Habari za Punde

MAKAMU WA PILI AKAGUA MAANDALIZI YA UZINDUZI WA MATOKEO YA SENSA DODOMA

Na.Abdulrahim Khamis.OMPR

Wananchi wa Mkoa wa Dodoma na Mikoa Jirani wametakiwa kushiriki katika Hafla ya Uzinduzi wa Matokeo ya Awali ya Sensa ya Watu na Makazi hafla inayotarajiwa kufanyika Oktoba 31 Mwaka huu.

Mwenyekiti Mwenza wa Kamati ya Kitaifa ya Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022 Mhe. Hemed Suleiman Abdulla ametoa Wito huo wakati akizungumza na Vyombo vya Habari baada ya ukaguzi na  kupokea Taarifa ya Maandalizi ya Hafla ya Uzinduzi wa Matokeo ya Awali ya Sensa ya Watu na Makazi katika Uwanja wa Jamhuri Jijini Dodoma.

Ameeleza kuwa Zoezi la Sensa ya Watu na Makazi la Mwezi Agosti Mwaka huu limekamilika kwa Asilimia kubwa ambapo kwa sasa Wananchi wana hamu ya kujua Matokeo ya Sensa hiyo yenye faida kubwa kwa maendeleo ya Tanzania.

Mwenyekiti Mwenza huyo ambaye Pia ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar ameeleza kuwa zoezi la Uzinduzi wa Matokeo hayo litafanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan katika Kiwanja cha Jamhuri Jijini Dodoma ambapo amewataka Wananchi kushiriki kikamilifu katika Uzinduzi huo.

Aidha Mhe. Hemed amewapongeza Wananchi kwa Ujumla kwa ushirikiano wao waliouonesha katika kipindi chote cha Zoezi hilo na kueleza kuwa Serikali inathamini mashirikiano yao hayo.

Sambamba na hayo Mhe. Hemed ameridhishwa na Maandalizi mazuri ya Hafla hiyo ya uzinduzi na ameipongeza Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma kwa kuwa mstari wa mbele katika Maandalizi hayo.

Nae Waziri wa Nchi Afisi ya Makamu wa Pili wa Rais Sera, Uratibu na Baraza la Wawakilishi Mhe. Hamza Hassan Juma ameeleza kuwa Maandalizi ya Hafla ya uzinduzi huo yamekamilika kwa Asilimia kubwa ambapo Serikali itakuwa karibu na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma ili kukamilisha Maandalizi hayo.

Aidha Mhe. Hamza ameeleza kuwa Serikali imezingatia Ushiriki wa Wananchi wa Pande zote mbili za Muungano Bara na Visiwani ambapo Wananchi mbali mbali wanatarajiwa kushuhudia Uzinduzi huo.

Afisi ya makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

29/10/2022

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.