Habari za Punde

Mhe Hemed ajumuika na waumini wa Msikiti wa Bweleo katika Ibada ya Sala ya Ijumaa



 Waumini wa Dini ya Kiislamu wametakiwa kutenga muda kwa ajili ya Kusoma Dini ili kujenga jamii iliyo njema.

 

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Alhajj Hemed Suleiman Abdulla ametoa kauli hiyo alipojumuika na Waumini wa Msikiti wa Bweleo Wilaya ya Magharibi B katika Ibada ya Sala ya Ijumaa. 

 

Amesema kuwepo kwa matendo maovu katika Jamii kunatokana na kukosa elimu ya Dini na Malezi ambapo jukumu la wazazi kuhimizana kuisoma Dini hatua ambayo jamii itafahamu mambo mema kuyafata na maovu kuyawacha.

 

Amesema Elimu ni jambo la muhimu ambapo ni vyema kwa waumini kutumia Misikiti kwa kuendeleza masuala ya Dini pamoja na kujadiliana masuala mbali mbali ya kijamii.

 

Aidha ameeleza kuwa Jamii inaposhikamana na Dini inakuwa na nafasi ya kumuabudu Mungu ipasavyo jambo ambalo litasaidia kupata kizazi inayomtambua Mungu na kusimamia maadili mema.

 

Mhe. Hemed amewasisitiza Waumini hao kuwa na umoja na mshikamano kwa kusaidiana katika masuala mbali mbali ili kuiweka jamii pamoja na yenye upendo.

 

Akitoa Khutba ya Sala ya Ijumaa Maalim Mussa Ali Kirobo amewataka Waumini hao kusimamia maadili mema hasa kukemea matendo maovu yaliyokithiri na kuwataka kurudi katika mafundisho ya Dini ili kupata kizazi kilicho chema.

 

Amesema Zanzibar kwa miaka ya nyuma ilisifika kwa kuwepo wasomi waliobobea katika Dini ambao walikuwa tegemezi kwa nchi za Afrika Mashariki na Falme za Kiarabu.

 

………………….

Abdulrahim Khamis

Afisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.