Habari za Punde

uongozi wa msikiti wa Rahmman kuweka utaratibu maalum wa kuwawezesha walimu wa Madrasa, ili waweze kujikimu na kutekeleza vyema majukumu yao.

 

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk.Hussein Ali Mwinyi akizungumza na kuwasalimia Wananchi wa Kijichi Wilaya ya Magharibi “A” Unguja baada ya kumalizika kwa Ibada ya Sala ya Ijumaa iliyofanyika katika Masjid Rahman Kijichi leo 11-11-2022

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi  Alhaj Dk. Hussein Ali Mwinyi ameutaka uongozi wa msikiti wa Rahmman kuweka utaratibu maalum wa kuwawezesha walimu wa Madrasa, ili waweze kujikimu na  kutekeleza vyema majukumu yao.

Alhaj Dk. Mwinyi amewaeleza hayo waislamu baada ya kukamilisha  ibada ya sala ya Ijumaa, iliofanyika ‘Masjid Rahman’, uliopo  Kijichi Mkoa Mjini Magharibi Unguja.

Amesema kuna umuhimu kwa uongozi wa msikiti huo kuweka  utaratibu maalum utakaowawezesha waislamu kutoa michango yao kwa ajili ya kuwawezesha walimu wanaofundisha katika madrasa ya msikiti huo ili waweze kujikimu kimaisha na kutekeleza vyema majukumu yao ya kufundisha.

Alisema katika hali ilivyo hivi sasa katika misikiti  mingi nchini, walimu wa madrasa wameachwa bila ya msaada wowote na hivyo kushindwa kujikimu kimaisha, huku wakibeba dhima kubwa ya kufundisha watoto dini ya Mwenyezi Mungu.

“Sasa huyu mtu tunamkabidhi watoto wetu kusomesha kitabu cha Mwenyezi Mungu, ataishi vipi bila ya kumuwezesha?”, alihoji Alhaj Mwinyi.

Aidha, alisema hatua hiyo inapaswa kwenda sambamba na kuwawezesha maimamu pamoja na kusisitiza umuhimu wa kuutunza msikiti huo kwa kuufanyia matengenezo ya mara kwa mara pale vifaa ikiwemo mifereji inapoharibika.

Alhaj Mwinyi alisema pamoja na msikiti huo kutumiwa kwa ajili ya sala, lakini pia inapaswa kutumika kwa shughuli nyenginezo za eibada.

Alitumia fursa hiyo kuwashukuru wafadhili waliofanikisha ujnezi wa msikiti huo, sambamba na kutoa shukrani kwa heshima aliyopewa ya kuufungua.

Nae, Katibu Mtendaji Ofisi ya Mufti wa Zanzibar, Sheikh Khalid Ali Mfaume alimshukuru Rais Alhaj Dk. Mwinyi  kwa kuungana na waislamu na kushiriki katika ibada tofauti katika kipindi cha miaka miwili ya uongozi wake, ikiwemo ufunguzi wa misikiti katika maeneo mbali mbali Unguja na Pemba,  na hivyo akawaomba waislamu kuendelea kumuombea dua.

Mapema, Khatibu katika sala hiyo ya Ijumaa, Sheikh Omar aliwataka waislamu kufuata maamrisho ya Mwenyezi Mungu na kuonyesha uchamungu wao kwa kuepuka yale yote aliyoyakataza.

Aidha, aliwataka waislamu kuwa na mwamko katika kutafuta elimu ya dini yao, sambamba na kuwa na msimamo wa kushukuru neema za Mwenyezi Mungu, ikiwemo uwepo wa amani nchini.

Msikiti huo wa ‘Masjid Rahmman ulifunguliwa Ijumaa iliopita, ambapo Rais Alhaj Dk. Mwinyi aliwakilishwa.

Imetayarishwa na Idaya ya Mawasiliano

Ikulu Zanzibar.

 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.