Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania, Zanzibar
(TAMWA-ZNZ) kimeishauri Serikali kuongeza juhudi katika kusimamia matukio ya
udhalilishaji wa kijinsia (GBV) ili haki iweze kutendeka na kwa wakati muafaka.
Pamoja na kupigwa vita kwa vitendo vya GBV na vya watoto
(VAC) bado vitendo hivyo vinaendelea na kiwango cha upatikanaji wa haki bado ni
mdogo.
Afisi ya Mtakwimu
Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar hivi karibuni imetoa taarifa ya mwaka
2022 ambapo imetaja kuripotiwa kwa matukio 1360 katika vituo vya polisi.
Taarifa hiyo inaeleza kuwa ni matukio 181 tu sawa na
asilimia 13 ndiyo yaliyotiwa hatiani, wakati makosa mengi bado yapo katika
hatua za polisi na mahakama na matukio mengine watuhumiwa wameachwa huru na
mengine hakuna hatua iliyochukuliwa wakati mengine watuhumiwa hawakupatikana.
Hivyo, kuna umuhimu mkubwa wa kuzidisha nguvu katika
kusimamia matukio haya katika hatua zote ili hali ya utafutaji wa haki kwa
waaathirika iweze kuleta maana zaidi.
Tunashauri taasisi husika pamoja na wananchi kutokufuta kesi
kwa sababu zozote zile kwani kesi GBV na VAC ni kesi dhidi ya nchi na siyo
dhidi ya mtu ama familia. Ili kurahisisha upatikanaji wa hukumu, Serikali
inahitaji kuimarisha mifumo ya mkono kwa mkono ili kesi isikilizwe sehemu moja
na kupatikana kwa hukumu ambapo sheria namba 9 ya ushahidi ya mwaka 2016 katika
kifungu cha 66 kimetoa nafasi ya kusikiliza kesi kwa njia ya kielectroniki.
Kama taarifa ilivyoeleza watoto wengi ndio walioathirika
hivyo, sambamba na kupatikana kwa haki ni vyema waathirika kupatiwa kiwango cha
kutosha cha msaada wa kisaikolojia ili ule msemo wa kutokuachwa nyuma mtu
yeyote uweze kufikiwa Zanzibar.
TAMWA, ZNZ inapenda kuzipongeza taasisi husika hata hivyo
kwa maendeleo haya hasa Afisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali kwa kutoa taarifa
hizi ambazo zitakuwa ni chachu ya kuchukua hatua nyengine
Dkt Mzuri Issa Mkurugenzi TAMWA-ZNZ
No comments:
Post a Comment