Habari za Punde

Kongamano la Uhuru wa Vyombo vya Habari Zanzibar

Mkurugenzi Mtendaji Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake TAMWA - Mainland Dkt. Rose Reuban akizungumza wakati wa majadiliano juu ya  uongozi  na wanawake kwenye  kongamano la wanahabari liliofanyika Ukumbi wa Golden Tulip kuelekea kilele cha Miaka 30 ya siku ya uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani,huko Uwanja wa Ndege Zanzibar.Mei 2 ,2023 PICHA NA YUSSUF SIMAI-MAELEZO ZANZIBAR

Na Rahma Khamis, Maelezo

Waandishi wa habari wanawake wametakiwa kutangaza mazuri yanayofanywa na viongozi wanawake ili kuwahamasisha wanawake wengine  kuwania nafasi hizo.

Akizungumza katika mjadala maalum ulioandaliwa kuelekea kilele cha maadhimisho ya siku ya uhuru wa vyombo vya habari katika Ukumbi wa Golden Tulip  Mkurugezi  wa Chama cha waandishi wa Habari wanawake Tanzania TAMWA  Rose Ruben amesema wanawake wengi wanakosa haki ya kuwania uongozi kutokana na utii na unyenyekevu uliojengeka kwao kulingana  na mila na desturi zao .
Amesema wanawake wana haki ya kuwa viongozi katika majimbo na sehemu nyengine kwani ni halali kwao  hivyo ni wajibu wao kujitoa kushika nafasi hizo zitakazoleta maendeleo kwa jamii na taifa kwa ujumla.
Aidha amefahamisha kuwa ingawa wameanza kujitokeza kuwania baadhi ya nafasi lakini hali ya kujitokeza kwao si ya kuridhisha kwani wengi wao wanakua na hofu jambo ambalo linarejesha nyuma harakati za kutaka kuwainua  kimaendeleo wanawake hao.
Nae Mkurugenzi wa chama cha waandishi wa Habari wanawake Zanzibar Dokta Mzuri Issa amefahamisha kuwa kwa miaka mingi wanawake wa Zanzibar walikuwa hawashiriki katika kuwania nafasi za uongozi jambo ambalo limewakosesha fursa nyingi za kimaendeleo.
Aidha amefahamisha kuwa wanawake wengi wanaingia Barazani kwa kutegemea nafasi za viti maalumu jambo ambalo linarejesha nyuma juhudi za kupata nafasi hizo na haipendezi kwani inaonekana ni huruma kutoka kwa wanaume ambazo zimepelekea kuwachagua.
Nao washiriki wa mjadala huo wamesema kuwa baadhi ya wanawake wanawarejesha nyuma wanawake wenzao kwa kuwapakazia mambo machafu ambayo hayana ukweli ndani yake kwa lengo la kuwakosesha nafasi hizo.
"kuna baadhi ya wanawake waanawarudisha nyuma wenzao kwa maslahi binafsi ili wasiendelee ,hivyo tusiipe nguvu misemo  yenye dhana potofu kama  adui wa mwanamke ni mwanamke mwenziwe kufanya  hivi sio sawa kwani akifanikiwa mwanamke mmoja imefanikiwa jamii nzima."walisema Washiriki hao.
Aidha amewashauri  waandishi wa habari wanawake kujikita zaidi katika kuhamasisha wanawake wenzao katika kushiriki katika mambo mbalimbali ya uongozi na kutokata tamaa katika kupambana na afasi hizo.
Hata hivyo washiriki hao wamewataka wanawake na wanahabari kujitoa ,kujituma na kujiamini katika  kupigania nafasi mbalimbali za uongozi kwani wanawake wanaweza.
Kongamano hilo la siku mbili linatarajiwa kufikia kilele chake kesho likiwa na ujumbe usemao "KUUNDA MUSTAKBALI WA UHURU WA KUJIELEZA KUWA KAMA KICHOCHEO CHA HAKI ZA BINAADAMU "

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.