Habari za Punde

Mhe Hemed ajumuika na Waumini katika Sala ya Ijumaa Masjid Al-noor Unguja Ukuu

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Alhajj Hemed Suleiman Abdulla akiwasalimia waumini wa Masjid AL-NOOR  uliopo UNGUJA UKUU KAE PWANI Mkoa wa Kusini Unguja baada ya swala ya IJUMAA.


 Waumini wa Dini ya Kiislamu wametakiwa kuitumia misikiti kutatua changamoto mbali mbali zinazowakabili na kuendea kuitunza Amani iliyopo nchini kwa maslahi ya Taifa.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Alhajj Hemed Suleiman Abdulla ametoa rai  hio wakati akisalimiana na Waumini wa Masjid AL-NOOR  uliopo UNGUJA UKUU KAE PWANI Mkoa wa Kusini Unguja.

Amesema kuwa misikiti ni sehemu muhimu kwa wanakijiji kuitumia katika kutatua changamoto zinazowakabili hasa katika suala zima la utunzaji wa amani ya nchi pamoja na kujadili mambo mbali mbali yanayohusu maendeleo.

Alhaj Hemed amesema kuwepo kwa amani, mshikamano na upendo kwa wanakijiji  kunaisaidia Serikali kutekeleza kwa vitendo yale yote waliyowaahidi wananchi wake kwa malsahi ya vizazi vya sasa na vya  baadae. Hivyo, amewataka waumini  na Wazanzibari kwa ujumla kuendelea kuwasaidia watu wenye mahitaji maalum ili kukuza upendo baina yao.

Aidha, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar amewasisitiza Wananchi kuendelea kuiombea Dua nchi yetu pamoja na Viongozi Wakuu  ili waweze  kuiongoza vyema Zanzibar  kwa   Busara na Uadilifu mkubwa  na kuweza kuwatumikia wananchi wake.

Sambamba na hayo, Alhaji Hemed amewatakaka wananchi kuendeelea kumuunga mkono Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaji Dkt. Hussein Ali Mwinyi katika yale yote anayoyafanya kwa maslahi ya wazanzibari na kuwapuuza wale wote ambao hawana nia njema na nchi hii.

  

Akigusia suala la Maadili ndani ya Zanzibar, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar amesema ni wajibu wa  kila mzazi na mlezi kuhakikisha anatumia nafasi aliyokuwa nayo kwenye familia yake ili kuijenga Zanzibar yenye maadili mema na utulivu kwa wananchi wake.

Amesema ni lazima kwa wazazi na walezi kuweza kujitathmini na kujua wajibu wao kwa watoto ili kuwaandaa mapema kimaadili na kinidhamu kwa lengo la kupata wanazuoni na viongozi bora hapo baadae.

 

Kwa upande wake Sheikh NASSOR AHMADA katika Khutba ya Sala ya Ijumaa  amewataka waumini Kuendelea Kukisoma Kitabu Kitukufu cha qur- an kwani kufanya hivyo kutasaidia kwa kiasi kikubwa kuishi kwa Amani na utulivu hapa nchini.

Amesema kupitia Qur-an kutasaidia kujua ni jinsi gani jamii inatakiwa kuishi ili kuweza kupata maendeleo endelevu hapa duniani na kupata ujira ulioridhiwa na Mwenyezi Mungu kesho ahera.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.