Habari za Punde

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Mwinyi Amekutana na Kuzungumza na Tume ya Kuangalia Jinsi ya Kuboresha Taasisi za Haki Jinai

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Hussein Ali Mwinyi akizungumza na Ujumbe wa Tume ya Kuangalia jinsi ya kuboresha Taasisi  za Haki Jinai Tanzania,ukiongozwa na Mwenyekiti wa wake Jaji Mkuu Mstaafu wa Tanzania Mhe. Mohamed Chande Othman (kulia kwa Rais) ulipofika Ikulu Jijini Zanzibar  kwa mazungumzo na kujitambulisha.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi amesema Serikali ya Mapnduzi ya Zanzibar na ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania zinasubiri kwa hamu ripoti ya Tume ya Maboresho ya mifumo ya taasisi za Haki jinai ambayo itatoa mwangaza kwa serikali zote mbili juu kuboresha mifumo na taasisi zinazohusiana na masuala hayo kwa nia ya kupatikana haki kwa ufanisi.

Dk. Mwinyi aliyasema hayo Ikulu, Zanzibar alipokutana na Tume hiyo iliyofika kujitambulisha.

Alisema kuwepo kwa tume hiyo kunaonesha dhahiri marekebisho yatakayohitajika kufanywa juu ya mfumo mzima wa haki, ikiwemo marekebisho ya kimuundo ya taasisi hizo za kisheria, hali aliyoieleza itakaleta ufanisi kwenye utekelezaji wa masuala ya haki.

Rais Mwinyi alisema ni matarajio yake baada ya kukamilika kwa kazi nzima waliyopewa tume hiyo kusikiliza, taasisi mbalimbali zikiwemo asasi binasi na za Serikali, viongozi wa kitaifa, wananchi na wadau wengine, ufanisi mkubwa utapatinaka.

Aidha, Dk. Mwinyi amesema ana matarajio makubwa ya kupatikana kwa mapendekezo mazuri kupitia ripoti ya tume hiyo ambayo itawasilishwa kwa Rais Dk. Samia Suhulu Hassan Mei 31 mwaka huu ili kuonyesha marekebisho yanayohitajika katika mfumo mzima wa kimuundo kwa taasisi zinzofanya kazi sambamba na tume hiyo kwa manufaa ya Serikali zote mbili

Alieleza, taarifa ya Tume hiyo itasaidia kurekebesha maeneo ya taasisi hizo ili kuleta tija kwa umma na taifa kwa ujumla.

“Kwa kweli mimi nafarajika sana kuona kuna kazi inafanyika kwenye maeneo hayo”. Alieleza Rais Mwinyi.

Aidha, Rais Dk. Mwinyi alitumia fursa hiyo kumpongeza na kumshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Samia Suluhu Hassan kwa uamuzi wa kuunda Tume hiyo ili kuleta tija kiutendaji kwa mifumo hiyo kwa mahitaji ya sasa na baadae.

Naye, Mwenyekiti wa Tume hiyo, Jaji Mkuu Mstaafu Mohamed Othman Chande, alisema wanatarajia kuwa na ziara ya kikazi ya siku nne kwa visiwa vya Unguja na Pemba ambako watazungumza na wadau mbalimbali nchini zikiwemo taasisi zinazoshughulikia haki jinai kama Jeshi la Polisi, Chuo cha Mafunzo, Mamlaka ya kudhibiti dawa za kulevya Zanzibar, Mamlaka ya kudhibiti na kupambana na Rushwa ZAECA, Uhamiaji, Mahakama, Mkemea Mkuu wa Serikali na taasisi nyengine.

Wadau wengine Mwenyekiti huyo aliwataja kuwa ni wananchi, asasi za kiraia na zaserikali.

Kwa Tanzania bara Mwenyekiti huyo alieleza tayari tume hiyo imekutana na wakuu wa taasisi zote za haki jinai na kutembelea mikoa 18 na wilaya 50, vituo vya polisi 46 na vituo vya magereza 19.

Pia alieleza tume ilitumia njia mbalimbali za kuwafikia wadau ikiwemo kufanya mikutano ya hadhara ambapo walifanya mikutano 25 iliyohudhuriwa na zaidi ya watu 8550, walitoa madodoso 1640 yaliyojazwa na askari wa jeshi la polisi na magereza wa ngazi za chini, kamati za ulinzi na usalama kwa ngazi za wilaya na mikoa, kamati za amani na wananchi ili kupata maoni, ushauri na mapendekezo yao. Aidha, alieleza tume hiyo pia ilitumia njia ya kupokea maoni ya wadau kwa barua kupitia posta, walitumia njia za barua pepe na mitandao ya kijamii.

Tume ya maboresho ya mifumo ya taasisi za Haki jinai imeundwa na Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan, Januari 31 mwaka huu na ilianza kazi zake mapema mwezi Februari kwa lengo la kutathmni mifumo ya haki jinai na kutathmini taasisi tano kuu za haki jinai ambazo ni Jeshi la Polisi, Ofisi ya taifa ya Mashitaka, Jeshi la Magereza, Mamlaka ya kuzuia na kupambana na Rushwa, Mamlaka ya kudhibiti na kupambana na dawa za kulevya na taasisi nyengine za kijinai zikiwemo Mahakama, Uhamiaji, Mkemea Mkuu wa Serikali na taasisi nyengine zinazohusu masuala ya jinai.

Tume hiyo inatarajiwa kukamilisha kazi zake mwishoni mwa mwezi Mei mwaka huu.

IDARA YA MAWASILINO, IKULU ZANZIBAR

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Hussein Ali Mwinyi akizungumza na Ujumbe wa Tume ya Kuangalia jinsi ya kuboresha Taasisi  za Haki Jinai Tanzania,ukiongozwa na Mwenyekiti wa wake Jaji Mkuu Mstaafu wa Tanzania Mhe. Mohamed Chande Othman (kulia kwa Rais) ulipofika Ikulu Jijini Zanzibar  kwa mazungumzo na kujitambulisha.
Baadhi ya Wajumbe wa Tume ya Kuangalia jinsi ya kuboresha Taasisi  za Haki Jinai,wakimsikiliza  Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Hussein Ali Mwinyi (hayupo pichani) wakati alipozungumza na Tume hiyo walipofika Ikulu Jijini Zanzibar leo  Kujitambulisha.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Hussein Ali Mwinyi (kulia) akiagana na Mwenyekiti wa Tume ya Kuangalia jinsi ya kuboresha Taasisis za Haki Jinai Mhe. Jaji Mkuu Mstaafu Mhe.Mohamed Chande Othman,baada ya mazungumzo na Tume hiyo  ilipofika Ikulu Jijini Zanzibar leo  Kujitambulisha.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.