Habari za Punde

Mkuu wa Wilaya ya Kusini Unguja Mhe.Rajab Mkasaba Azindua Uvunaji wa Zao la Tungule Shamba la kikundi cha Kumekucha Mzuri Makunduchi.

 

MKUU wa Wilaya ya Kusini Unguja Mhe.Rajab Yussuf Mkasaba amezindua ufunaji wa zao la Tungule kwa Kikundi cha Wanaushirika wa Kumekucha kiliopo Shehia ya Mzuri Makunduchi kwa kuzitumia vyema fedha za mkopo wa Uviko 19 na kuweza kuendeleza kilimo cha mbogamboga ambacho kinawapatia tija na kujikwamua kimaisha.
MKUU wa Wilaya ya Kusini Unguja Mhe.Rajab Yussuf Mkasaba akiwa amebeba ndoo ikiwa na tungule baada kuzindua uvunaji wa zao hilo, katika shamba la Kikundi cha  Kumekucha Mzuri Makunduchi Wilaya ya Kusini Unguja.

MKUU wa Wilaya ya Kusini Mhe.Rajab Yussuf Mkasaba akiwa katika picha ya pamoja na Wanakikundi cha Kumekucha cha Shehia ya Mzuri Makunduchi,baada ya kuzinduzi ufunaji wa zao la Tungule.Wanaushirika wa kikundi hicho kwa kuzitumia vyema fedha za mkopo wa Uviko 19 na kuweza kuendeleza kilimo cha mbogamboga ambacho kinawapatia tija na kujikwamua kimaisha.

MKUU wa Wilaya ya Kusini Rajab Yussuf Mkasaba amewapongeza Wanaushirika wa kikundi cha Kumekucha kiliopo Shehia ya Mzuri Makunduchi kwa kuzitumia vyema fedha za mkopo wa Uviko 19 na kuweza kuendeleza kilimo cha mbogamboga ambacho kinawapatoa tija na kujikwamua kimaisha.

Mkuu huyo wa Wilaya ya Kusini ametoa pongezi hizo huko katika shamba la Ushirika wa Kumekucha liliopo Shehia ya Mzuri Makunduchi, Wilaya ya Kusini, Mkoa wa Kusini Unguja mara baada ya kuzindua uvunaji wa tungule (nyanya) huko katika shamba la Ushirika huo.

Mkasaba alitumia fursa hiyo kumpongeza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi kwa kuwakumbuka Wajasiriamali na kuwawekea fedha nyingi ili waweze kukopa na kuendesha shughuli zao za kimaendeleo.

Alisema kuwa Ushirika huo umeonesha mfano mkubwa wa kuthamini fedha za mkopo ambazo wameweza kuzifanyia mradi mkubwa wa kilimo cha mboga mboga.

Aliwahakikishia Wanaushirika hao kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar chini ya uongozi wa Rais Dk. Mwinyi itaendelea kuwaunga mkono wajasiriamali wote ili kuhakikisha wanafikia lengo walilolikusudia katika kupambana na umasini na kujikwamua kiuchumi.

Aidha, Mkuu huyo wa Wilaya ya Kusini aliwasisitiza Wanaushirika hao waendelee kushirikiana ili waweze kupata maendeleo makubwa zaidi katika Ushirika wao.

Sambamba na hayo, aliwaeleza kwamba iwapo wataendelea na juhudi zao hizo walizozichukua katika kuimarisha sekta ya kilimo kwa kujikusanya pamoja na kuunda ushirika huo na kuweza kuomba mkopo na kuutumia vizuri hivyo kuna uwezekanao mkubwa wa kupewa kipaumbele pale watakapomaliza mkopo na kuamua kukopa kwa mara nyengine tena.

Akisoma risala ya Ushirika huo kwa Mkuu wa Wilaya, Bi Rehema Issa Ameir ambaye ni miongoni mwa Wanakikundi cha Kumekucha alisema kuwa mnamo Juni 6,2022 waliweza kupata mkopo ambao ulizinduliwa na Rais Dk. Mwinyi.

Hivyo, Wanaushirika hao walimpongeza Rais Dk. Mwinyi kwa juhudi zake hizo ambazo zimewapelekea hivi sasa kuanza kuonja matunda yake “ Tunampongeza sana kwa jitihada zake hizo na leo tunakukaribisha wewe mwenyewe kuona maendeleo ya Dk. Hussein Ali Mwinyi”, alisema Bi Rehema.

Akieleza historia fupi ya Ushirika huo, Bi Rehema alisema kuwa Ushirika huo ulianzishwa Machi 3, 2012 ukiwa na wanachama 20 ukianzia na shughuli za kilimo cha migomba kwa muda na baadae wakaona haja ya kuingia katika kilimo cha mboga mboga ambacho hadi leo wanaendelea nacho.  

Pamoja na hayo, Wanaushirika hao walieleza changamoto waliyonayo ambayo ni kukosa umeme wa uhakika na usio salama kwa ajili ya kuendeleza shughuli zao za kilimo.

Imetayarishwa na Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Kusini,

Mkoa wa Kusini Unguja.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.