Habari za Punde

Waziri Mkuu Mhe Kassim Majaliwa Akisoma Hutuba ya Kuahirisha Bunge.Tutumie kwa Uangalifu Chakula Kilichopo

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akielekea kwenye jukwaa kusoma hotuba ya kuahirisha Bunge jijini Dodoma,
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisoma hotuba ya kuahirisha Bunge jijini Dodoma
 

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema katika kukabiliana na upungufu wa chakula unaoweza kujitokeza kwa baadhi ya maeneo nchini, Serikali inawataka wananchi waendelee kutumia chakula kilichopo sasa kwa uangalifu na waepuke matumizi mabaya ya chakula au yasiyokuwa ya lazima kama vile utengenezaji wa pombe na matumizi ya chakula katika sherehe zisizo za lazima.

 

Ameyasema hayo leo (Ijumaa, Novemba 11, 2022) wakati akiahirisha Mkutano wa Tisa wa Bunge la 12 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jijini Dodoma. Amesema katika kukabiliana na hali ya ukame na kuchelewa kuanza kwa mvua za msimu 2022/2023, wakulima waendelee kutumia mbinu bora na walime mazao yenye kuhimili ukame.

Pia, Waziri Mkuu amesema wakulima waendeleze kilimo kinachohimili ukame na chenye ufanisi mkubwa ikiwemo matumizi ya mbolea za mboji, samadi, kilimo cha matandazo ambacho huimarisha uhifadhi wa maji na unyevunyevu kwenye udongo; kupanda mbegu za mazao ya chakula yanayokomaa kwa muda mfupi na kutumia maji vizuri kwenye skimu za umwagiliaji.

“Maafisa ugani endeleeni kushirikiana na vituo vya utafiti vilivyopo kwenye maeneo yenu kwa lengo la kupata na kusambaza teknolojia za uzalishaji wa mazao, kufuatilia kwa karibu taarifa za mara kwa mara kutoka Mamlaka ya Hali ya Hewa nchini ili kuwa na wigo mpana wa kuwashauri wakulima kuhusiana na hali ya hewa na kilimo kwa wakati.”

Akizungumzia kuhusu hali ya upatikanaji wa chakula, Waziri Mkuu amesema mwezi Juni hadi Julai 2022, Serikali ilifanya tathmini ya awali ambayo ilionesha kuwa, uzalishaji wa mazao ya chakula unatarajiwa kufikia kiasi cha tani 17,403,880. Mahitaji yote ya chakula kwa mwaka 2022/2023 ni kiasi cha tani 15,073,855. Kwa kulinganisha uzalishaji na mahitaji, nchi inatarajiwa kuwa na kiwango cha utoshelevu wa kiasi cha asilimia 115.

Kadhalika, Mheshimiwa Majaliwa amesema mwezi Oktoba, 2022 Serikali kupitia Wizara ya Kilimo ilifanya Tathmini ya Kina ya Hali ya Upatikanaji wa chakula kwa ngazi ya kaya katika maeneo ambayo yalibainika kuwa na upungufu wa uzalishaji wa mazao ya chakula kwa msimu 2021/2022.

Mheshimiwa Majaliwa amesema kutokana na matokeo ya tathmni hiyo, Serikali kupitia Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) imetenga jumla ya tani 4,572,300 za chakula kwa ajili ya kupelekwa kwenye maeneo yenye changamoto ya upatikanaji wa chakula.

Amesema hadi kufikia mwezi Oktoba, 2022 jumla ya Halmashauri 20 zimepelekewa chakula kama ifuatavyo: Liwale (tani 200), Nachingwea (tani 100), Bunda (tani 400), Geita TC (tani 100), Nzega (tani 300), Sengerema (tani 300), Monduli (tani 100).

Halmashauri nyingine ni Ngorongoro (tani 100), Butiama (tani 100), Meatu (tani 100) Kishapu (tani100), Longido (tani 1,872), Urambo (tani100), Handeni (tani 100), Mkinga (tani 100), Chemba (tani (100), Chamwino (tani 100), Mbulu (tani 100), Mwanga (tani 100) na Hai (tani 100). 

Mheshimiwa Majaliwa amesema pamoja na hatua hizo, Serikali inaendelea kufanya ufuatiliaji wa karibu wa hali ya upatikanaji wa chakula hususan mazao ya nafaka na kuchukua hatua mbalimbali ikiwemo kupeleka chakula kutoka Hifadhi ya Taifa ya Chakula (NFRA) kitakachouzwa kwa bei ya chini ya bei ya soko.

Hata hivyo, Waziri Mkuu amesema hadi kufikia Novemba, 2022 unyeshaji wa mvua katika maeneo mengi yanayopata mvua hizo hasa mikoa ya Pwani, Dar es Salaam, Tanga, Morogoro, Arusha, Kilimanjaro na Manyara ni wa kusuasua. Kwa upande wa mikoa ya Kagera, Geita, Mara na Mwanza, mvua za vuli zinaendelea kunyesha na mazao ya chakula shambani yapo katika hatua mbalimbali za ukuaji.

(mwisho)

IMETOLEWA NA:

OFISI YA WAZIRI MKUU,

IJUMAA, NOVEMBA 11, 2022.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.