SERIKALI ya Mapinduzi
ya Zanzibar imesema inajitahidi kupambana maeneo tofauti ili ifanikishe miradi
yake iliyoidhamiria kuifanikisha kwaajili ya kuendelea kuwaletea Maendeleo wananchi wake.
Rais wa Zanzibar na
Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi ameyasema hayo Ikulu,
Zanzibar alipozungumza na Mwakilishi Mkaazi wa Shirika la Maendeleo la
Umoja wa Mataifa (UNDP) nchini Tanzania, Bi. Christine Musisi aliefika
kumtembelea.
Dk. Mwinyi alisema
daima Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inalishukuru Shirika la Kimataifa la
UNDP kwa kuendelea kuiunga mkono Serikali kwenye masuala mbalimbali ya
maendeleo.
Alisema SMZ na UNDP
wana ushirikiano mzuri na kulipongeza Shirika hilo kwa kuendelea kuiunga Mkono
Tanzania ikiwemo Zanzibar hasa kwa kuiongezea nguvu za kifedha Taasisi ya Ufuatiliaji
na Usimamizi utendaji kazi Serikalini, PDB, Zanzibar.
“Tunahitaji
kuiwezesha zaidi PDB ili kuhakikisha inafanikisha ipasavyo majukumu yake” alieleza
Rais Dk. Mwinyi.
Rais Dk. Mwinyi
alimwelezea mgeni wake huyo ushirikiano anaoupata kwa PDB katika kutekeleza
majukumu yake, hivyo aliipongeza UNDP kwa kuiunganga mkono.
Alisema Serikali
imeweka nguvu zake huko bila ya kutegemea bajeti kutoka Serikali kuu pekee
badala yake inahangaika kwa wadau mbalimbali wa maendeleo ili kuiongezea bajeti.
Aidha Rais Dk. Mwinyi
aliridhia ombi la UNDP la kukutana pamoja kwa baadhi ya Mabalozi ambao ni wadau
wa maendeleo wa shirika hilo wakiwemo Canada, Uingereza na Norway.
Akizungumza kwenye
hafla hiyo, Mwakilishi huyo wa UNDP, Christine Mwasisi alimpongeza Rais Dk.
Mwinyi kwa uongozi wake wa kuendeleza amani na kuendelea kuimarisha uchumi wa
Zanzibar.
Alimueleza Rais Dk.
Mwinyi UNDP kwasasa inatekeleza miradi sita barani Afrika ikiwemo mitatu kwa
Tanzania ambapo Zanzibar wanashirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar
katika kutekeleza miradi ya kupambana na matukio ya Uhalifu Zanzibar, ambapo
alieleza mradi huo wanashirikiana na Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka chini ya
ufadhili wa Serikali ya Uingereza na Umoja wa Ulaya (EU).
Alieleza mradi
mwengine ni uwezeshaji kwenye masuala ya utawala wa kisheria ambapo alieleza
mradi utaangalia haki na wajibu kwenye masuala ya jinsia ikiwemo masuala ya
wanawake na watoto ambapo alieleza mradi huo unatarajiwa kushirikiana na Baraza
wa Wawakilishi Zanzibar.
Pia Bi. Mwasisi
alieleza mradi mwengine utahusisha masuala ya fedha ambao Mwakilishi huyo alisema
tayari timu ya mradi huo imeshakutana na Waziri wa Fedha wa Zanzibar Dk. Saada Mkuya
Salum na kujadiliana kwa hatua za awali na wadau wa wizara hiyo.
Aidha, mbali na mambo
mengine pia mgeni huyo alimueleza Rais Dk. Mwinyi kwamba UNDP ilivyojipanga
kufanyakazi na Sekta ya Uchumi wa Buluu pamoja na sekta ya Mazingira endelevu.
IDARA YA MAWASILINO, IKULU ZANZIBAR
No comments:
Post a Comment