Habari za Punde

Mabalozi Wapokea Nyenzo za Kiswahili

Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Pauline Gekul akiongea na Mabalozi Septemba 20, 2022 Mtumba, Mji wa Serikali jijini Dodoma; Mhe. Simon Sirro Balozi wa Tanzania nchini Zimbabwe (watatu kushoto), Mhe. Caroline Chipeta Balozi wa Tanzania nchini Uholanzi (wa kwanza kushoto) na Mhe. Luteni Generali Mathew Mkingule Balozi wa Tanzania nchini Zambia (wa pili kushoto). Wa pili kulia ni Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo Bw. Saidi Yakubu.

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo Bw. Saidi Yakubu akimkabidhi Mhe. Simon Sirro Balozi wa Tanzania nchini Zimbabwe vitabu vya kufundishia Kiswahili Septemba 20, 2022 Mtumba, Mji wa Serikali jijini Dodoma.

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo Bw. Saidi Yakubu akimkabidhi Mhe. Luteni Generali Mathew Mkingule Balozi wa Tanzania nchini Zambia vitabu vya kufundishia Kiswahili Septemba 20, 2022 Mtumba, Mji wa Serikali jijini Dodoma.

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo Bw. Saidi Yakubu akimkabidhi Mhe. Caroline Chipeta Balozi wa Tanzania nchini Uholanzi vitabu vya kufundishia Kiswahili Septemba 20, 2022 Mtumba, Mji wa Serikali jijini Dodoma.

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo Bw. Saidi Yakubu akiwa katika picha ya pamoja na Mabalozi; Mhe. Simon Sirro Balozi wa Tanzania nchini Zimbabwe, Mhe. Caroline Chipeta Balozi wa Tanzania nchini Uholanzi na Mhe. Luteni Generali Mathew Mkingule Balozi wa Tanzania nchini Zambia


Na Eleuteri Mangi, WUSM.

Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo kupitia Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA) imewapatia vitabu Mabalozi wa Tanzania nchini Zimbabwe, Zambia na Malawi ambavyo ni nyenzo ya kubidhaisha lugha ya Kiswahili katika nchi mbalimbali duniani.

Mabalozi hao ambao wamefanya ziara y Wizarani Dodoma leo Septemba 20, 2022 ni Mhe. Simon Sirro Balozi wa Tanzania nchini Zimbabwe, Mhe. Caroline Chipeta Balozi wa Tanzania nchini Uholanzi na Mhe. Luteni Generali Mathew Mkingule Balozi wa Tanzania nchini Zambia.

Vitendea kazi walivyokabidhiwa ni vitabu vya vya kufundishia lugha ya Kiswahili ikiwemo Kamusi Kuu ya Kiswahili Toleo la Tatu la 2022, Mwongozo wa Kufundisha Kiswahili kwa Wageni pamoja na kitabu cha Furahia Kiswahili ambavyo vyote ni nyenzo ya kukuza na kueneza lugha ya Kiswahili katika nchi wanazoenda kufanyakazi.

Akizungumza na Mabalozi hao Ofisini kwake Mtumba Mji wa Serikali jijini Dodoma, Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Pauline Gekul amesema Mabalozi hao wameipa lugha ya Kiswahili kipaumbele, ndiyo maana wameona ni vema kabla ya kwenda kwenye vituo vyao vya kazi wafike Wizarani kupata nyenzo za kufanyika kazi ili kueneza lugha hiyo kwenye nchi walizopangwa kufanyakazi.

Naye Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Bw. Saidi Yakubu amewahimiza Mabalozi hao kuwa wawakilishi wa nchi kwa kuhakikisha wanaongeza mikataba (MOU) ya kufundisha Kiswahili katika nchi wanazokwenda kufanya kazi vikiwemo vyuo vikuu vya nchi hizo, kuhimiza kuanzishwa kwa vituo vya kufundisha Kiswahili, kutumia programu tumizi ya TEHAMA kufundisha Kiswahili inayojulikana “Swahili Prime” pamoja na kuwahimiza Watanzania kutumia fursa ya lugha ya Kiswahili katika nchi hizo ikiwemo ukalimani.

Kwa upande wake Mhe. Caroline Chipeta Balozi wa Tanzania nchini Uholanzi kwa niaba ya Mabalozi waliofika Wizarani hapo amesema kuwa Tanzania ndiyo msingi wa lugha ya Kiswahili, hivyo wanawajibu wa kukikuza na kukibidhaisha Kiswahili kwa kuwa ni kipaumbele cha Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Aidha, Balozi Mhe. Chipeta ameongeza kuwa watatumia fursa hiyo kuanzisha madarasa ya kufundishia Kiswahili kwenye vituo vyao vya kazi ili kuongeza kasi ya kukuza na kuieneza lugha ya Kiswahili duniani.

Mkurugenzi wa Maendeleo ya Utamaduni Dkt. Emmanuel Temu, Mkurugenzi Msaidizi Dkt. Resani Mnata pamoja na Katibu Mtendaji wa BAKITA Bi Consolata Mushi wamehudhuria kikao hicho. 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.