Habari za Punde

SMZ Kuifanyia Mageuzi Makubwa Sekta ya Michezo kwa Kujenga Viwanja vya Kisasa - Dk.Mwinyi

 

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akihutubia katika viwanja vya Matumbaku Miembeni Wilaya ya Mjini Unguja, baada ya kuweka Jiwe la Msingi la Ujenzi wa Viwanja vya Michezo, vinavyojengwa na Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar (ZSSF) ikiwa ni shamrashamra za Maadhimisho ya Miaka 59 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar

SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar imesema imekusudia kuifanyia mageuzi makubwa sekta ya michezo visiwani kwa kujenga viwanja vya kisasa vinavyoendena na hadhi ya miaka 59 ya Mapinduzi.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi ameyasema hayo alipoweka jiwe la msingi la viwanja vya michezo, Matumbaku, wilaya ya Mjini, Mkoa wa Mjini Magharibi, Unguja unaosimamiwa na Mfuko wa Hifadhi ya Jamii, (ZSSF).

Dk. Mwinyi aliiagiza bodi ya Mfuko wa ZSSF kuharakisha ujenzi ili ukamilike kwa wakati na wananchi wapate huduma wanazostahiki

Aidha, aliiamuru bodi hiyo kuikopesha fedha serikali ili wakamilishe kwa wakati maeneo yote ya ujenzi wa viwanja hivyo vikiwemo viwanja vya mpira wa mikono, (basketball netball, handball na volball) ambavyo vilikua nje ya bajeti na kuahidi fedha zote watakazotumia serikali itawarejeshea.

Akizungumzia fedha za serikali za ahuweni ya uviko 19, Dk. Mwinyi alieleza, fedha zote serikali imezielekeza kwenye miradi mikubwa ya jamii ikiwemo Elimu, Afya, Maji safi na salama, umeme na kuwawezesha wananchi kiuchumi, hivyo mradi wa viwanja vya michezo Matumbaku unatekelezwa kwa pesa za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na sio fedha za uviko 19.

Alisema Serikali imelitumia eneo la Matumbaku kuweka ujenzi huo baada ya eneo la zamani la Malindi kupisha ujenzi wa maegesho ya magari na kutuo cha kisasa na mabasi, Aidha Dk. Mwinyi alieleza, kuna mradi mwngine unaojenga barabara za lami na kazi zake zimeanza rasmi kwenye maeneo mbalimbali ya mji.

Makamo wa Pili wa Rais, Hemed Suleiman Abdulla wakati akizungumza kwenye hafla hiyo, aliwataka viongozi na wananchi wa Zanziabr kwa pamoja kuzungumza lugha moja ya maendeleo, hivyo aliwaomba watendaji na wasimamizi wa mitadi yote ya maendeleo waikamilishe kwa wakati ili wananchi waendeelee kufurahia matunda ya Mapinduzi.

Aidha, alieleza miradi yote iliyozinduliwa na kuwekewa mawe ya msingi ni ya mda mfupi pia ni jitihada zinazofanywa na serikali ya awamu ya nane ya Dk. Hussein Mwinyi na kuongeza kuwa mafanikio ya miradi hiyo ni utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi 2020 /2025.

Naye, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango, Dk. Saada Salum Mkuya, alisema ujenzi wa viwanja hivyo umegharimu shilingi bilioni 1.1 nakuongeza kuwa serikali imefanikiwa kuokoa shilingi bilioni 1.4 kwa kutumia wakandarasi wa ndani ambao ni Jeshi la Kujenga Uchini nchini, JKU kwa kuhakikisha ujenzi wa kiwango cha juu kabisa.

Katika hatua nyengine, Waziri wa Habari Utalii Vijana na Michezo, Tabia Maulid Mwita alieleza ujenzi wa viwanja hivyo ni hatua ya kupigiwa mfano kwani fedha zake hazikutokana na ufadhili wowote bali ni fedha za Serikali kutoka ZSSF.

Akizungumza kwenye sherehe hizo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Dk.Juma Malik Akili alisema ujenzi wa viwanja hivyo ni upishwaji wa miradi mitatu mikubwa ya maendeleo kwenye viwanja vya zamani vya michezo, Malindi ukiwemo ujenzi wa kituo cha mabasi cha kisasa, ujenzi wa maegesho ya magari na ujenzi kituo cha mabasi Kijangwani, hivyo alieleza ujenzi wa kisasa wa viwanja vya michezo, Matumbaku ni uimarishwaji wa sekta ya michezo nchini na  kuwaondoshea wananchi usumbufu kutokana na kuhamishiwa viwanja vyao vya awali.

Alisema tayari Serikali imewapatia ZSSF eneo la Malindi kwajili ya uwekezaji huo pamoja nakusubiri taratibu za mwongozo wa michoro kutoka Mamlaka ya mji Mkongwe ili wakamilishe mradi huo.

Mradi mpya wa viwanja vya kisasa, Matumbaku ulianza  Julai mwaka jana baada ya kuingia makubaliano na ZSSF na ulitarajiwa kukamilika Oktoba mwaka jana lakini ulichelewa baada ya baadhi ya vifaa vilivyoagiziwa kutoka nje ya nchi kutofika kwa wakati.

KITENGO CHA MAWASILIANO,

IKULU

 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.