Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango Bw. Lawrence
Mafuru (kulia ) Pamoja na timu ya Wizara ya Fedha na Mipango walipotembelea
kiwanda cha Tanzania Breweries Ltd. (TBL) kushoto ni Mkurugenzi
wa Masuala ya Ushirikiano TBL Bi. Lucia Mwamboka.
Naibu Katibu
Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango Bw. Lawrence Mafuru (katikati) akimsikiliza
Mkurugenzi wa Mahusiano Serengeti Breweries Ltd Bw. John Wanyancha (kushoto), kulia ni
Kamishna wa Sera Bw. Elijah Mwandumbya wa Wizara ya Fedha na Mipango.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango Bw. Lawrence
Mafuru akiwa kwenye majadiliano na timu ya kiwanda cha bia cha Tanzania
Breweries Ltd (TBL) jijini Dar es Salaam. Kushoto ni timu ya Wizara ya Fedha na
Mipango na kulia ni timu ya TBL.
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Wizara ya Fedha na Mipango inataka kuangalia upya tozo za stempu za kielektroniki (ETS) ambazo kwa miaka mitatu iliyopita sekta ya viwanda imekuwa ikilalamika kuwa tozo hizi zimekuwa kubwa, hayo yamesemwa na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango Bw. Lawrence Mafuru alipokuwa katika ziara ya kutembelea viwanda vya kutengeneza bia vyaTanzania Breweries Ltd na Serengeti Breweries Ltd jijini Dar es Salaam.
“Kuna
haja ya Serikali kusikiliza hoja hii haiwezekani kwamba kuna kitu ambacho
wenzetu wanakiona na sisi hatukioni. Kwa mrejesho ambao tumeupata na sisi
tumejionea mfumo unavyofanya kazi, lakini pia tumepata fursa ya kuona mfumo
mwingine ambao unafanya kazi sambamba na mfumo unaolalamikiwa, sasa huo
mwingine unatumia ‘block chain technology’ ni almost bure na sasa tunajiuliza
nini ambacho hatukioni; ambacho wenzetu wanakiona,”Alisema Bw. Mafuru
Bw.
Mafuru alisema kuwa atawasiliana na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ili waeleze
kwa kina ni nini hasa ambacho wamekibaini kwenye huo mfumo.
“Wawekezaji hawa ambao wako tayari na hawapingi mfumo wa stempu za kielektroniki
wanausapport kabisa ila wanachokisema una gharama na kwa hakika ukiangalia
gharama zinazozungumzwa kama zingekuwa hazilipwi maana yake ni kwamba zingekuwa
sehemu ya mapato ya Serikali.” Alisema Bw. Mafuru
Bw.
Mafuru alisema nia hasa ya kufanya ziara hii ni kutimiza wajibu wa Wizara ya Fedha
katika eneo la kusimamia uchumi kwani maendeleo ya nchi pamoja na uchumi wa
Tanzania unategemea sana ushiriki wa sekta binafsi katika uzalishaji na utoaji
wa ajira.
“Ziara
hii imelenga kutuwezesha sisi kuelewa kwanza changamoto ambazo wenzetu kwenye sekta
hii hasa sekta ya utengenezaji wa vinywaji, changamoto gani wanazopitia Pamoja
na kupata mrejesho kutoka kwao kuhusu sera za hivi karibuni za kibajeti ambazo
tumezipitisha kupitia bajeti ya Serikali, Sheria ya fedha lakini pia utekelezaji wa ile
blue print, ambayo Serikali imekuwa ikiendelea kutekeleza. Hivyo tunafanya jitihada ya kupata
mrejesho na hatimae tuweze kujua wapi ambapo tunahitaji kuongeza jitihada, wapi
tunafanya vizuri na wapi hatufanyi vizuri ili tuweze kurekebisha kwa kujua
kwamba tutakapoendelea kurekebisha maeneo hayo basi tutaendelea kuifungua nchi
yetu kiuchumi” Alisema Bw. Mafuru
Aidha
Bw. Mafuru alisema jambo muhimu sana ambalo ameliona ni kwamba; kuna haja
Serikali kufanya kazi kwa Pamoja kwani kila
mtu akifanya kazi kwenye eneo lake peke yake atairudisha nyuma na kuiuchelewesha
Serikali.
Alisema kuwa Kuna hoja ambazo viwanda hivyo
vimeziibua ambazo zinahitaji Taasisi na Wizara
zingine za kisekta ziweze kuingilia na kufanya maamuzi kwani kuna maamuzi yako
tangu mwaka 2016 ambayo yangetakiwa kufanyika ili kwa wanaohitaji kuwekeza
waweze kuwekeza. Hivyo amesema wamechukua hili angalizo na watakaa na TRA ili
kujua nini hasa hoja yao.
Bw.
Mafuru aliongeza kuwa ili kuongeza uwekezaji nchini inapaswa kuwawekea
mazingira rafiki ya kuwa na uhakika kama mitaji yao iliyopo hapa Tanzania
italindwa ili waweze kuleta mitaji mingine.
“Makampuni
yote mawili tuliyoyatembelea leo yana
mipango ya kuongeza uwekezaji wao nchini lakini kuna kitu kinang’ang’ania
kwenye mawazo yao ya kutokuwa na uhakika
kama mambo yale ambayo yana miaka mitatu,
minne hayajashughulikiwa ni kitu gani kinawapa guarantee waje kuongeza mitaji
yao, kwa hiyo kuna hoja hapa ambayo na sisi tumepata mrejesho ambao tutakwenda
kushare na wenzetu Serikalini na Mamlaka zinazohusika kwa lengo la kuratibu na
jitihada za Serikali ili tuweze kuyashughulikia haya mambo ambayo ni kikwazo
katika ukuzaji wa hizi sekta”. Alisema Bw. Mafuru
Bw.
Mafuru alisema kuhusu fursa za uwekezaji, kuna changamoto ya upungufu kwenye
soko la chupa za kujaza bia na
uzalishaji huo umekuwa kwa muda mrefu unategemea kiwanda kimoja tu hapa nchini. Kwa kuwa wametuambia wengine wako chini ya
kiwango chao cha uzalishaji na kwa sababu tu ya ukosefu wa chupa, hii inatuambia kisera inabidi kufanyike jitihada za
kuwezesha sekta hiyo ya uzalishaji wa chupa ili kuweza kuongeza uzalishaji huu.
“Kwa
hivyo ni sekta ambayo iko coordinated tukijua kwamba sasa kuna changamoto ya
chupa na tutaongea na Wenzetu wa Wizara ya Viwanda Biashara na Uwekezaji waweze kuangalia namna gani wana fast truck
wawekezaji ambao wanaweza kuwekeza katika ilo eneo kwa sababu kuna fursa na
bahati nzuri fursa hii sio tu kwa Tanzania chupa zetu zinauzwa hadi nchi Jirani
kwa hiyo itatusaidia kupata fedha za kigeni kwa hivyo ukiona ni bia lakini
inapanua na mambo mengine ambayo ndio uchumi wenyewe. Alisema Bw. Mafuru
Kwa
upande wa Mkurugenzi wa Masuala ya Ushirikiano TBL Bi. Lucia Mwamboka alisema
wana matumaini kwamba mazungumzo
yaliyofanyika leo na timu ya Wizara ya Fedha na Mipango yataleta tija kwa nchi
na wako tayari kutoa ushirikiano kwa Serikali kwa lengo la kutanua wigo wa
kukusanya kodi. Pia aliongezea kwenye suala la stempu za kielektroniki alisema
kuwa ni mfumo mzuri ambao ulianzishwa na TRA lakini bei ni kubwa japo wanaamini
kuwa Serikali inalifanyika kazi.
Naye
Mkurugenzi wa Mahusiano Serengeti Breweries Ltd Bw. John Wanyancha alisema wamerafijika sana
kwa ujio wa viongozi kutoka Serikalini Wizara ya Fedha na Mipango kusikilia
malalamiko yao na kuona jinsi ambavyo wanafanya kazi. Wanaamini kwamba hii
ziara ya Serikali kuja kuwasilikiliza wawekezaji ni njia nzuri sana ya kuleta
mageuzi chanya katika maendeleo ya viwanda hapa Tanzania.
Katika
suala la huduma za kijamii Serengeti Breweries Company Ltd. wameweza kuzalishaji
ajira za moja kwa moja katika kiwanda chao, pia jukumu la usafirishaji linafanywa
na kampuni binafsi ya Watanzania ambao wanapata kipato chao kutokana na sekta
hii ya uzalishaji bia. Pia wanatoa ufadhili kwa wataalamu wa kilimo kwa sababu
wana utaratibu wa kununua ngano ambayo
wanaitumia kutengeneza bia. Hivyo wataalamu ambao waliwasomesha ndio
wanaosaidia kutoa elimu ya kuboresha mazingira ya uzalishaji kwenye mashamba
yao.
Sekta
hizi za vinywaji ndio hasa zimekuwa kinara katika uchangiaji kwenye eneo la kodi
ni vyema Serikali ifanye jitihada za kutatua changamoto zao ili waendelee
kuchangia kwa sehemu kubwa na waendelee kukua na kuongeza ajira, kuleta
maendeleo ya kiuchumi ambayo ndiyo matarajio ya Serikali.
No comments:
Post a Comment