Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega amekutana na wadau wa maendeleo kutoka taasisi na makampuni mbalimbali nchini Italia na kujadiliana nao fursa mbalimbali ambazo wanaweza kuzitumia kuwekeza nchini Tanzania hususan katika sekta ya mifugo na uvuvi.
Waziri Ulega amekutana na wadau hao jijini Rome wakati wa ziara yake ya kikazi nchini Italia iliyoanza Machi 30, 2023.
Wakati akiongea kwa nyakati tofauti na washirika hao wa maendeleo, Mhe. Ulega aliwaeleza kuwa, kwa sasa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan imedhamiria kubadilisha mfumo wa uzalishaji wa sekta za mifugo na uvuvi kutoka katika kufanya shughuli zao kiasili na kujiendesha kibiashara ili kuongeza uzalishaji wake.
Aliendelea kusema kuwa katika kuhakikisha sekta hizo mbili zinabadili mfumo wake wa utekelezaji kuwa wa kibiashara, Serikali inatekeleza Mpango wa Mabadiliko wa Sekta ya Mifugo wa Mwaka 2022/2023-2026/2027 na Mpango Kambambe wa Maendeleo wa Sekta ya Uvuvi wa Mwaka 2021/2022-2036/2037.
“Rais wetu, Dkt. Samia Suluhu Hassan amedhamiria kubadilisha mfumo wa uzalishaji wa sekta za mifugo na uvuvi kutoka katika kufanya shughuli zake kiasili na kujiendesha kibiashara ili kuongeza uzalishaji wake, hivyo, kukutana kwetu leo ni fursa nzuri ya kujadiliana nanyi ili muweze kuona fursa za uwekezaji katika sekta hizo mbili ambazo kufanikiwa kwake kunahitaji ushiriki wenu”, alisema Ulega
Halikadhalika, Waziri Ulega alitumia fursa hiyo pia kuwaeleza wadau hao kuwa serikali ya Tanzania ingependa kupata wawekezaji mahiri katika sekta ya mifugo hususan eneo la biashara ya nyama kwa kushirikiana na Kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO), kuwekeza kwenye mnyororo wa thamani katika sekta za mifugo na uvuvi hususan zao la dagaa kutoka ziwa Victoria.
Kwa upande wa Mkurugenzi wa Italia, anayeshughulikia nchi za Afrika, Mhe. Balozi Giuseppe Mistretta alikubali ombi la Waziri Ulega la kuiweka nchi ya Tanzania miongoni mwa nchi za kipaumbele katika masuala ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Aidha, Waziri Ulega alisema kuwa anatambua ushirikiano uliopo baina ya serikali na wawekezaji kutoka nchini Italia katika kusaidia kukuza uchumi wa Tanzania huku akiwakaribisha wawekezaji wengi zaidi kufanya uwekezaji nchini humo.
Katika ziara yake hiyo, Waziri Ulega alikutana na viongozi wa taasisi ya SACE, Benki ya Uwekezaji ya Italia (CDP), Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Maendeleo ya Viwanda (UNIDO), COGEMAT Slaughtering and Meat Technology na Mkurugenzi wa Italia, anayeshughulikia nchi za Afrika, Mhe. Balozi Giuseppe Mistretta.
No comments:
Post a Comment