Habari za Punde

Siku ya Uanuai Duniani Yaadhimishwa Mkoani Dodoma

Na Brown Jonas

Wizara ya Utamaduni Sanaa na Michezo imeadhimisha kilele cha Siku ya Uanuai wa Utamaduni katika Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) ambayo huadhimishwa duniani kote tarehe 21 Mei kila mwaka.

Akizungumza wakati wa maadhimisho hayo Mkurugenzi wa Maendeleo ya Utamaduni wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt. Emannuel Temu amesema Serikali imeamua kuadhimisha siku hiyo kwa kuandaa kongamano la Wanazuoni ili kupata uelewa wa pamoja kuhusu dhana ya Siku ya Uanuai wa Utamaduni unavyohusianishwa na Maendeleo Endelevu kwenye muktadha wa jamii na makabila mbalimbali nchini.

“Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo imeona ni vyema iandae kongamano hili muhimu kwa kuendesha mjadala kwa Wanachuo na Wanazuoni kwa kufanya mawasilisho ya mada na mijadala kwa lengo la kujenga  uelewa wa pamoja kuhusu dhana ya Siku ya Uanuai wa Utamaduni Duniani” Amesema Dkt.Temu

Dkt. Temu amewaasa washiriki wa kongamano hilo kutoka Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Chuo cha Mipango na Chuo cha Mt. Yohana wazingatie mila na desturi za Kitanzania ili kulinda tamaduni.

Hii ni mara ya tatu kwa Serikali kuadhimisha siku hiyo ambayo imekua chachu ya kutoa elimu sahihi juu ya maadili na utamaduni kwa jamii hususani kundi la vijana.


No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.