JUMLA ya matukio 504 ya
udhalilishaji yaliripotiwa Zanzibar nzima kwa kipindi cha miezi mitatu, kutoka
Novemnba 2022 hadi mwezi Januari, 2023 ambayo yalihusisha vitendo vya ubakaji,
kulawiti, vipigo kwa watoto na udhalilishaji wa kijinsia.
Miongoni mwa matukio hayo 41
pekee yaliripotiwa Mkoa wa Kaskazini Unguja kwa kipindi hicho.
Mwenyekiti wa taasisi ya
Zanzibar Maisha Bora Foundation na Mke wa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa
Baraza la Mapinduzi, Mama Mariam Mwinyi alitoa takwimu hizo alipozungumza na
watoto, wazazi, walezi, walimu na viongozi wa Mkoa wa Kaskazini Unguja
alikojumuika nao kwenye matembezi ya kupinga vita dhidi ya udhalilidhaji.
Aliposhiriki matembezi ya
kupinga vita dhidi ya udhalilishaji
Mama Mariam Mwinyi alisema
matukio hayo ni mengi na yanazidi kila uchao hivyo, alivitaka vyombo vya sheria
kutekeleza juhudi za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kutowaachia huru
watuhumiwa wa makosa ya udhalilishaji nchini.
“Tunawaomba sana Jeshi la
polisi wasiwatoe hawa watu wanaotuhumiwa kwa makosa ya udhalilishaji” Kwa hisia
alisisitiza Mama Mariam.
Mwenyekiti huyo wa Zanzibar
Maishabora Foundation, aliipongeza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa
kuanzisha mahakama maalumu ya kushughulikia mashauri ya udhalilishaji, kuonhgeza
mahakimu 10, majaji watatu ambao wameongeza idadi ya majaji kwa Majakama kuu
kufikia 12 pamoja na kuajiri makaadhi wanne wanaoshughulikia mashauri ya
familia.
Aidha, alipongeza hatua ya
Serikali kwa kuzuia dhamana kwa watuhumiwa wote wa makosa ya udhalilidhaji.
Akizungumzia masuala ya
vipigo kwa watoto, aliwasihi wazazi/walezi na walimu wa skuli na madrsa
kutowaadhibu watoto kwa kipigo chenye kupitiliza na kuwataka watumie busara ya
kuwapa adhabu zenye huruma badala ya kuwazuru kwa vipigo vikali.
“Hatupingi watoto kuchapwa
wanapokosea, sababu ni sehemu ya ulezi na makuuzi yao lakini isiwe vipigo
vyenye kupitiliza” alionya Mama Mariam Mwinyi.
Pia aliwasihi walimu na
wazazi/walezi hao kuweka tabia ya kuwasikiliza watoto/wanafunzi kwani
kunawengine hupitia ukatili mkubwa lakini kutokana na hofu kwa wanayoyapitia
kwenye jamii zao huogopa kusema
wanapokua majumbani ana skuli kwa walimu wao.
Mama Mariam Mwinyi alitumia
fursa hiyo kuwaeleza watoto kuvunja ukimya badala yake wawe jasiri kuzungumza
kwa yanayowatokezea, ikiwemo vitisho, vipigo, kunyanyaswa kwa namna yoyote iwe
na watu wazima au watoto wenzao wawe tayari kuzungumza badala ya kuweka usiri
ili jamii iwasaidie.
Pia aliwataka kuwa makini na
watu wakaribu na familia zao, wakiwemo walezi, jirani na jamii wanayoishi nayo
hata kwenye mazingira wanayosomea kwa kutotoa fursa ya mtu yeyote kushika miili
yao kwa namna yoyote.
Alisema matukio mengi ya
udhalilishaji nayoripotiwa kwenye vyombo vya sheria yanahusisha watu wa karibu
na familia na jamii ya watoto inayowazunguruka.
“Msiruhusu watu washike miili
yenu, msiruhusu kukoshwa na mtu asiekua mama yako au kuvaa nguo mbele za watu,
mujitahidi kuheshimu miili yenu, hata wakati wa kuvaa nguo jitahidi uwe peke
yako kuutunza mwili wako.” alisihi Mama Mariam.
Pia Mama Mariam alikemea
tabia ya baadhi ya wazazi/walezi kuwabusu watoto midomoni nakueleza kwamba
tabia hiyo inachochea viashiria vya udhalilishaji nakuongeza ni chanzo cha
maambukizi kwa baadhi ya maradhi.
Katika hatua nyengine Mama
Mariam Mwinyi aliipongeza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa jitihada ya
kuimarisha sekta ya elimu nchini kwa kuongeza skuli mpya nchi nzima na kukarabati za zamani hali
iliyopunguza msongamano wa wanafunzi mashuleni.
Naye, Waziri wa Maendeleo ya
Jamii, jinsia Wanawake na Watoto, Riziki Pembe Juma aliwataka wanaume kwa
nafasi na dhamana zao kuungana na jamii kuendelea kuwalinda na kuwastahi
watoto, kukemea na kuwa msatari wambele kupinga udhalilishaji wa kijinsia.
Alieleza matukio mengi ya
udhalilishaji wa kijinsia yakiwemo ubakaji, kulawiti, kutelekeza na kutorosha
wasichana wanaume ndio wahusika wakubwa wa vitendo hivyo.
Hata hivyo, aliipongeza
Taasisi ya Zanzibar Maisha Bora Foundation kwa kuungamkono juhudi za Serikali
kwa kuendelea kuwa bega kwa bega kupinga vitendo vya udhalilishaji wa kijinsia
katika harakati zake.
Akizungumza kwenye hafla hiyo
Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Unguja Ayoub Mahmoud alisema, Mkoa huo wanaendelea
kupambana na ongezeko la vitendo hivyo, kwa kuchukua hatua mbalimbali za
kupunguza na kutokomeza udhalilishaji, ikiwemo ya kuongeza uelewa kwa jamii
yakiwemo makundi ya wavuvi ambao wanalalamikiwa sana kwa kutelekeza familia
wanapokua dagoni, elimu kwa wakulima na vyombo vya ulinzi na usalama, madrasa
na mashuleni.
Alieleza mkoa pia umewafikia
watu wenye ulemavu kuwa nao karibu
kuwalinda na kuwathamini na kutoa uelewa kwa jamii juu ya kushirikiana
nao kwenye masuala mbalimbali ya maendeleo.
Alisema licha ya juhudi kubwa
zinazochukuliwa na Serikali ya mkoa huo
kupinga udhalilishaji bado suala la muhali mkoani humo ni changamoto
sugu, nakueleza kwamba wanawake na watoto wanaathiriwa zaidi na masuala ya
ubakaji, kulawiti, kutorosha, shambulio la aibu, kukashifu, mvutano wa malezi,
shabulio la kuumiza mwili, dawa za
kulenya pamoja na mashambulio ya hatari
Aidha, alieleza ndoa za umri mdogo huongeza talaka nyingi mkoani humo, hali inayochangia kushindwa kuhimili familia na watoto, pia alieleza serikali ya mkoa imejitahidi kuzibiti maundi maovu na kufanya ziara za kustukiza maeneo yenye vichocheo vya mporomoko wa maadili.
Matembezi ya kupinga vita dhidi ya udhalilidhaji yaliandaliwa na Taasisi ya Zanzibar Maisha Bora Foundation yakiwa na kaulimbiu “Mimi ni shujaa, nitaulinda mwili wangu na kuutunza” yalikwenda sambamba na maadhimisho ya mwaka mmoja tokea kuzinduliwa kwa taasisi hiyo.
No comments:
Post a Comment