariki (JAMAFEST) linalofanyika kuanzia Septemba 4-12, 2022 Bujumbura nchini Burundi.

Mkurugenzi wa Miundombinu ya Kiuchumi na Huduma za Usaidizi wa Kijamii Eliabi Khalid Chodota akichangia wakati wa wasilisho la mada ya “Lugha Ya Kiswahili Inamchango Mkubwa katika Kukuza Diplomasia ya Uchumi” Septemba 07, 2022 Bujumbura nchini Burundi.


Washiriki wakifuatilia mada kuhusu “Lugha ya Kiswahili Inavyoweza Kukuza Diplomasia ya Uchumi kwa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki” Septemba 07, 2022 wakati wa Tamasha la Tano la Sanaa na Utamaduni la Jumuiya ya Afrika Mashariki (JAMAFEST) linalofanyika kuanzia Septemba 4-12, 2022 Bujumbura nchini Burundi.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.