Habari za Punde

Kuandaa mikutano ya mara kwa mara katika ngazi ya jamii itasaidia kutatua kero na upatikanaji wa haki kwa wakati

 

Mkurugenzi wa  PEGAO kupitia mradi wa SWIL unaofadhiliwa na Ubalozi wa Norway  Tanzania akizungumza na waandishi wa Habari Pemba. 

WAHAMASISHAJI jamii kupitia mikutano 39 walioifanya na jamii katika Wilaya nne za kisiwa cha Pemba walifanikiwa kuibua jumla ya changamoto/matatizo/kero 44 kwa mwaka 2022.

Kero hizo ziliibuliwa maoneo tofauti kisiwani Pemba katika Wilaya ya Wete kero 12, Micheweni 12, Chake Chake 9 na Mkoani 11.

Kero walizoziibua walifanikiwa kuzifikisha katika ngazi mbali mbali kwa ajili ya utatuzi, ambapo kero 17 zilifanikiwa kutafutiwa ufumbuzi, huku kati ya hizo 10 zikitatuliwa katika kipindi kifupi cha uhamasishaji jamii kujua na kudai haki zao.

Miongoni mwa kero zilizopatiwa ufumbuzi ni pamoja na kero za upatikanaji wa maji safi na salama, upatikanaji wa huduma bora za elimu kwa makundi maalum, na miundo mbinu ya barabara ambapo kero zote zinaathiri zaidi wanawake kufikia lengo lao la kushiriki katika nafasi za uongozi.

Hivyo, ili kujenga jamii yenye uwezo wa kutambua umuhimu wa kudai haki zao za msingi, PEGAO inatoa ushauri kwa jamii, masheha na uongozi wa Serikali za Mitaa kushirikiana pamoja kupitia kamati za shehia kwa lengo la kuanda mikutano ili kujadili changamoto zinazo wakabili ili kuzipatia ufumbuzi kwa wakati sahihi.

“Tunaamini kwamba kupitia ushirikishwaji wa wananchi kujadili changamoto na kero zinazo wakabili wanawake kupata haki zao za msingi ikiwemo kiuongozi itasaidia kukuza uelewa wa jamii kushiriki moja kwa moja kudai haki zao, alieleza Mwenyekiti wa wahamasishaji jamii wilaya ya Wete Mkoa wa Kaskazini Pemba”, Bi Husna Ali Said.

Mwenyekiti huyo alisema viongozi wa serikali za mitaa zitambue kwamba inao wajibu wa kuandaa mikutano ngazi ya jamii ili kukabiliana na changamoto zinazo wakabili ili kujenga jamii yenye kufuata misingi ya usawa wakijinsia kwa wote katika kila eneo na kutafuta njia bora ya kukabiliana na changamoto hizo nikupitia ushiriki wao kujadili changamoto hizo.

Kwa kutambua umuhimu wa mwanamke, Sheria na Sera mbali mbali za Zanzibar zimeeleza kuhusu haki ya wanawake kushiriki katika demokrasia na uongozi, Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984, pia hata dira ya Zanzibar ya 2050 inautambua ulazima huo wa kujenga usawa wa kijinsia  katika jamii.

Aidha Sera ya Utawala Bora ya mwaka 2011, inaeleza katika tamko lake Na 4.2 kwamba Serikali kwa mashirikiano na wadau mbalimbali itahakikisha kuwa kutakuwa na ushirikishwaji bora na ulio sawa kwa wanawake na wanaume katika vyombo vyote vya kutoa maamuzi katika ngazi zote.

Mradi wa kuwawezesha wanawake katika uongozi unatekelezwa na Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania, TAMWA ZNZ, Jumuiya ya Wanasheria Wanawake Zanzibar (ZAFELA) na Jumuiya ya Utetezi wa Mazingira na Jinsia Pemba (PEGAO) kwa kushirikiana na Ubalozi wa Norway.

Imetolewa na PEGAO kwa kushirikiana na ZAFELA na TAMWA ZNZ.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.