Habari za Punde

Taasisi zinazoendelea na ujenzi wa Ofisi zatakiwa kukamilisha majengo yao kwa wakati Jijini Dodoma

 

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera Bunge na Uratibu Mhe. George Simbachawene akitoa vyeti wakati wa hafla ya kukabidhi vibali vya ujenzi wa Ofisi za Taasisi Dodoma Ukumbi wa Hazina – Dodoma.

Serikali imeziagiza Taasisi zote zinazoendelea na ujenzi wa majengo ya Ofisi zao Jijini Dodoma kuhakikisha ujenzi huo unakamilika kwa kuzingatia taratibu zote za ujenzi ikiwemo ubora, muda, bajeti iliyotengwa na thamani ya fedha ili kuleta tija inayotarajiwa.

Maagizo hayo yametolewa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera Bunge na Uratibu Mhe. George simbachawene wakati wa hafla ya kukabidhi Vibali vya Ujenzi wa Ofisi za Taasisi za Serikali Dodoma iliyofanyika katika Ukumbi wa Hazina mapema.

 

Waziri Simbachawene amesema, kila Taasisi ya Serikali ihakikishe inajenga majengo ya Ofisi zake ili kuendelea kuunga mkono jitihada za Serikali za kuhamishia Makao makuu yake Dodoma na kuifanya Dodoma kuwa eneo lenye ufanisi.

 

“Taasisi zote zilizoelekezwa kuhamia Dodoma kwa mujibu wa ratiba niliyoitoa leo zihakikishe zinatekeleza maagizo hayo na Makatibu Wakuu wa Wizara husika wahakikishe wanasimamia mpango kazi wa utekelezaji wake,”alisema Mhe.Simbachawene

 

Aliongezea kuwa, Mpango huu ni utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi ya CCM ya Mwaka 2015 kama ilivyoainishwa katika Ibara ya 151 chini ya kifungu (a), (b) na (c) vinavyoielekeza Serikali kutunga Sheria ya kuitambua Dodoma kuwa Makao Makuu ya Nchi na kuhakikisha kwamba majengo ya Wizara na Taasisi yanajengwa Dodoma badala ya Dar es Salaam.


Aidha Waziri ameagiza Ofisi ya Katibu Mkuu – Sera, Bunge na Uratibu kwa kushirikiana na Mamlaka husika kuendelea kuratibu Mpango wa Serikali na taasisi zake kuhamia Dodoma pamoja na ujenzi wa miundombinu ya kiuchumi na uboreshaji wa huduma mbalimbali za kijamii Dodoma.

Sambamba na hilo, Serikali imekamilisha ratiba na mwongozo utakaowezesha Taasisi za Serikali ambazo bado zinaendelea kutekeleza majukumu yake Dar es Salaam kuweza kuhamishia shughuli zao Jijini Dodoma kwa awamu.

“Katika utekelezaji wa suala hili, Mheshimiwa Waziri Mkuu ametoa maelekezo kwamba Taasisi 42 zihamie Dodoma ndani ya mwaka huu wa fedha wa 2022/23; Taasisi 36 zitahamia Dodoma katika mwaka ujao wa fedha wa 2023/24 na Taasisi 19 zitahamia katika mwaka 2024/25 wakati Taasisi 27 zimeelekezwa, kwa kuzingatia aina ya majukumu zilizonazo, kuendelea kutekeleza majukumu yake Mkoani Dar es Salaam.” Alieleza.

Alisisitiza kuwa, hatua hii itakamilisha sehemu kubwa ya Mpango wa Serikali wa kuhamia Dodoma ambapo hadi sasa tayari Taasisi 65 zilishahamia Dodoma tangu mwaka 2016 hadi 2022.

Waziri ameziagiza Taasisi nyingine ambazo bado hazijaanza maandalizi ya ujenzi wa Ofisi za serikali Dodoma ziwasilishe Ofisi ya Waziri Mkuu Mahitaji ya Viwanja vya ujenzi wa Ofisi za taasisi Dodoma kwa ajili ya uratibu wa pamoja.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule, ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha nyingi kwa ajili ya ujenzi wa miundo mbinu ya kuwezesha taasisi kuwepo.

“Tunaishukuru Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kazi kubwa mnayoifanya kwa kupanga makao makuu ya serikali yetu yanakuwa ni mji wa kisasa na mji uliopangwa.”alisema Mhe. Rosemary.

Awali Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Sera Bunge na Uratibu Dkt, John Jingu akitoa taarifa ya utekelezajia amesema Ofisi ya waziri Mkuu imeidhinisha vibali 55 kwa nyakati tofauti kuanzia mwaka 2018 kati ya hizo taasisi 20 zimekamilisha ujenzi, taasisi 16 zinaendelea na ujenzi na taasisi 19 zimeanza maandalizi ya ujenzi.

“Majengo haya yanajengwa katika maeneo mbalimbali, na ujenzi huu unazingatia mpango kabambe wa Jiji la Dodoma.”

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera Bunge na Uratibu Mhe. George Simbachawene akitoa vyeti wakati wa hafla ya kukabidhi vibali vya ujenzi wa Ofisi za Taasisi Dodoma Ukumbi wa Hazina – Dodoma.

Watendaji Wa Ofisi ya Waziri Mkuu Sera bunge na Uratibu na Watendaji wa Ofisi za Taasisi mbalimbali wakiwa katika hafla ya kukabidhi vibali vya ujenzi.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.