Habari za Punde

Hotuba ya Makamu wa Rais Mhe.Philip Mpango Wakati wa Kukabidhi Tuzo

 

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango akihutubia Viongozi na wamiliki wa viwanda mbalimbali hapa nchini wakati wa Hafla ya utoaji wa Tuzo za 16 za Rais za wazalishaji bora wa viwandani katika Ukumbi wa Serena Jijini Dar es salaam leo tarehe 18 Novemba 2022.

Kwanza napenda kutoa shukrani kwa Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara na Shirikisho la Viwanda Tanzania (CTI) kwa kumualika Mheshimiwa Rais kuwa Mgeni Rasmi katika Hafla hii muhimu ya utoaji Tuzo za Rais kwa wazalishaji bora wa Viwandani kwa mwaka 2021. Mheshimiwa Rais alipenda sana kujumuika nanyi leo, lakini ameshidwa kutokana na majukumu mengine ya kitaifa aliyonayo na hivyo amenipa heshima ya kumwakilisha.

Mheshimiwa Rais anaupongeza Uongozi wa CTI kwa kuandaa Hafla hii na kuendeleza utoaji wa Tuzo kwa Viwanda Vilivyofanya Vizuri kila mwaka.  Malengo ya mashindano ya Tuzo za Rais kwa wazalishaji bora viwandani ni mazuri sana. Baadhi ya malengo hayo ni: kutambua mchango wa wenye viwanda katika ukuaji wa uchumi; kuwahamasisha wenye viwanda waendelee kuzalisha bidhaa bora zitakazoshindana katika masoko ya kimataifa; kuhamasisha ubunifu viwandani katika matumizi ya teknolojia; na kuongeza uuzaji wa bidhaa nje ya nchi na hivyo kuongeza mapato ya nchi katika fedha za kigeni.  Kwa sababu hiyo, Mheshimiwa Rais ametoa pongezi za dhati kwa washindi wote na amenituma niwaeleze kwamba Serikali inatambua mchango wenu mkubwa katika ukuaji wa uchumi wa Taifa na kuboresha ustawi wa maisha ya watanzania. Aidha, kwa niaba yake, napenda kuwahakikishia wenye viwanda na wadau wote wa sekta hii muhimu kwamba, Serikali ya Awamu ya Sita itaendelea kushirikiana nanyi, kuwaunga mkono, kutunga sheria na sera rafiki kwa uwekezaji katika viwanda na sekta zote mwambata wa ukuaji wa sekta hii.

Ndugu Mwenyekiti, Washiriki na Wageni Waalikwa;

Duniani kote sekta ya viwanda ndiyo chimbuko la maendeleo ya haraka ya nchi. Sekta ya Viwanda imekuwa mhimili mkuu katika kuongeza thamani ya malighafi, kutoa ajira kwa wananchi, kuongeza mapato ya serikali pamoja na fedha za kigeni, kuongeza na kuboresha sayansi na teknolojia, kuongeza uzalishaji na hivyo kukuza uchumi na kuondoa umasikini. Kwa kutambua umuhimu huo, Mpango wetu wa Tatu wa Maendeleo wa Miaka Mitano, umejikita katika kujenga uchumi shindani wa viwanda kwa maendeleo ya watu.  Msingi mmojawapo wa mwelekeo huu ni ukweli kuwa watanzania walio wengi wanajishughulisha na kilimo na wanaitegemea sekta ya viwanda kuongeza thamani ya mazao yao na hivyo kukuza kipato chao.

Ndugu Washiriki na Wageni Waalikwa;

Kwa ujumla, sekta ya viwanda imeendelea kuwa imara licha ya misukosuko inayoendelea duniani. Mchango wake katika Pato la Taifa ulikuwa asilimia 8.5, 8.3 na 7.8 kwa mwaka 2019, 2020 na 2021, mtawalia. Katika kipindi kama hicho, ukuaji wake ulikuwa asilimia 5.8, 4.5 na 4.8. Hali hiyo ya kushuka kwa mchango na ukuaji wa Sekta ya Viwanda imetokana na athari za UVIKO-19. Kwa upande wa mauzo ya nje, sekta ya viwanda imeendelea kuwa chanzo muhimu cha fedha za kigeni ambapo ziliongezeka kutoka dola za Marekani bilioni 0.85 mwaka 2019, 0.9 mwaka 2020 hadi 1.2 mwaka 2021. Kwa mwaka unaoishia Septemba 2022, mauzo ya bidhaa za viwanda nje ya nchi yaliongezeka kwa takribani asilimia 77.0 kufikia dola za Marekani bilioni 1.5 ukilinganisha na dola za Marekani bilioni 0.85, kipindi kama hicho mwaka 2020. Hatua hii, imeongeza mchango wa sekta ya viwanda katika mauzo yote nje ya nchi kufikia asilimia 13 hivi sasa ukilinganisha na chini ya asilimia 10 mwaka 2020.

Katika eneo la viwanda vya sukari, uzalishaji wa ndani wa sukari ya kawaida umeongezeka kwa takriban asilimia 33 kufikia tani 420,000 mwaka 2021 kutoka tani 316,000 mwaka 2018 na hivyo kuipunguzia Serikali mzigo wa kuingiza bidhaa hiyo nje ya nchi kuziba upungufu kutoka wastani wa tani 100,000 kwa mwaka hadi tani 50,000 kwa mwaka. Nafahamu mmejipanga tuwe tunazalisha tani 756,0000 ifikapo 2025 na hivyo kuondoa kabisa pengo la sukari hapa nchini na kuwa na ziada. Ziada hiyo itatumika kama malighafi ya kuzalisha sukari za viwandani (industrial sugar) kwani bado Serikali inatumia takribani dola za Marekani milioni 140 kwa mwaka kuagiza bidhaa hiyo kutoka nje.

Aidha, uwezo wa ndani wa kuziongezea thamani korosho ghafi pamoja na uzalishaji wa bidhaa nyingine zitokanazo na zao hilo muhimu la kibiashara nao umeimarika. Nimeelezwa kuwa takribani tani 70,000 za korosho (zaidi ya theluthi moja ya korosho zinazozalishwa kwa mwaka) zimebanguliwa hapa hapa nchini kwa mwaka 2022, sawa na ongezeko la zaidi ya asilimia 100 ukilinganisha na tani 34,000 mwaka 2021. Pia kumekuwa na ongezeko la uzalishaji wa mafuta ya maganda ya korosho (Cashewnut Shell Liquid), ambapo katika msimu uliopita lita 55,000 ziliuzwa nje ya nchi. Hii ni hatua kubwa ya kujivunia. Hakikisheni jitihada hizo zinakuwa endelevu na sasa mjiwekee lengo la kubangua korosho ghafi zote kwa asilimia 100.

Napenda niwapongeze pia kwa ubunifu wenu wa kuanza kuzalisha nishati mbadala kwa kutumia malighafi za ndani. Mwezi Agosti 2022 nilizindua nishati ya mkaa utokanao na mabaki ya mkaa wa mawe (Rafiki Briquettes) unaotengenezwa na STAMICO. Sasa tunataka kuona bidhaa hizo muhimu zinazalishwa kwa wingi na kwa gharama nafuu ili kuhamasisha wananchi wetu wazitumie na wakati huo huo kusaidia kutunza mazingira na misitu yetu inayokatwa kwa ajili ya mkaa na kuni.

Ndugu Washiriki na Wageni Waalikwa;

Pamoja na mafanikio hayo, ninaendelea kusisitiza umuhimu wa viwanda vyetu kuongeza thamani ya bidhaa zetu ghafi. Bado nchi yetu imeendelea kuuza nje ya nchi bidhaa nyingi za mazao ya kilimo na maliasili zikiwa ghafi, na hivyo kusababisha nchi kupata mapato kidogo ya fedha za kigeni na kuhamisha ajira za vijana wetu. Nilipokutana nanyi mwaka jana, nilieleza kutofurahishwa na ongezeko la uagizaji wa bidhaa ambazo zinaweza kuzalishwa humu nchini. Changamoto hii bado ni kubwa: kwa mfano, takribani asilimia 12 ya fedha za mauzo nje ya nchi (export earnings) zinatumika kulipia uagizaji wa bidhaa za walaji (consumer goods) ambazo nyingi tunaweza kuzalisha wenyewe hapa nchini; na kwa mwaka unaoishia Septemba 2022, tumetumia takribani dola za Marekani milioni 346 kuagiza mbolea.  Naomba nitumie fursa hii kuhimiza wenye viwanda wote hapa nchini mfanye jitihada na kuongeza uwezo wa uzalishaji katika viwanda vyenu ili kukidhi mahitaji ya ndani na hivyo kupunguza upotevu huu wa rasilimali hii ya fedha za kigeni.

Ndugu Washiriki, Wageni Waalikwa, Mabibi na Mabwana;

Serikali ya Awamu ya Sita imeendelea kuboresha mazingira ya kufanya biashara na uwekezaji hapa nchini. Mathalani, Serikali imefanya maboresho zaidi ya kitaasisi, sheria, sera za fedha na bajeti. Hadi sasa, zaidi ya kodi na tozo 230 zisizo na tija zimefutwa; na takribani sheria na miongozo 40 imeboreshwa na majukumu ya baadhi ya taasisi yameendelea kuboreshwa ili kuongeza ufanisi; na huduma za uwezeshaji wa biashara na uwekezaji zimesogezwa karibu na wadau katika Serikali za Mitaa ili kupunguza usumbufu usio wa lazima.

Vilevile, Serikali imeendelea kuongeza na kuimarisha miundombinu ikiwamo ya usafirishaji ili kuhakikisha maeneo yote ya nchi yanafikika kwa urahisi. Hali kadhalika, tumeendelea na ujenzi wa miradi ya umeme, ili kuwa na nishati ya uhakika, huku ujenzi wa reli ya kisasa (SGR) unaendelea kwa kasi kubwa, ili iweze kuongeza ufanisi katika usafirishaji wa mizigo kutoka sehemu moja hadi nyingine. Sambamba na hili, tunadhamiria pia kuiunganisha reli yetu na nchi jirani kama Burundi na DRC ili kuchochea biashara ya kikanda na kuwezesha Taifa kunufaika na huduma (logistics) na usafirishaji wa madini na bidhaa mbalimbali kutoka katika nchi hizo.

Aidha, tunaendelea na jitihada za upanuzi na kuongeza ufanisi wa Bandari zetu kuu za Dar es salaam, Mtwara na Tanga pia Bandari katika Maziwa Makuu na kuimarisha mfumo wa forodha kwa ajili ya upitishaji na utoaji wa mizigo kwa haraka.   Serikali pia inaendelea na ujenzi wa bandari kavu nchini ikiwa ni pamoja na bandari kavu ya Kwala, Mkoa wa Pwani ili kupunguza msongamano wa makasha (containers) na magari kutoka bandari ya Dar es Salaam.

Ndugu Washiriki, Wageni Waalikwa, Mabibi na Mabwana;

Sambamba na jitihada hizo za ndani, Mheshimiwa Rais ameendelea kukuza uhusiano wa kimataifa. Kwa mfano, Mheshimiwa Rais aliridhia kusainiwa kwa Mikataba ya Kutotoza Kodi Mara Mbili (Double Taxation Avoidance Agreement) na nchi kumi (10) ili kuvutia na kuimarisha biashara na uwekezaji. Vilevile, Mheshimiwa Rais amekuwa mstari wa mbele kutangaza vivutio vya utalii hapa nchini kupitia Filamu ya Royal Tour na kufanya mazungumzo na Viongozi wa wafanyabiashara na wawekezaji (Business Leaders) katika nchi mbalimbali za kimkakati alizotembelea ndani na nje ya Bara la Afrika.

Hatua hizi zote zimeleta matokeo chanya na kuendelea kuvutia idadi kubwa ya wawekezaji wa ndani na nje ya nchi. Kwa mfano, mwaka 2021 miradi iliyosajiriwa na Kituo cha Uwekezaji (TIC) ilikuwa 256 (ikiwa na thamani ya dola za Marekani bilioni 3.7) kutoka 208 mwaka 2020 (yenye thamani ya dola za Marekani bilioni 1.1). Kwa kipindi cha Julai 2021 – Machi 2022, Serikali imeweza kuvutia jumla ya wawekezaji wakubwa 206. Kati yao, waliowekeza katika viwanda ni 99, sawa na asilimia 49. Idadi ya watalii ambao ni watumiaji wakubwa wa bidhaa zetu za viwanda, pia iliongezeka kwa takribani asilimia 49 hadi kufikia watalii 922,692 mwaka 2021 ukilinganisha na idadi ya watalii 620,867 iliyofikiwa mwaka 2020.

Ndugu Mwenyekiti na Washiriki;

Mmeeleza changamoto mbalimbali zinazoikabili sekta ya viwanda nchini. Naomba niseme tu kwamba nimezipokea kwa niaba ya Serikali.  Hata hivyo, ni vyema pia nieleze kwa ufupi hatua zilizochukuliwa na Serikali hadi sasa.

Mmesema juu ya changamoto ya tozo kubwa ya Stempu za kielektroniki (Electronic Tax Stamps) kwenye bidhaa zinatozwa ushuru wa bidhaa (excisable goods). Kupitia hadhara hii napenda niwahakikishie tu kwamba jambo hili linafanyiwa kazi na Taasisi husika Serikalini kwa kushirikisha wadau na bila shaka suluhu itapatikana hivi karibuni. Lengo ni kuhakikisha huduma hiyo inatolewa kwa gharama ndogo zaidi.

Kuhusu malimbikizo mbalimbali, Serikali imeboresha Mkakati wa Kusimamia Madeni ya Wazabuni na inaendelea kulipa malimbikizo ya madai ya waliotoa huduma Serikalini. Katika kipindi cha Julai – Oktoba 2022 pekee, zaidi ya shilingi bilioni 420 zimeshalipwa. Pia, katika kipindi hicho, Serikali  imepunguza kwa asilimia 74 (au shilingi bilioni 9.5) ya madeni ya ushuru wa forodha wa ziada (15% additional import duty) kwa waingizaji wa sukari ya viwandani; na asilimia 32 (au shilingi bilioni 180.2) ya deni la Ongezeko la Thamani (VAT refunds). Aidha, ili kuharakisha malipo ya fidia za VAT, Serikali imeendelea kuimarisha mfumo wa uhakiki wa madai kimtandao (Electronic Fiscal Management Systems).

Kuhusu kero ya TASAC, katika kipindi cha mwaka huu wa fedha 2022/2023, Serikali imeondoa jukumu la uondoshaji mizigo bandarini iliyokuwa inafanywa na TASAC isipokuwa kwa bidhaa hatarishi. Lengo la hatua hii ni kuvipunguzia viwanda vyetu gharama za uzalishaji ili kuviongezea uwezo wa ushindani kwenye masoko ya ndani na nje ya nchi yetu. Kama bado mnayo malalamiko, msisite kuyawasilisha Serikalini kupitia kwa Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara.

Kuhusu kupanda kwa gharama za mafuta, hii ni changamoto ya kidunia hasa kwa nchi kama Tanzania ambazo hatuzalishi mafuta.  Hata hivyo, Serikali imejitahidi kupunguza makali ya athari ya kupanda kwa bei ya mafuta duniani kwa njia mbalimbali ikiwamo kutoa ruzuku ya takribani shilingi bilioni 459 ili kudhibiti kupanda kwa gharama za uendeshaji katika sekta mbalimbali.

Kuhusu ukwasi, Sera ya fedha, imeendelea kuwa wezeshi: Katika kipindi cha Julai-Septemba 2022, ukuaji wa mikopo kwa sekta ya viwanda ulikuwa ni zaidi ya wastani wa  asilimia 30 ukilinganisha na ukuaji wa chini ya asilimia 5 kwa kipindi kama hicho 2021.

Ndugu Viongozi, Washiriki na Wageni Waalikwa;

Serikali inapoendelea kuchukua hatua mbalimbali kuboresha mazingira ya kufanya biashara na kuondoa changamoto zinazoathiri ukuaji wa sekta ya viwanda, wadau wote wa viwanda hatuna budi kutumia kikamilifu fursa hizo. Hivyo, napenda kusisitiza na kuelekeza mambo yafuatayo:

Jambo la Kwanza, Mchango wa sekta ya viwanda katika mauzo nje ya nchi wa asilimia 13, bado ni wa chini mno ukilinganisha na fursa zilizopo. Mmenieleza hapa kwamba mmeanza utafiti wa kina ili kubaini changamoto zinazowakwamisha. Lakini ahadi yenu ya kunikabidhi matokeo ya utafiti huo na mapendekezo  Mwezi Aprili 2023 naona ni mbali mno ukizingatia nililitoa agizo hili mwaka jana. Mheshimiwa Waziri, nataka kazi iharakishwe na taarifa iwasilishwe Serikalini mapema zaidi lakini bila kuathiri ubora wake.

Jambo la Pili, Tumeridhia kujiunga na Eneo Huru la Biashara la Afrika (AfCFTA) lenye watu takribani bilioni 1.4. Lakini Mkakati kuhusu namna Tanzania itakavyoshiriki na kunufaika na soko hilo katika mchanganuo mpana wa kisekta, bado uko katika hatua ya maandalizi. Naiagiza Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara kukamilisha Mkakati huo haraka kwa kushirikiana na wadau wote. Vilevile, Wizara iandae kanzidata ya wote wanaoshiriki katika soko hilo, yaani wafanyabiashara, wenye viwanda n.k.

Na Jambo la Mwisho, Napenda niwakumbushe CTI kwa kushirikiana na Ofisi ya Makamu wa Rais  - Mazingira; Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara; na Ofisi zetu za Ubalozi, kupitia Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kuchangamkia fursa na rasilimali za kimataifa  katika kulinda mazingira (mfano: Green Climate Fund)  kuibua miradi ya utunzaji wa mazingira kama vile utengenezaji wa nishati mbadala, viwanda vya kuchakata taka ngumu (waste management) na miradi mingine ya aina hiyo. Ni lazima tujipange na kuchangamkia fursa kama hizi.

Ndugu Mwenyekiti;

Napenda kuhitimisha kwa kuwapongeza washiriki wote wa shindano la mwaka 2021, hususan wale ambao wameshinda tuzo mbalimbali. Kwa washiriki ambao hawajafanikiwa, nawasihi msikate tamaa. Badala yake muongeze jitihada ili mfanye vizuri zaidi mwakani. Aidha, napenda pia kuyashukuru makampuni na taasisi zote hususan Benki ya NBC, ambaye ni Mdhamini Mkuu kwa kudhamini na kuchangia gharama mbalimbali. Mchango wenu ni muhimu katika kukuza sekta ya viwanda na kuongeza ushindani katika soko la ndani na nje ya Tanzania.

Ninafahamu kuwa mnayo shauku kubwa kutaka kufahamu washindi wa Tuzo za Rais ya Wazalishaji Bora wa Viwandani kwa Mwaka 2021. Hivyo, naomba nihitimishe hotuba yangu na kutoa fursa kwa zoezi la utoaji na upokeaji Tuzo za Rais.


Viwanda Juu!

CTI Oyee!

Mungu Ibariki, Afrika.

Mungu Ibariki, Tanzania,

Asanteni sana kwa kunisikiliza.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.